loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mabosi mashirika, taasisi wajiokoa

MASHIRIKA, taasisi na Kampuni za Serikali 183 kati ya 187 yamepeleka gawio serikalini ya jumla ya Sh trilioni 1.30 hadi jana ambayo ni siku ya mwisho kuwasilisha gawio hilo.

Mashirika yaliyoshindwa kuwalisha gawio lake ni manne ambayo kutokana na hali mbaya iliyo nayo, serikali imeyasamehe hivyo watendaji wake na wenyeviti wa bodi zake hawataondolewa.

Msajili wa Hazina, Athuman Mbuttuka alisema kampuni nne ambazo zimeshindwa kutoa gawio ni Tanzania Pharmaceutical Ltd ambayo haijafanya kazi, Abood Seed Oil Industries Limited ambayo imerudishwa serikalini, Datel Tanzania Limited ambayo haifanyi kazi na Bodi ya Usajili wa Walimu ambayo ni mpya ambayo bodi na menejimenti bado hazijateuliwa.

Alisema mashirika na taasisi 136 kati ya 187 yametoa gawio la chini ya Sh milioni 100 ndani ya siku 60 ambapo yametoa Sh bilioni 25.12.

Kwa ujumla serikali imepokea gawio la Sh trilioni 1.30 kati yake Rais Dk John Magufuli alipokea gawio la Sh trilioni 1.05 na akatoa agizo Novemba 24 mwaka huu na ndani ya siku 60 gawio lililopokelewa ni Sh bilioni 25.12.

Kutokana na taasisi hizo za serikali kuwasilisha gawio, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amepongeza mashirika, taasisi na kampuni hizo kwa kuitikia agizo la Rais John Magufuli la kutoa gawio kwa takribani asilimia 100.

Pia alitoa rai kwamba mwaka 2020 taasisi, kampuni na mashirika hayo yasisubiri rais atoe maelekezo ndipo waanze kulipa gawio na kutoa michango, wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu kwa nafasi zao wanatakiwa kuwajibika ili kuinua utendaji na kulipa gawio na michango kusaidia serikali kutekeleza shughuli za maendeleo.

Waziri Mpango alitoa pongezi kwa taasisi hizo jana wakati akipokea gawio kutoka kwa taasisi sita zilizotoa jijini Dodoma ambapo tangu rais atoe rai hiyo Sh bilioni 25.12 zimekusanywa katika kipindi hicho ambayo itasaidia kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.

Waziri Mpango alisema kati ya kampuni, taasisi na mashirika 187 yametoa gawio na mchango serikalini, isipokuwa taasisi nne ambazo zina sababu maalumu na kuwaadhibu watendaji wake ni sawa na kupiga viboko maiti.

Zilizotoa gawio jana ikiwa ni saa kadhaa kabla ya kufika saa 6:00 muda wa mwisho kutoa gawio ni kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDART) ilitoa gawio la Sh milioni 100, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) Sh milioni 110, Tanzania Development Financial Limited Sh milioni 300, Mwananchi Engineering and Construction Company Limited (Meco) Sh milioni 300, Kiwanda cha Saruji Mbeya na William Diamond Sh milioni 572,173,512.

Alimpongeza Rais Dk John Magufuli kwa kuvunja rekodi maana haijawahi kutokea katika historia ya nchi hii kwa mashirika, taasisi, wakala na kampuni ambazo serikali ina hisa kutoa gawio, michango asilimia 15 na michango ya huduma za jamii.

Dk Mpango alisema taasisi, mashirika na kampuni zote zimeitikia mwito huo isipokuwa nne ambazo Msajili wa Hazina Athuman Mbuttuka amesema zimeshindwa kutoa gawio kutokana na kutokuwa na uzalishaji, upya wa taasisi na kampuni nyingine kurejeshwa serikalini kutokana na mwekezaji kutokidhi vigezo vya mkataba wa ubinafshaji.

“Kazi hii haikuwa rahisi sana, nikifikiria wingi wa taasisi mashirika na kampuni 187 ambazo hazikuchangia, nilijua kabisa lazima damu ya wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu itamwagikia! Lakini naona imekuwa tafauti kabisa… Nawapongeza wenyeviti wa bodi na watendaji husika wangekuwa wameonesha utovu wa nidhamu kwa kukaidi amri ya Rais, hivyo nilikuwa tayari kuwafukuza kazi (leo) na wangeondoka kwa aibu kubwa ya kushindwa mbele ya macho ya Watanzania.”

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments