loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kiswahili muhimu uchumi wa viwanda

Kwa kipindi kirefu kumekuwa na mikakati ya kuongeza pato la taifa na kuifanya nchi ya Tanzania kuwa na uchumi imara na madhubuti.

Kasi hiyo imeongezeka zaidi katika kipindi cha utawala wa awamu ya tano ambapo mbali na mambo mengine kuna juhudi za dhati zinazofanyika katika kuifanya nchi ijitegemee katika mambo mbalimbali kwa kutumia mapato ya ndani.

Nikirejelea hotuba ya kwanza katika Bunge la 11 aliyoitoa Rais John Magufuli mwaka 2015 alisema kwamba serikali yake itasimamia sheria ili kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unaongezeka kwa kujenga na kuendeleza viwanda ili kutengeneza ajira.

Kutokana na kauli hiyo, Rais alionesha nia ya dhati ya kukuza uchumi kwa kuendeleza viwanda na kutengeneza ajira. Lugha ya Kiswahili ina fursa nyingi ambazo zinaweza kutumika kusaidia katika kutekeleza malengo ya Rais Magufuli ya kukuza uchumi katika biashara, kilimo, elimu, utamaduni na siasa. Juhudi za Rais katika kukuza uchumi zimekuwa zikienda sambamba na kuimarisha matumizi ya Kiswahili katika nyanja mbalimbali.

Maendeleo ya Tanzania ya uchumi wa viwanda yanahitaji si tu uchumi ulio imara bali pia mbinu na mikakati imara ya kufanikisha lengo hilo.

Lugha ni nyenzo muhimu sana katika kufikia malengo hayo. Nchini Tanzania, lugha ya Kiswahili ni daraja muhimu sana baina ya wananchi na viongozi wao.

Uimarishaji wa lugha ya Kiswahili mbali na mambo mengine utaiwezesha nchi kutekeleza kwa vitendo sera ya maendeleo ya viwanda na kufikia katika uchumi wa kati.

Ili kuwa na uchumi imara ni muhimu kutumia lugha ambayo inaeleweka na inatumiwa na watu wengi jambo linalosaidia katika kurahisisha mawasiliano.

Lugha ya Kiswahili ni bidhaa adimu sana ambayo ikiwekewa mikakati imara ya kuiuza na kuiendeleza inaweza kukuza uchumi kwa kuongeza mapato ya ndani na nje.

Lugha ya Kiswahili ni bidhaa yenye watumiaji takribani milioni 200 duniani na kwa Afrika ni ya pili baada ya lugha ya Kiarabu kwa kuwa na watumiaji wengi. Kwa mantiki hii, Kiswahili ni bidhaa adimu sana ambayo watumiaji takribani milioni miambili wanaitumia na watumiaji wapya wanatarajiwa kuongezeka.

Hivi karibuni limeibuka wimbi la fursa za Kiswahili kwa nchi za Kusini mwa Afrika kama Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia jambo linaloashiria mahitaji na umuhimu wa bidhaa hii adimu. Hii ni fursa muhimu sana kwa nchi ya Tanzania kutumia lugha ya Kiswahili kama bidhaa ambayo itachangia katika maendeleo ya uchumi wa viwanda.

Katika uchumi, lugha ya Kiswahili inaweza kutumika kama chanzo cha mapato hivyo kuwezesha uchumi kukua. Mathalani kunaweza kuwa na miradi ya Kiswahili yenye lengo la kukusanya mapato ya ndani na ya nje.

Makala hii itazifafanua fursa mbili ambazo zinaweza kutumika kukuza uchumi kwa kutumia lugha ya Kiswahili ambazo ni kupitia miradi ya Kiswahili kwa wageni na machapisho.

Kwa mfano, kwa kutumia miradi ya kufundisha wageni, Kiswahili kitaiingizia nchi fedha ambazo zitatumika katika shughuli za maendeleo.

Miradi hii inaweza kuwa ya muda mfupi kwa walelani watalii na wafanyabiashara. Pia, miradi ya kufundisha wageni inaweza kuwa ya muda mrefu na endelevu hasa kwa wale wageni wenye lengo la kuishi Tanzania kwa mfano mabalozi, wanafunzi wa vyuo, wachezaji wa mpira, wafanyakazi katika kampuni za kigeni n.k.

Vilevile, miradi ya kufundisha Kiswahili kwa wageni inaweza kufanyika kwa Watanzania kwenda kufundisha nje ya nchi ambapo mbinu na mikakati imara inatakiwa hasa katika uratibu wa miradi ya namna hii ili kuhakikisha nchi inapata mapato.

Tunaelewa kwamba kuna Watanzania wapo nje ya nchi wanafundisha Kiswahili kwa wageni katika taasisi na vyuo mbalimbali.

Suala la msingi hapa ni kuwa na uratibu mzuri ili nchi ipate mapato kutokana na shughuli kama hizi ambazo bila shaka zingechangia katika pato la taifa.

Jambo la msingi la kuzingatia pia wakati wa kuendesha miradi ya Kiswahili kwa wageni hasa kwa kipindi hiki cha kukua kwa kasi ya teknolojia ya mawasiliano ni kuandaa miradi inayoendana na kasi hiyo.

Hivyo, miradi inaweza kufanywa kwa kutumia njia za mtandao ili kumrahisishiamwanafunzi popote alipo aweze kujifunza lugha ya Kiswahili kwa ufanisi.

Kwa kutumia teknolojia na mbinu bora za ufundishaji kuna uwezekano mkubwa sana wa kupata wanafunzi katika sehemu mbalimbali duniani na hivyo mbali na kukuza lugha na kutoa mafunzo panaweza kuwa na mkakati maalumu wa kukusanya kodi itakayolenga kuongeza mapato ya taifa kwa ujumla.

Kwa upande mwingine, kunaweza kuwa na miradi ya machapisho mbalimbali ya Kiswahili kwa lengo la kuwasaidia wafundishaji na wajifunzaji wa lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania.

Machapisho haya ni pamoja na kamusi na vitabu mabalimbali vya kufundishia na kujifunzia Kiswahili. Kama ilivyopendekezwa hapo juu machapisho nayo yanaweza kuwa kwa njia ya mtandao na njia ya nakala ngumu ili kuendana na kasi ya sayansi na teknolojia.

Kwa ujumla, ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni na uandaaji wa machapisho ya Kiswahili ni vipengele viwili miongoni mwa vingi vinavyoweza kukamilishana na kutumika kama fursa kwa wazungumzaji na wajuzi wa Kiswahili.

Fursa hii inaweza kutumiwa na mtu mmojammoja, vikundi vya watu, asasi za kiserikali na zisizo za serikali. Kwa kufanya hivyo, siyo tu tutakuwa tumeongeza pato la taifa na kukuza lugha ya Kiswahili bali pia itakuwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na tatizo la ajira.

Mwandishi wa makala haya ni Mchunguzi Lugha Mwandamizi, BAKITA. wageni wanaoishi Tanzania matha-

foto
Mwandishi: Fatuma Abdallah

Post your comments