loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Watoa huduma za fedha wabanwa

BAADHI ya kampuni za simu za mkononi zimeweka bayana idadi ya wateja wao waliozimiwa mawasiliano baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuanza kuzima laini za simu zisizosajiliwa kwa alama za vidole mwanzoni mwa wiki.

Aidha, mawakala wanaotoa huduma za fedha kwa njia za mtandao za M-pesa na Halopesa, ambao wanatumia laini zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine, wametakiwa kwenda kujisajili upya kwa alama za vidole kwa kutumia majina yao au kwenda na barua ya mtu mwenye laini hiyo ikielekeza anataka kubadili usajili.

Miongoni mwa kampuni zilizoweka bayana idadi ya wateja wao waliofungiwa laini ni VodaCom Tanzania na Halotel, huku kampuni nyingine hususan Airtel zikisema suala hilo waulizwe TCRA kwa kuwa ndiyo wenye jukumu la kutoa takwimu hizo.

Gazeti hili liliwasiliana na Ofisa Mwandamizi Mkuu wa TCRA, Semu Mwakyanjala, ili kupata taarifa hiyo, lakini naye alisukumia mpira huo kwa kampuni za simu kwamba ndiyo wanaopaswa kutoa takwimu za idadi ya wateja wao waliozimiwa laini kwa kutosajili kwa alama za vidole.

Mbali na laini hizo, pia mawakala wa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu yaani M-Pesa na Halopesa ambao hawakujisajili nao wamefungiwa.

Hatua hiyo imetokana na agizo la TCRA kuziagiza kampuni zote za simu nchini kufunga laini za wateja ambao wameshindwa kusajili laini zao kwa kutumia alama za vidole mpaka Januari 20, mwaka huu.

Akizungumzia uamuzi huo wa serikali, Mkurugenzi Mtendaji wa VodaCom Tanzania PLC, Hisham Hendi, alisema wateja 157,000 wa kampuni hiyo ni miongoni mwa watu 975,000 waliozimiwa laini na TCRA, huku Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Kampuni ya Halotel, Mhina Semwenda, akisema wateja 99,000 wa kampuni yao nao ni miongoni mwa waliofungiwa laini zao.

Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mbando, alisema jukumu la kutoa takwimu hizo ni la TCRA kwa kuwa wanajua ni wateja wangapi wakampuni hiyo walioazimiwa laini kwa kutosajili kwa alama za vidole.

Kwa upande wake, Hendi aliwataka wateja wa Vodacom waliofungiwa laini kutembelea vituo vya huduma au mawakala wa kampuni hiyo zaidi ya 35,000 nchini kusajili laini zao ili waendelee kutumia huduma za kampuni hiyo.

Hendi aliwataka wateja wao ambao hawajapata namba za utambulisho kutoka NIDA, waendelee na mchakato wa kupata namba hizo au vitambulisho vitakavyowawezesha kujisajili kwa kutumia alama za vidole na kuepuka usumbufu wa kufungiwa huduma.

Aliwataka wateja hao kutambua kuwa usajili kwa alama za vidole utapunguza idadi ya matapeli wanaosumbua wateja kwa kuwa kujisajili kwa biometria kutamtambulisha kila mtumiaji wa simu na hivyo kurahisisha vyombo vya usalama kupambana na matapeli.

M-Pesa, Halopesa Kuhusu huduma ya M-Pesa, Hendi alisema kwa kuwa usajili huo umehusisha pia mawakala wa huduma hiyo waliokuwa wakitumia laini za watu wengine, nao sasa wanatakiwa kuzisajili kwa majina yao ili kujiweka katika mazingira salama.

Aliwataka mawakala waliokuwa wakitumia laini za watu wengine kufika katika vituo vya usajili wakiwa na barua zinazoonesha kuwa wamepatiwa namba hizo na watu wenye namba hizo ili kubadilisha usajili na kupewa wao kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja, Harriet Lwakatare, aliwataka wateja kujipatia namba za utambulisho wao watakazozitumia kujisajili kwa alama za vidole kwa kupiga *152*00# au kutuma ujumbe mfupi kwenda namba 15096.

Mawakala wa Halopesa, nao wametakiwa kujisajili upya kwa alama za vidole kwa kutumia majina yao yaliyopo kwenye kitambulisho cha taifa.

Semwenda alisema kampuni ya Halotel ilianza muda mrefu kuwasajili mawakala wa Halopesa kwa kutumia kitambulisho cha taifa na walioshindwa kufanya hivyo walifungiwa huduma na kwamba usajili wa Halopesa kwa alama za vidole bado unaendelea.

Baadhi ya mawakala wa M-Pesa waliozungumza na gazeti hili akiwamo, Juma Nangole wa Buguruni, walisema wamekuwa wakitumialaini ya M-Pesa zisizokuwa zao walizonunua au kuazimwa na watu wengine.

Wakala Beatrice Haroon anayefanya shugughuli zake eneo la Tazara, Dar es Salaam, alisema usajili wa laini ya M-Pesa kwa jina lake umemuondolea usumbufu aliokuwa akiupata kutokana na awali laini hiyo kuwa na jina la kiume huku yeye ni mwanamke na hivyo ilikuwa ikiwatatiza waliokuwa wakitoa fedha kwake.

Matapeli waendelea Wakati uzimaji wa laini ukiendelea, mwananchi mmoja jijini Dar es Salaam alilieleza gazeti hili kuwa, jana alitumiwa ujumbe unaomtaka kutuma pesa kwenye namba uliosomeka: “Utume hiyo hela kwenye namba hii 0747831547 jina litakuja Albert Mlonge laini hii haifungwi.”

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera na Evance Ng’ingo

Post your comments