loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Tanzania itafuzu kombe la dunia 2022’

BAADHI ya makocha na wachambuzi wa soka nchini wamesema Tanzania haipaswi kuwaogopa wapinzani waliopangwa kundi moja katika michuano ya kufuzu Kombe la Dunia Qatar 2022 bali kuwaheshimu.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) juzi lilipanga makundi ya kufuzu kombe la dunia, tukio lililofanyika nchini Misri na Tanzania ikaangukia kundi J, lenye timu za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Benin na Madagascar.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi makocha na wachambuzi walisema Tanzania ina nafasi ya kufanya vizuri kinachotakiwa ni kuheshimu wapinzani kwa sababu wana wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya Bara la Afrika.

Kocha Keneth Mkapa anayefundisha Mji Njombe ambayo inacheza Ligi Daraja la Kwanza alisema chochote kinaweza kutokea kwa sababu Tanzania kuna wachezaji wengi wazoefu wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi tofauti na siku za nyuma.

“Kuogopa hakupo tunapaswa kuwaheshimu kwa sababu wote tuna wachezaji wanaocheza nje, kuna akina Simon Msuva, Mbwana Samatta, tukijipanga kama tulivyofanya hivi karibuni tutafanikiwa,” alisema.

Naye Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ alisema kundi hilo sio gumu kinachotakiwa ni kupambana na kupata matokeo mazuri katika mechi zote kwasababu vijana siku hizi wanapata hamasa kutoka kwa wachezaji wakongwe ni jukumu lao kujitangaza kwa kujituma.

“Mimi sioni kama tumepangwa kundi gumu, tupo kwenye kiwango cha kimataifa, tuna Samatta anayecheza Aston Villa na Msuva aliyeuzwa Ureno, yeyote anayekuja mbele yetu ni mchezaji sawa na wa kwetu,”alisema.

Naye mchambuzi wa soka, Ally Mayai alisema Tanzania inazimudu timu hizo, kinachotakiwa ni kupambana kushinda mechi zote za nyumbani na kuingia hatua ya pili kutasaidia kuiweka nchi katika kiwango bora duniani.

“Mchakato ni mgumu kwa sababu nchi zinazokwenda ni tano na inayotakiwa katika kundi ni moja tu hivyo kuwe na mpango wa kuhakikisha wanashinda mechi zote za nyumbani,”alisema mchezaji huyo wa zamani wa Yanga

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments