loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Majarida ya maadili kujenga taasisi kimaadili

Wiki iliyopita, tuliangalia namna mafunzo ya maadili yanavyoweza kusaidia katika kujenga taasisi kimaadili, kwa kuhakikisha kuwa mafunzo stahiki kuhusiana na suala zima la maadili yanawafi kia watumishi wote, ili wawe tayari kutekeleza majukumu yao kulingana na matakwa ya kanuni za maadili.

Katika toleo hili, tunaangalia namna majarida (newsletters) ya maadili yanavyoweza kusaidia katika kujenga taasisi kimaadili, kwa kuhakikisha kuwa habari mbalimbali kuhusu maadili zinawafikia watumishi wote, ili wawe tayari kutekeleza majukumu yao kulingana na matakwa ya kanuni za maadili.

Kwa jumla jarida la maadili lina umuhimu mkubwa kwa vile linawafanya waatumishi wawe na uelewa mkubwa kuhusu maadili na kuwafanya watumishi hao waweze kuchukua hatua mbalimbali za kimaadili kulingana na uelewa wao.

Uelewa mkubwa wa mambo haya ya maadili unatokana na matumizi ya jarida husika, ambapo jarida linaweza kutumika kama jukwaa la kuzungumzia kanuni mbalimbali za maadili ya utumishi wa umma na maadili ya kitaaluma, kwa minajili hiyo hiyo ya kujenga uelewa wa kanuni hizo kwa watumishi.

Mwanazuoni Ross na wenzake, walipata kuandika makala yao ya mwaka 1993 ambapo pamoja na mambo mengine, walibainisha kuwa majarida ya maadili yanaweza kutumika kwa ajili ya kundika mambo mbalimbali kama vile sera na mada tata za maadili na kueleleza nini taasisi inaweza kufanya ili kuweka mambo sawa.

Aidha, jarida la maadili linaweza kutumika kuandika kuhusu mtanziko (njiapanda) wa maadili na namna mtanziko huo unavyoweza kutatuliwa.

Mambo haya ni muhimu sana hususan pale ambapo mtumishi katika kufikia maamuzi anaweza akajikuta na mambo mawili tu ya kuchagua na kila moja kati ya mambo hayo lina ubaya wake na uzuri wake kimaadili.

Jarida la maadili linaweza kutumika pia kuwatambulisha watumishi wote wenye dhamana ya maadili kwa watumishi wengine. Itakumbukwa kwamba taasisi ya umma inatakiwa kuwa na watu maalumu wanaoshughulikia masuala ya maadili.

Watu hawa ni kama maafisa maadili, wajumbe wa kamati za maadili na mamlaka za nidhamu na ajira za taasisi husika. Pia jarida hili la maadili ni muhimu sana kwa sababu linaweza pia likasaidia sana, kuwajulisha watumishi juu ya shughuli mbalimbali za kimaadili ambazo zimefanyika au zinatarajiwa kufanyika katika taasisi husika.

Kwa mfano jarida linaweza kuandika kuhusu mafunzo ya maadili yanayotarajiwa kutolewa kwa watumishi wote.

Jarida la maadili vilevile linaweza kutumika kuwajulisha watumishi juu ya mambo ambayo ni tishio kwa maadili ndani ya taasisi husika na utumishi wa umma kwa ujumla, ili watumishi hao waweze kuchukua tahadhari mapema kabla ya madhara kujitokeza.

Vilevile jarida la maadili linaweza kutumika kuzungumzia mada mbalimbali muhimu kamavile uongozi wa maadili, utamaduni wa taasisi, kamati za maadili na mawasiliano kuhusiana na mambo ya maadili, ili kuondoa ukimya kwenye suala zima la maadili na kuwafanya watumishi ndani ya taasisi husika kukua kimaadili.

Kwa kuzingatia umuhimu wa jarida la maadili katika taasisi ya umma, ni wazi kuwa linahitahijika jarida zuri la maadili. Ili taasisi iweze kuwa na jarida zuri la maadili, kuna mambo mengi ya kuzingatia, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa jarida husika lina timu nzuri ya kuandaa jarida la maadili, ili kulifanya jarida hilo kukidhi vigezo muhimu.

Vilevile ni muhimu muda wa maandalizi ya jarida hilo ukawa unajulikana vizuri na wadau mbalimbali, ili waweze kuchangia kwa kuzingatia muda, pale wanapohitaji kuchangia mambo muhimu kuhusu maadili.

Vilevile ni muhimu ikajulikana kwa watumishi, kuwa jarida la maadili linatoka mara ngapi kwa mwaka na lini ili wasomaji waweze kufuatilia na kuhakikisha kuwa wanayapata majarida hayo na kuyasoma kila mara yanapotoka.

Waandaaji ni lazima wahakikishe kuwa kuna maelekezo ya kutosha kuhusu namna bora ya kuandaa makala kwa wale wanaochangia na maelekezo hayo yawafikie wadau wa jarida hilo kwa muda mwafaka, ili maandalizi ya jarida katika kila toleo yakamilike kwa wakati mwafaka.

Kwa kumalizia, ni vizuri ikafahamika kwamba ziko njia nyingi za kuwasilisha masuala ya kimaadili kwa wadau na kwa maana hiyo ni muhimu kwa wahusika kuangalia ni mambo gani yanafaa kwenda kwenye jarida la maadili na mambo gani yanafaa kutumia njia mbadala.

Hoja hii inaungwa mkono na mwanazuoni mwingine wa maadili, Murphy, ambaye katika makala yake ya mwaka 1988 alipata kusema kuwa, siyo kila jambo la kimaadili linatakiwa kuwekwa katika jarida la maadili, kwavile mambo mengine yanaweza kuachwa yaingie katika mfumo usiokuwa rasmi.

foto
Mwandishi: Dk Alfred Nchimbi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi