loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM ataja kinachomtesa, Lugola njiapanda

RAIS John Magufuli amesema Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye hawafai kuhudumu tena katika nyadhifa zao baada ya kukubali kusainiwa mkataba wa Euro milioni 408 na kampuni moja ya Ulaya bila kuidhinishwa na Bunge.

Amesema kuwa mkataba huo ambao haupo kwenye bajeti umesainiwa na Jenerali Andengenye ambao una masharti makubwa endapo ungevunjwa.

Rais Magufuli amesema kuwa anawapenda viongozi hao lakini kwa kusainiwa mkataba huo usio na manufaa kwa taifa ni dhahiri kuwa hawakupaswa kuwepo katika hafla ya kukabidhi nyumba za askari na maofisa wa Magereza leo Ukonga, jijini Dar es Salaam.

“Kama kuna kitu kinachonitesa na Wizara ya Mambo ya Ndani,” alisema Rais huku akielezea sakata la mkataba huo tata wa zaidi ya Sh trilioni moja. “Lugola nakupenda sana, ni mwanafunzi wangu nilimfundisha shule ya sekondari Sengerema lakini kwenye hili hapana,” aliongeza huku akitoa kauli kama hiyo kwa Kamishna Andengenye.

Hata hivyo, Rais ameridhia ombi la Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo, Meja Jenerali, Jacob Kingu kujiuzulu huku akimwagia sifa kwa uamuzi huo.

Mbali na kuwataja viongozi hao waandamizi, Rais aliigeukia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa kuwataka waliohusika katika sakata hilo la utiaji saini kujitathmini na kuchukua hatua.

Rais amesema serikali itaendelea kuboresha makazi askari na wanajeshi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wao.

Amelitaka Jeshi la Magereza kubadilika na kuiga Jeshi la Kujenga Taifa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi