loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Magufuli atishia kufuta Wakala wa Majengo

RAIS Dk John Magufuli ametaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ubadilike, vinginevyo atakuja kuuvunja na kubaki na vyombo vinavyoweza kujituma katika kufanya kazi.

Aidha, amelinyooshea kidole jeshi la Magereza akilitaka lijirekebishe na kujifunza kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kuwa lina nguvu kazi inayoweza kutumika katika uzalishaji mali na kujenga miundombinu yakiwemo makazi ya maofisa na askari.

Alisema hayo kupitia sherehe za ufunguzi wa majengo 12 yenye makazi ya familia 172 za maofisa na askari wa Magereza katika gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam; ujenzi uliogharimu Sh bilioni 13.

Awali, Rais Magufuli aliagiza Jeshi la Magereza lipewe Sh bilioni 10 lakini baada ya TBA iliyopewa zabuni ya ujenzi kushindwa kumaliza kazi kwa miezi 27 wakiwa wamefikia asilimia 45, aliagiza kazi hiyo ikabidhiwe kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia JKT. Jeshi lilipatiwa Sh bilioni tatu na kufanikiwa kukamilisha ujenzi huo kwa miezi sita.

“TBA siwapongezi kwa sababu hawakumaliza na wabadilike, wasipobadilika, siku zijazo tutaivunja tuwe na jeshi, tuwe na watu ambao wanaweza kujituma kufanya kazi,” alisema Rais Magufuli.

Alifafanua, “TBA walitumia miezi 27 kujenga asilimia 45… Jeshi la Wananchi kupitia JKT wametumia miezi sita kujenga asilimia 55.” alisema.

Majengo hayo yatapunguza tatizo la makazi kwa askari kwa asilimia 18.8. Rais Magufuli alisema ana furaha kubwa kwa sababu Novemba 26, 2016 alipofanya ziara ya kushitukiza katika gereza hilo la Ukonga, alilikuta katika hali mbaya.

Alisema tangu ukoloni nyumba hizo zilikuwa hazijawahi kukarabatiwa.

Akieleza furaha yake zaidi ya kukamilika kwa nyumba hizo, Rais Magufuli alisema serikali ilitoa Sh bilioni 10 kujenga nyumba hizo kupunguza tatizo la makazi kwa magereza.

Fedha hizo zilitolewa Desemba 2016 lakini baada ya miaka miwili alipofanya ziara nyingine hapo kukagua maendeleo ya fedha zilizotolewa, alisikitishwa kukuta zimejengwa kwa asilimia 40 hadi 45 wahusika wakiwa TBA.

“Iliniumiza ilinisikitisha na ndiyo maana nikaamua kwamba kikosi gani kingine ambacho kinaheshimika katika kufanya kazi tofauti na hawa… nilitoa bilioni kumi hawakufanya kitu na ni chombo cha serikali,” alisema.

Aitega Magereza

Katika hotuba yake, Rais Magufuli pia alishangaa jeshi la magereza lenye magereza 129 kushindwa kukarabati makazi ya askari kwa kutumia wafungwa wanaokula na kulala bure badala yake wanajengewa nyumba na JKT yenye kambi 24.

“Sasa wenye kambi 24 wanakwenda kuwajengea wenye kambi 129! Nyumba hizi zimejengwa na JKT ni lazima ndugu zangu, na mimi niseme kwa dhati bila unafiki, tuna wajibu wa kujitathimini watu wa Magereza kwamba kwa nini tuwe na magereza 129 tumeshindwa kujijengea wenyewe nyumba,” alisema.

Alishukuru JKT kwa kujenga nyumba hizo na kusema watakapolala watajifunza kuwa wana wajibu wa kujipanga kuhakikisha makazi ya askari wa magereza yanaboreshwa. Kwa takwimu zilizopo ni kwamba wapo wafungwa na mahabusu wapatao 30,208.

“NI lazima chombo kama magereza tujipange ni namna gani tutaimarisha makazi yetu ya askari. Askari wanateseka. Wanakaa kwenye nyumba zinavuja, wanaweka maplastiki kuzuia mvua. Leo JKT wamevuta maji lakini Magereza hawajayaingiza kwenye nyumba.”

Akiendelea kuhoji utendaji wa Magereza, Rais Magufuli alieleza kusikitishwa na kusuasua kwa ujenzi wa jengo la kiwanda cha kutengeneza viatu cha Gereza Kuu Karanga kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF (ambao ni wabia) ulitoa Sh bilioni tisa tangu Oktoba 2019 lakini hadi sasa Jeshi la Magereza limeshindwa kuharakisha ujenzi huo ambao umefikia asilimia 49 pekee ilhali mitambo inayopaswa kufungwa katika jengo hilo imeshawasili bandari ya Dar es Salaam. Mkataba ulisainiwa Oktoba 18 na ilikuwa yale majengo wamalize ili mashine zinazotoka Italia zije ziwekwe humo.

“Na wametengeneza asilimia 49 ya hilo jengo. Unajiuliza, hizo mashine zitakapokuja zitapelekwa kwenye jengo lipi?,” alihoji Magufuli.

Alimuagiza Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Phaustine Kasike kuhakikisha majengo mapya 12 yaliyojengwa katika Gereza la Ukonga yanatunzwa na kuendeleza utaratibu wa kujenga nyumba za maofisa na askari wake pamoja na kukarabati zilizopo, kwa kuwa haridhishwi na hali duni ya makazi ya maofisa na askari wa magereza nchini.

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments