loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wakulima korosho walipwa mil 600/-

ZAIDI ya Sh milioni 600 tayari zimerejeshwa kwa wakulima wa zao la korosho mkoani Mtwara, fedha ambazo wakulima hao walikuwa wakidai katika msimu wa mwaka 2017/2018 na 2018/2019.

Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mtwara, Enock Ngailo ameyasema hayo wakati alipokuwa akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa waandishi wa habari mkoani humo kuanzia Oktoba hadi Desemba 2019.

Zoezi hilo ni endelevu hadi pale wakulima hao watakapopata stahiki zao na kati ya fedha hizo zaidi ya Sh milioni 20 wamelipwa wanachama wote wa Chigugu Amcos wilayani Masasi mkoani humo.

Marejesho hayo yanahusu watu wote ambao wamehusika na ubadhirifu wa fedha za malipo ya korosho kwa wakulima hao kinyume cha sheria ambapo kwa mkoa wa Mtwara fedha wanazodai wakulima kwa ajili ya malipo hayo ni zaidi ya Sh bilioni moja.

“Maagizo aliyoyatoa Rais John Magufuli Oktoba 16, 2019 alipokuwa akisikiliza kero za wananchi Wilayani Masasi kuwa watu wote waliohusika na wizi au ubadhirifu wa fedha za malipo ya korosho kwa wakulima warejeshe fedha zote ili wakulima walipwe fedha zao,”alisema.

Hata hivyo, taasisi hiyo katika kipindi hicho iliendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya kuzuia na kupambana na rushwa kulingana na sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Katika kipindi hicho, jumla ya taarifa 80 za makosa ya rushwa na makosa mengine ya jinai yamepokelewa na taasisi hiyo na uchunguzi wake bado unaendelea katika hatua mbalimbali ambapo taasisi zinazolalamikiwa ikiwemo halmashauri malalamiko 33.

Vyama vya ushirika (23), polisi (4), wanasiasa (4), Tanesco (2), Bodi ya mazao mchanganyiko (2), Bima (1), Cotc 1, Brela (1), Crdb (1), Tanroads (1), NMB(1), Temesa (1) na binafsi (6).

Kuanzia Januari 2020 taasisi hiyo katika kuzuia na rushwa imejiwekea mikakati mbalimbali ikiwemo kuendelea kutoa elimu kwa umma, kwa lengo la kuwafanya wananchi kuweza kuchukua hatua na kushiriki mapambano dhidi ya rushwa.

KAMPUNI ya uchimbaji ...

foto
Mwandishi: Sijawa Omary, Mtwara

Post your comments