loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simbachawene amrithi Lugola

RAIS Dk John Magufuli baada ya kutengua uteuzi wa nafasi kadhaa za viongozi wa Serikali katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutokana na kusaini mkataba usio na tija kwa nchi, amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.

Dk Magufuli amemteua Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, George Simbachawene kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Simbachawene amechukua nafasi ya Kangi Lugola ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais jana.

Wakati Rais akimteua Simbachawene kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azan Zungu, ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Pia aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, ambaye jana Rais Magufuli alisema amepokea barua yake ya kujiuzulu, Meja Jenerali Jacob Kingu, ameteuliwa kuwa Balozi.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi alisema Ikulu jana, Dar es Salaam kuwa, Rais amefanya mabadiliko hayo madogo na pamoja na kuteua mabalozi wapya watatu akiwamo Kingu, amewaongezea muda mabalozi saba waliokuwa wakiiwakilisha nchi katika mataifa mbalimbali ambao muda wao ulikuwa umekwisha.

Balozi Kijazi alisema pia kuwa Rais Dk Magufuli ametengua uteuzi wa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye kuanzia jana Januari 23, mwaka huu.

Alisema nafasi yake itajazwa baadaye. “Pia Rais Magufuli ameagiza Takukuru wafanye uchunguzi haraka kuhusiana na mkataba uliosainiwa kati ya kampuni ya kutoka nje ya nchi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambao hauna tija kwa nchi,” alisema Balozi Kijazi.

Mbali na Kingu, mabalozi wengine wapya walioteuliwa na Rais jana ni Dk John Simbachawene kutoka Ofisi ya Rais Ikulu na Kamishna Jenerali Faustine Kasike ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Kamishna Jenerali wa Magereza. Balozi Kijazi alisema nafasi ya Kasike itajazwa baadae na vituo vya mabalozi hao watatu walioteuliwa, vitatangazwa baadae.

Vilevile, Balozi Kijazi alisema Rais amewaongezea muda wa miaka miwili mabalozi saba wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za nje ambao muda wao ulikwisha. Mabalozi hao ni George Madafa (Italia), Paul Mella Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Job Masima (Israel), Dk Emmanuel Nchimbi (Brazil), Dk Asha Rose Migiro, (Uingereza), Benedict Mashiba (Malawi), na Sylvester Mabumba (Comoro).

Alisema tarehe za kuapishwa mawaziri na mabalozi walioteuliwa itatangazwa baadae. Awali jana, Rais Magufuli alitangaza kumuengua Waziri Lugola katika sherehe za ufunguzi wa majengo 12 ya makazi ya familia 172 za maofisa na askari wa Magereza katika gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Magufuli alisema:“Lugola nampenda sana. Ni mwanafunzi wangu nilimfundisha Sengerema sekondari…Lakini kwenye hili hapana. Nilitegemea hata hapa nitakuta hayupo.”

Pia Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias Andengenye alikumbwa na fagio hilo ambalo chanzo ni kutia saini makubaliano ya zabuni ya kununua vifaa vya zimamoto na uokoaji vyenye thamani ya Euro milioni 408.5 (zaidi ya Sh trilioni moja) kutoka kampuni ya nje bila kufuata sheria.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya watu, Rais Magufuli alimpongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu kwa kuandika barua ya kujiuzulu wadhifa wake ikiwa ni uwajibikaji kutokana na sakata hilo.

Wengine ambao Rais Dk Magufuli amewataka wajitafakari kwa kuhusika katika sakata hilo ni maofisa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliohusika kupitisha makubaliano hayo wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi akiwa msibani (alipofiwa na mkewe).

Wamo pia maofisa kutoka Zimamoto. Rais Magufuli aliweka bayana kuwa hakutarajia kuwaona viongozi hao (Lugola na Andengenye) kwenye sherehe hizo za ufunguzi ambazo awali, Waziri Lugola alimsifia na kumpigia debe Rais kwa kutekeleza ipasavyo ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015.

“Nampongeza sana Meja Jenerali Kingu ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kuwajibika, na hii imempa heshima kwamba angalau ametambua kwamba inawezekana haya hakuyafanya mwenyewe lakini kwa kuwa yeye ni katibu mkuu amewajibika kwenye hilo.

“Nitaendelea kumheshimu. Lakini Mheshimiwa Lugola, Kamishna Jenerali Andengenye, ninawashangaa kuwaona mko hapa. Ninawapenda sana lakini huu ndiyo ukweli, sitaki kuwa mnafiki. Urafiki na upendo uko pale pale lakini katika suala la kazi hakuna namna.”

Akirejelea hotuba ya Lugola muda mfupi kabla ya kumtumbua, Magufuli alisema, “Umenisifia sana hapa nakushukuru lakini kwenye hili hapana lazima niwe mkweli sitaki kuwa mnafiki… Andegenye unafanya kazi nzuri sana. Umejenga nyumba hata Chato, lakini kwenye hili ulilolifanya, unakwenda Ulaya unasaini kwa mradi ambao haujapitishwa hata na Bunge, hapana.”

