loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wawakilishi wapongeza ubunifu TSN

KAMATI ya Kudumu ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, imeipongeza kampuni ya magazeti ya serikali (TSN) kwa kuja na mbinu mpya za kujiendesha kibiashara.

Kwa sasa kampuni hiyo inayozalisha magazeti ya HabariLEO, Daily News na SpotiLeo, imekuja na miradi mipya ikiwamo kuwa na shirika la habari (news agency) litakaloandaa habari na kuziuza kwa vyombo vingine vya habari ndani nan je ya nchi.

Pamoja na hayo, kampuni hiyo ya TSN imekuja na mradi wa uchapishaji kidigitali, kuwa mshauri wa masuala ya habari, kupiga picha kibiashara na kutengeneza dokumentari.

Akizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo kwa kampuni ya TSN jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Musa Foum Musa, alisema ubunifu huo wa TSN utaiwezesha kampuni hiyo kujiongezea mapato, lakini pia kufikia lengo la kuwahabarisha Watanzania habari kutoka maeneo mbalimbali ikiwamo vijijini.

“Tunaomba tu hii miradi mingine mnayofikiria kuianzisha muanze kuitekeleza haraka ili kama kuna watu wanaotaka hata kuwaiga ikiwamo sisi Zanzibar tuwaige. Maana hata wahenga walisema chema chajiuza,” alisema.

Kaimu Meneja wa kiwanda cha uchapishaji cha TSN, Boniface Mwajombe, akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mhariri Mtendaji wa kampuni hiyo, Tuma Abdallah, alisema mipango na mikakati hiyo ina lenga kukuza kipato cha kampuni hiyo, lakini pia kuwa chombo bora na cha kuaminika cha habari nchini.

“Vision (dira) ya kampuni yetu ni kuwa chombo kinachokubalika na kuaminika nchini. Tunataka TSN iwe mouth piece (mdomo) wa serikali, kuelezea sera za serikali, kuwawezesha wananchi kupata habari kuhusu nini serikali yao inafanya na kuchukua mawazo ya wananchi na kuyachapisha kwenye vyombo vyetu vya habari,” alisema.

Mwajombe alisema TSN ina amini katika kasi na teknolojia kutokana na mabadiliko ya duniani, ubunifu wa miradi mipya na kutumia njia rahisi kufanya biashara na kufikia masoko na umma ili wateja na wadau wapate bidhaa zenye ubora na kwa muda muafaka.

Ametoa mfano namna TSN ilivyomuinua mwanafunzi wa Simiyu, aliyefanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha nne licha ya kusoma katika mazingira duni, hali iliyosababisha sasa kijana huyo kupata misaada mbalimbali ikiwamo kuendelezwa kielimu na wazazi wake kujengewa nyumba na wadau mbalimbali.

“Katika eneo la ubunifu, TSN inataka kuwa shirika la habari, mradi wa uchapishaji ikiwamo uchapishaji wa kidijitali, huduma ya ushauri, kupigapicha kibiashara na kuziuza kwa wateja na kutengeneza dokomentari.”

“Katika eneo hili la dokomentari tunawakaribisha wabunge na wawakilishi kupitia mradi wetu wa jimbo kwa jimbo hasa kipindi hiki cha uchaguzi. Hii ni fursa ya kuitumia ili watu wajue kiongozi wao amefanya nini kipindi chote cha uongozi wake,” alisema.

Mwanjombe alieleza namna kampuni hiyo ya magazeti ya serikali inavyoshirikiana na Wakala wa Uchapaji ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Shirika la Magazeti ya Serikali (SMS).

Alisema ushirikiano huo ulianza zamani kwani wamekuwa wakishirikiana kitaaluma, ambapo wamekuwa wakibadilishana ujuzi, lakini pia kwa TSN imekuwa ikichapisha gazeti la Zanzibar Leo.

“Mara ya mwisho kuchapisha Zanzibar Leo ilikuwa mwaka 2016 lakini kwa bahati mbaya tulikuwa tunadai zaidi ya Sh milioni 300, lakini walipunguza hadi kufikia Sh milioni 289, tunaomba wapunguze angalau Sh milioni 10 au 20 kila mwezi,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Saleh Mneno, alikiri kufahamu deni hilo na kuahidi kukutanisha pande zote mbili TSN na SMS ili kuangalia namna ya kulilipa.

KAMPUNI ya uchimbaji ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments