loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Shahidi kesi ya Mbowe aeleza alivyopigwa risasi

SHAHIDI wa 12 katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake nane, Aida Ulomi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kusutu jinsi alivyopigwa risasi na Polisi na kisha kuwekwa mahabusu siku 14.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba huku akiongozwa na wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala mahakamani hapo jana Ulomi alidai kuwa siku ya tukio ambayo ilikua ni Februari 16, 2018 alitoka nyumbani kwake Vijibweni wilaya ya Kinondoni majira ya saa 8:00 mchana kuelekea Kinondoni mtaa wa Lunguya kumuona mama yake mdogo ambaye alikuwa akiumwa.

Alidai baada ya kukamilisha dhamira iliyompeleka Kinondoni alianza safari yake kurejea Kigamboni lakini akiwa kituo cha basi Kinondoni Studio ndipo alipokutwa na mkasa huo.

“Baada ya kumuona mama yangu mdogo majira ya saa 11:45 jioni nilianza safari ya kurudi Kigamboni ambapo nilikwenda kupanda daladala katika kituo cha Kinondoni studio ambapo tulikuwa abiria wengi hapo kituoni . Tukiwa hapo yalikuja magari matatu ya Polisi yakitokea upande wa Magomeni na kuanza kupiga risasi juu,”alisema.

Ulomi alidai hali hiyo ilileta taharuki ambapo abiria waliokuwepo kituoni walianza kukimbia huku wakimwambia naye akimbie kwani zile zilikuwa ni risasi za moto, akaungana nao kukimbia kuelekea lango la kuingilia jengo la ofisi za CCM Kinondoni ambako watu wengi walikuwa wakikimbilia kujiokoa.

Aliongeza kuwa kabla hajafika katika geti hilo alihisi kitu kizito kikimpiga mguuni na damu zikaanza kumtoka akashindwa kuendelea kukimbia huku watu wengine wakiendelea kukimbia kuelekea ndani ya Jengo la CCM Kinondoni.

“Nilihisi kitu kizito kimenipiga mguuni na damu zikaanza kutoka nikashindwa kuendelea, wenzangu wakaniambia mama umeshapigwa risasi nikakaa chini.

Baada ya muda mfupi wakaja askari wanne wa kiume wakaniambia nilikuwa kwenye maandamano, nilishangaa na kuwaaambia mimi sielewei ni fujo gani, walinipiga kisha wakawaita askari wa kike na kuwaagiza wanichukue,”alisema na kuongeza:

“Wale askari wa kike waliniburuza mpaka kwenye ukingo wa barabara ambako walikutana na askari mwingine aliyeonekana kuwa mkubwa wao ambaye aliwaamuru waniweke chini na nilimsikia akiwaambia ‘mwekeni huyo mama chini kumeshatokea maafa, okoteni maganda yote ya risasi yaliyopo eneo hili’,” aliongeza.

Aliendelea kueleza kuwa baada ya askari hao kumaliza kuokota maganda walimchukua na kumuingiza kwenye gari la polisi pamoja na watu wengine waliokamatwa na kuelekea katika ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni maeneo ya Magomeni kabla ya kupelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay majira ya saa 1:00 usiku.

MGOMBEA ubunge kwa tiketi ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi