loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Waziri Kairuki aomba kiwanda kizalishe gesi za hospitali

WAZIRI wa Nchi Ofi si ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angela Kairuki (pichani) amekiomba kiwanda cha kuzalisha chuma na mabomba cha Lodhia Group cha wilayani Mkuranga mkoani Pwani kuzalisha kwa wingi gesi kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa hospitalini.

Kairuki aliyasema hayo kwenye kiwanda cha Lodhia alipokitembelea kujua mafanikio na changamoto zinazovikabili viwanda vilivyopo mkoa wa Pwani. Kairuki alisema kuwa kutokana na kiwanda hicho kuzalisha gesi kwa ajili ya shughuli zao kiwandani hapo ni vema wakazisaidia na hospitali mbalimbali.

“Tumefurahi kuona mmeanza kusaidia baadhi ya hospitali. Hili ni jambo jema. Tunaomba msaidie gesi hospitali zetu kunusuru wagonjwa,”alisema. Alisema huduma ya gesi kwa wagonjwa hospitalini ni muhimu hivyo ni vema wakatoa huduma hiyo ya kijamii kama sehemu ya mchango wao kwa jamii.

“Serikali ndio inataka wawekezaji kama hawa ambao mbali ya uzalishaji wanasaidia jamii na kuinua pato la Taifa kupitia kodi na tozo,” alisema.

Aidha alisema taasisi wezeshi zinapaswa kutoa elimu badala ya kuwa maadui kwani wanapaswa kushirikiana nao na si kuwatisha na kuwapiga faini zisizokuwa na sababu,”alisema Waziri Kairuki.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Sailesh Pandit alisema mapato wanayoyatoa serikalini kutokana na tozo ni Sh bilioni 35 hadi 40 kwa mwaka.

Pandit alisema kwa sasa wameanza kutengeneza nondo zenye unene wa milimita 40 ambazo zinatumika kwenye ujenzi wa daraja la Salender na mradi wa umeme wa Nyerere katika Mto Rufiji.

Kiwanda hicho kilianza uzalishaji mwaka 2002 na kimetoa ajira rasmi 1,500 na zisizo rasmi 3,000.

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: John Gagarini

Post your comments