Alisisitiza kuwa mtu yeyote anayetaka kufanya kazi naye ni lazima afanye anavyotaka. “Tusubiri wakati utakapokuja kwa wale (viongozi) watawaona unafanya lolote wanakuangalia tu basi utakuwa utawala wa namna hiyo lakini kwa utawala wangu hapana.”

Akisisitiza kuwa mkataba huo ulikuwa ni wa hovyo, Magufuli alisema “Hatuwezi tukaendesha nchi kwa misingi ya ajabu namna hii. Yanayokwenda kununuliwa kwenye mkataba ni ya hovyo. Mara drones (ndege zisizo na rubani).”

Alisema mwenye mamlaka ya kukopa fedha za nchi ni Wizara ya Fedha peke yake na kwamba hilo linajulikana. Alisema bila kuwa hivyo, kila wizara itakopa na hata yeye atakopa.

Awali, akieleza namna uongozi ulivyo mgumu, Rais Magufuli alisema kati ya wizara zinazomtesa ni ya Mambo ya Ndani.

Kwa mujibu wa rais, katika miaka minne ya uongozi wake, zimeundwa tume nyingi kuchunguza wizara hiyo kutokana na kufanyika miradi aliyoiita ni ya hovyo.

Alisema alitegemea watu watakuwa wanajifunza lakini kikubwa ni kwamba watu wanakosa uadilifu. Akirejelea mkataba huo uliosababisha Lugola na viongozi wenzake kuenguliwa, alisema ulitayarishwa na kusainiwa bila kupangwa kwenye bajeti wala kupitishwa na Bunge .

Alisema wakati wa vikao na kampuni moja ya nje, wahusika wote kutoka Tanzania waliokwenda kwenye majadiliano walilipwa posho ya kikao dola 800 na kulipiwa tiketi za ndege. Mkataba unaeleza kwamba ukitakiwa kuvunjwa, mambo ambayo yameshaanza kutekelezwa lazima yaendelee kutekelezwa.

Lugola azungumza

Alipohojiwa na waandishi wa habari baada ya sherehe hizo za ufunguzi, Lugola alisema hatua zilizochukuliwa dhidi yake ni nzuri zinalenga kujenga vizuri serikali. Alipoulizwa kuhusu tuhuma zilizosababisha kuenguliwe, Lugola alisema,

“Siwezi kurudia mheshimiwa Rais alizungumza na Watanzania pale kwa hiyo mimi sioni sababu ya mimi kurudia tena. Naomba Watanzania waendelee kumuamini Rais, kumuunga mkono katika juhudi za serikali na sisi tutaendelea kumuunga mkono. Aliahidi kupitia ubunge, ataendelea kumsaidia Rais kwa kutumikia serikali kwa heshima akizingatiaheshima kubwa aliyopewa kuongoza wizara hiyo ya mambo ya ndani.

“Kwa hiyo mimi niko vizuri na wala msidhani kuwa kuna shida imenitokea katika hatua hizo. Ni hatua nzuri, njema kabisa naomba muelewe hivyo…Ni kuendelea kuchapa kazi.

“Sisi wabunge wa CCM wakichukuliwa wachache kuunda baraza, na sisi tunakuwa benchi; ni wachezaji wakati wote, tunapiga jaramba tunaweza kuingia na sisi sasa ambao tuko benchi tunaendelea kuwashangilia waendelee kumsaidia Rais hadi watakapomaliza awamu na kuingia kwenye uchaguzi.”

Kabla ya kutumbuliwa Awali kabla ya Magufuli kumuengua, Lugola alimsifia Rais anavyotekeleza ilani ya CCM ya uchaguzi wa 2015 ikiwa ni pamoja na serikali yake kutumia fedha kwa ajili ya maendeleo. Alisema kumewapo watu wanaoona anayofanya ikiwamo ukusanyaji wa fedha zinazopaisha uchumi, lakini hawataki kukubali matokeo.

“Nataka niwahakikishie ibara ya 146 (5) uliwahakikishia Watanzania kwamba vyombo vya ulinzi na usalama utavipatia makazi kwa ajili ya kujenga ari na molari kwa askari kwa ajili ya kuendelea kulinda nchi hii amani na usalama.

“Wale wanaoendelea kubeza juhudi zako mheshimiwa Rais, ambao wanaona kwamba macho yao hayaoni lakini tunawaambieni, siku za serikali ya awamu ya tano zinakaribia mwisho. Watanzania wenye imani, Watanzania wenye moyo wanaokuunga mkono ni asilimia 99.1.

“Hako 0.1 ni wale ambao mioyo yao imeshikiliwa na adui shetani. Lakini kwa jina la Yesu mwana wa Mungu aliye hai walegee na ninawafunga minyororo ya upofu ili na hiyo asilimia waweze kukubali kazi unayoifanya,”alisema. Aliongeza kuwa Rais Magufuli ataendelea kuwa juu zaidi.

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha na Stella Nyemenohi

Post your comments