loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Waliozamia 'Sauzi' kizimbani Dar

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewahukumu Watanzania 30 waliozamia nchini Afrika Kusini na kurudishwa nchini, baada ya kukiri na kutiwa hatiani kwa mashitaka ya kuondoka nchini kinyume cha sheria za uhamiaji.

Washitakiwa hao ambao walifikishwa mahakamani hapo jana, walisomewa mashitaka hayo kwa mahakimu wawili tofauti.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustina Mbando, aliwahukumu wazamiaji 16 kutumikia kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh 300,000 kila mmoja baada ya kukiri mashitaka yao.

Washitakiwa hao ni Omar Kaulu, Dominic Fabric, Sefu Mohammed, Hamad Hashiri, Asbawi Omar, Abdallah Hamad, Razan Ally, Moosa Salimu, Mawki Ally, Daniel Joshua, Amari Abduli, Abdullah Ramadhan, Mohammed Tuwa, Aziz Mohammed, Rajabu Shamanism na Adam Seifu.

Alisema kutokana na makosa hayo kujirudia, kila mshitakiwa atatakiwa kutumikia kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh 300,000.

Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Godfrey Ngwijo, aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa washitakiwa kwa sababu utaratibu wa kutoka nje ya nchi unafahamika.

Washitakiwa hao kwa nyakati tofauti waliomba mahakama iwapunguzie adhabu kwa sababu wamekaa sana gerezani walipokuwa Afrika Kusini na kwamba wameikosea Serikali ya Tanzania pamoja na serikali waliyotoka hivyo wapewe onyo na kupunguziwa adhabu.

Awali, akisoma mashitaka Ngwijo alidai washitakiwa hao walitoka nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume cha kanuni za uhamiaji namba 20 (3) (a) G.N namba 657 ya mwaka 1997 inayosomwa pamoja na kifungu namba 48 (2) ya Sheria ya Uhamiaji namba 54 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016.

Alidai Januari 21, mwaka huu maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), washitakiwa hao wakiwa raia wa Tanzania walikutwa wakiwa wametoka nje ya nchi bila kufuata utaratibu wa kutoka nchini kwenda Afrika Kusini kwa kupitia mipaka inayojulikana.

Washitakiwa wote walikubali mashitaka hayo na upande wa mashitaka uliwasomea maelezo ya awali, ambapo ulidai tarehe zisizofahamika washtakiwa kwa nyakati tofauti walitoka Tanzania na kuingia Afrika Kusini bila kufuata taratibu.

Ngwijo alidai washitakiwa walikamatwa nchini Afrika Kusini na kuletwa Tanzania na kwamba walifikishwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na na kasha kupelekwa Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam na kuchukuliwa maelezo.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salum Ally, aliwahukumu washitakiwa 14 kutumikia kifungo cha miezi 18 jela au kulipa faini ya Sh 50,000 kila mmoja, baada ya kukiri kosa hilo.

Washitakiwa hao ni Adam Luzz, Suleiman Saidi, Kapaya Fredric, Semboko Abubakari, Mambosasa Francis, Juma Mhina, Chale Othoman, Salehe Iddy, Mohammed Kassim, Hassan Ally, Boban Abed, Abdul Kessy, John Joseph na Mawazo Frank.

Baadhi ya washitakiwa wamelipa faini na kuondoka mahakamani hapo pamoja na ndugu zao. Hata hivyo, wakati washitakiwa hao walipofikishwa mahakamani baadhi ya wazazi walidai watoto wao walindoka nchini bila kuwaaga na wengine walilalamika watoto wao kubadili majina.

MGOMBEA ubunge Jimbo la ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi