loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Waziri atoa muda mabaraza wafanyakazi

WAZIRI wa Nchi, Ofi si ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (pichani) ametoa agizo kwa mabaraza ya wafanyakazi yasiyohai 66 kati ya 487 yaliyoundwa kuhakikisa mwishoni mwa Februari yamehuishwa na kufanya vikao kwa mujibu wa sheria.

Akifungua Kikao cha Tatu cha Baraza la Tano la Wafanyakazi la Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) jijini hapa jana, Mhagama amesema mabaraza hayo yanatakiwa kufanya vikao kwa mujibu wa sheria kama agizo namba moja la mwaka 1970 linavyotaka.

“Nachukua nafasi hii kutoa gizo kwa mabaraza ambayo hayapo hai kuwa ifikapo mwishoni Februari yanatakiwa kuwa yamehuishwa na kufanya vikao vyake kwa mujibu wa sheria,”amesema.

Mhagama alisema Ofisi ya Waziri Mkuu iliagiza kwamba taasisi za serikali ziunde na kuhuisha mabaraza ya wafanyakazi katika taasisi na wizara ili mabaraza yawe hai na yatekeleze majukumu yake. Lakini hadi mwishoni mwa mwaka jana, jumla ya taasisi 487 za umma na binafsi zilipaswa kuwa na mabaraza ya wafanyakazi katika maeneo ya kazi.

“Kati yake mabaraza 211 kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ni mabaraza 161 tu yalikuwa hai na yanafanya vikao wakati mabaraza 50 hayako hai,” alisema.

Alisema kati ya mabaraza 276 kutoka Serikali Kuu kwa maana ya wizara na idara zinazojitegemea, wakala wa serikali na mashirika ya umma, mabaraza 260 ndiyo yapo hai na 16 hayapo hai.

Akitoa ufafanuzi wa changamoto za NBS zilizotolewa na Mtakwimu Mkuu wake, Dk Albina Chuwa, Waziri Mhagama alisema kitendo cha wenye viwanda kutoshirikiana na NBS, anatoa agizo kwa watendaji wa ofisi yake wanapofanya ukaguzi lazima mjumbe kutoka NBS awepo katika kundi hilo.

Kuhusu suala la uhaba wa vitendea kazi hasa magari na watumishi, alisema mazungumzo yanaendelea serikalini ili kupata vifaa hivyo muhimu hasa wakati huu kuelekea maandalizi ya sensa na makazi ifikapo 2022.

Awali Mtakwimu Mkuu NBS, Dk Albina Chuwa aliomba ofisi ya takwimu ya taifa kusaidiwa ili wenye viwanda watoe ushirikiano na NBS kwa ajili ya kupata takwimu mbalimbali za viwandani.

Pia aliomba vifaa hasa magari wakati huu ambao NBS ipo kwenye maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi 2022 kwa ajili ya kusafiri maeneo mbalimbali na kupata takwimu zinazotakiwa kwa matumizi ya serikali na wadau wengine.

Pia aliomba kusaidiwa kuongezewa watumishi ambapo sasa inao 188 tu ili kupata takwimu nyingi zaidi za Watanzania milioni 55 lazima kuwa nao wa kutosha hata kama watakwimu wa wilaya sasa wapo chini ya taasisi hizo.

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi