loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dar watumia kondo la mama kuzalisha gesi

MRADI mpya wa kushughulikia taka za afya hospitalini, unaotumia kondo la nyuma la mama baada ya kujifungua kuzalisha gesi, umeonesha mafanikio makubwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala.

Akizungumzia mafanikio ya miaka minne ya hospitali hiyo katika awamu ya tano, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala, Dar es Salaam, Dk Daniel Mkungu alisema mradi huo umeonesha mafanikio makubwa hospitalini hapo na tayari hospitali ya Sinza nao wanaanza kuutekeleza.

“Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, kwa kushirikiana na Shirika na Maendeleo ya UNDP, walibuni mradi huu na sisi tukaupokea na kuutekeleza na ni miaka miwili tangu tuwe nao tumeona mafanikio, alisema Dk Mkungu ambaye pia ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya akinamama.

Akiuzungumzia utekelezaji wa mradi huo, Dk Mkungu alisema baada ya wizara kuuibua hospitali hiyo iliutekeleza ikiwa ni mradi wa majaribio kwa kujengwa mtambo wa kuchakata na kusindika makondo hayo pamoja na mabaki ya vyakula kisha kuzalisha gesi ambayo hutumika kwa matumizi mbalimbali hospitalini hapo.

Dk Mkungu alisema gesi inayozalishwa ni aina ya Methane ambayo huunguzwa na kutumika kuchemshia maji kwenye wodi ya wazazi waliojifungua hospitalini hapo na hivyo kuondoa adha ya awali ya ndugu wa mzazi aliyejifungua kuleta maji ya moto kutoka nyumbani.

“Tumefurahi kwa mtambo huu kujengwa na kuwa na mafanikio chanya, leo hakuna tena harufu mbaya ya taka zinazozalishwa hospitalini hapa kama makondo ya nyuma, na mabaki ya vyakula nao yanaingia kwenye mtambo huo na kuchakatwa kisha kusindikwa na kuzalisha nishati hiyo ya gesi,”alisema Dk Mkungu.

Alisema mtambo huo umezuia harufu mbaya iliyokuwa inatoka hospitalini hapo ya taka na makondo hayo na kwamba hivi sasa kondo la nyuma limegeuka kuwa bidhaa na kwamba kwa siku zijazo watasambaza gesi hiyo kwenye jiko la kanteni hospitalini hapo ili itumike kupikia.

”Hospitali nyingine zinaweza kutumia fursa hii kuzalisha gesi na hivyo kulinda mazingira na kuokoa gharama za nishati kwenye matumizi mbalimbali , kama kupikia na wakati huo huo kulinda mazingira,”alisema Dk Mkungu.

Akizungumzia hali ya mazingira kwa sasa hospitalini hapo, Ofisa afya wa hospitali hiyo, Sifa Mgaya alisema mazingira ni bora na hakuna harufu mbaya tena inayotoka ya taka hospitalini hapo.

“Mtambo huu umekuwa mkombozi kwetu umesaidia kuondoa harufu kwa sababu kondo la nyuma asilimia 80 ni maji kuliteketeza huchukua muda mrefu na hata ukichoma bado kuna moshi unaoenda angani, lakini sasa tumegeuza taka hizi kuwa malighafi,”alisema Mgaya.

Alisema mtambo huo unazalisha gesi kiwango cha kubiki mita 2.5 na kwamba kwa siku huzalisha wanawake kati ya 20 hadi 100 kutofautiana na msimu kwani kuna msimu huzalisha hadi mama 100 kwa siku.

Mgaya alisema teknolojia hiyo ya ujenzi wa mtambo kama huo barani Afrika umeanza kutekelezwa kwenye nchi nne ambazo ni Ghana, Mauritus, Zambia na Tanzania.

Nchini Tanzania mradi huo wa majaribio unatekelezwa kwenye hospitali na vituo vya afya vitano ambavyo ni hospitali hiyo ya Mwanyamala, Sinza, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Hospitali ya Mbagala Rangi tatu na kituo cha afya cha Buguruni cha Anglikani.

Alisema gharama za ujenzi wa mtambo huo ni kati ya shilingi milioni 15 hadi 25 kulingana na mazingira ya eneo.

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi