loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Fundisheni kwa mbinu bila kuchuja wanafunzi’

MAFUNZO ya uongozi na usimamizi wa elimu ni moja ya njia inayotoa fursa kubwa kwa viongozi ngazi ya shule katika kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kuongoza na kusimamia shughuli za shule.

Mfumo huu pia unatoa fursa kubwa kwa viongozi wa ngazi hizo kusimamia taaluma na kuleta matokeo chanya katika nyanja za uongozi na usimamizi wa shughuli.

Kumekuwepo na mawakala mbalimbali wa serikali nchini ukiwemo Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) ambao umekuwa ukitoa mafunzo ya aina hiyo kwa wakuu wa shule za sekondari za serikali na binafsi.

Mafunzo yanalenga kubadilishana mawazo ya namna bora ya kuboresha utendaji shuleni sambamba na kutoa maelekezo ya utendaji kazi ili kutoa elimu bora, kubadilishana mawazo ya namna bora ya kuboresha utendaji shuleni na kutoa maelekezo ya utendaji kazi.

Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari Balili iliyopo Mbagala Kuu, Temeke, Mwalimu Lucas Hassan, anasema kupitia njia hiyo, amejifunza mambo mengi ya uongozi katika taaluma hiyo.

Anasema kupitia uzoefu kwa nafasi ya ukuu wa shule katika shule mbalimbali nchini, ameshiriki mafunzo ya uongozi na usimamizi kutoka kwa wadau na kubaini upungufu mbalimbali unaowanyima fursa baadhi ya Watanzania haki yao ya kupata elimu.

Hassan ambaye pia ni mwalimu wa masomo ya Bayolojia na Kemia, anasema alibaini sera za shule nyingi za binafsi zimekuwa zikimnyima fursa mwanafunzi mwenye uelewa mdogo kupata haki yake ya msingi ya kupata elimu, kwa kuwaondoa wote ambao watakuwa hawajafikia viwango vilivyowekwa na shule.

Anasema kwa kutambua umuhimu wa wanafunzi wa Kitanzania kuwa na haki sawa ya kupata elimu bora, Shule ya Sekondari ya Balili inayo mikakati mbalimbali ya kuwezesha wanafunzi wote kupata elimu bora ili kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na maendeleo ya viwanda nchini kwa kubuni mbinu mbalimbali za kuwainua kielimu.

Mkuu wa shule hiyo, Richard Mgonja, anasema badala ya kubagua wanafunzi kwa kuchuja ili kupata na kufundisha wenye uwezo mkubwa hali ambayo wakati mwingine huzipa baadhi ya shule umaarufu usiostahili, shule yao haibagui wanafunzi kama baadhi ya shule binafsi zinavyofanya, badala yake imekuwa ikiwachukua wanafunzi wote wanaofundishika ili wote wainuke kitaaluma na kutimiza haki na ndoto zao za kupata elimu bora.

“Ndiyo maana licha ya kwamba huwa tunaandaa na kuwafanyisha watoto mitihani ya mara kwa mara ili kuwapa uzoefu kwa kuwaondolea woga wa mitihani sambamba na kuwapa mbinu bora za kuchagua na kujibu maswali, pia tuna utaratibu wa mwanafunzi mmoja mmoja kumjenga kisaikolojia ili aweze kuendelea kumudu masomo yake na aweze kufanya vizuri katika mitihani yake,” anasema.

“Uongozi wa shule umeunda bodi inayoitwa Balili Examination Board (BEB) inayofanya kazi ya kutunga mitihani ya kila mwisho wa mwezi na kuwapatia walimu waweze kuwapa wanafunzi, na wanafunzi waliofanya vizuri na wale walioonesha juhudi kitaaluma kwa kupanda hatua moja hupatiwa motisha mbalimbali zikiwepo fedha,” anasema Mgonja.

Kuhusu ushirikiano na jamii, anasema: “Tunawashukuru wazazi na walezi kwa ushirikiano wanaouonesha kwetu kwa kuitikia mwito pale wanapohitajika kufanya hivyo.” Anaomngeza: “Hili ni jambo jema ili watoto wetu wazidi kunufaika na sera ya taifa ya elimu bila malipo hali ityakayoliwezesha taifa kuwa na wataalamu watakaoungana na azima ya serikali kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda.”

Mwalimu Mgonja anasema shule hiyo imejipanga kuzalisha wataalamu wa kutosha katika masomo ya sayansi ili kuunga mkono serikali katika kuzalisha wataalamu wa fani hiyo.

“Shule yetu inasimamia maadili ya watoto ipasavyo kazi ambayo tumekuwa tukiifanya kwa kushirikiana na viongozi wa elimu kutoka ofisi ya elimu ngazi ya kata sambamba na viongozi wa dini waliopo eneo shule ilipo,”anasema Mgonja na kuongeza kuwa, wanafunzi wamekuwa wakifundishwa uzalendo ili waweze kukua na kuendelea kuilinda amani ya nchi.

Anasema wanaangalia namna ya kuwasaidia watoto wanaotoka katika familia zisizojiweza kwa kutoa punguzo la ada au kuwasomesha bure ili kuwawezesha kutimiza ndoto zao za kupata elimu.

Walimu hao wanatoa mwito kwa serikali kuhakikisha shule zote hasa za binafsi, zinakuwa na mbinu za bora zaufundishaji ili kusaidia wanafunzi wote, badala ya kuchuja wanafunzi na kuwaacha wenye uwezo mdogo au wa kawaida.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments