loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ushindi wampa jeuri kocha Yanga

KOCHA wa Yanga, Luc Eymael amesema wachezaji wa kikosi hicho wameanza kuingia kwenye mfumo ambao utawapa manufaa ya kuendendelea kupata pointi tatu ili kukoleza mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Eymael ametoa kauli hiyo akiwa na furaha baada ya kikosi hicho kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Singida United, mchezo wa ligi hiyo uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Liti, Singida.

Alisema licha ya wachezaji wake kucheza kwa kuelewana hasa sehemu ya kiungo, lakini jambo lililomvutia zaidi ni ushindi huo na namna ambavyo wachezaji wake walivyojitahidi kutengeneza mazingira na kutafuta mabao safi.

“Kwa kiasi fulani wachezaji wangu wameanza kuelewa mfumo ambao natamani watumie na kuona wanacheza na hata wachezaji wapya kama Benard Morrison ameongeza kitu kizuri nafikiri tutakuwa bora zaidi siku zijazo,” alisema.

Eymael alisema wachezaji wake walianza kuonesha kiwango bora hata kwenye mchezo uliopita, ambao walipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC lakini walikuwa wakikosa ubunifu na namba ya kupenya ngome ya wapinzani na kufumania nyavu.

Pamoja na Mbeligiji huyo kufurahishwa na matokeo hayo, alidai ushindi huo sio tu umehamsha ari kwa mashabiki wa timu hiyo, bali pia umeongeza nguvu ya kuendelea kupambana kwenye michezo ijayo kuhakikisha wanazidi kufanya vyema baada ya kutoka kupoteza michezo miwili mfululizo.

Kocha wa Singida United, Ramadhan Nswanzurwimo alisema kilichosababisha wachezaji wake kupoteza mchezo huo ni kubadilisha kikosi kilitoka kushinda mchezo uliopita dhidi ya Ruvu Shooting kwa kuwaingiza wachezaji wengi wageni iliowasajili hivi karibuni katika dirisha dogo.

Alisema wachezaji wake walionekana kutokuwa fiti kwenye utimamu wa mwili na kusababisha makosa kibao yaliyowafanya wapinzani wao kuchukua nafasi hiyo kupata ushindi huo ambao umewafanya kuongeza idadi ya pointi.

“Kiukweli mimi kama kocha nawajibika kwenye makosa ya kubadilisha kikosi kilichotoka kushinda mchezo uliopita, jambo ambalo sikutegemea kwani nilidhani wangekuwa bora zaidi, lakini walinekana kuchoka na kufanya makosa yaliyo wagharimu na kupoteza mchezo nyumbani, “alisema Nswanzurwimo.

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Post your comments