loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mahakama inayotembea Dar yaendesha kesi 50

MAHAKAMA ya Jiji la Dar es Salaam kupitia mahakama inayotembea imeendesha kesi zaidi ya 50 za makosa ya utupaji taka ngumu hovyo.

Mahakama hiyo juzi iliweka kambi siku nzima Uwanja wa Mnazi Mmoja ambapo maofisa wa Manispaa ya Ilala waliwafikisha mahakamani hapo watuhumiwa waliowakamata kwa makosa ya utupaji taka ngumu kuanzia juzi na jana.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Jiji, Hanipha Mwingira alisema waliofikishwa mahakamani hapo ni watuhumiwa waliovunja kanuni za Manispaa ya Ilala inayokataza utupwaji hovyo wa taka ngumu ambapo adhabu ni Sh 100,000.

Amesema asilimia kubwa ya waliofikishwa mahakamani hapo walikiri kutenda kosa na kukumbana na faini huku asilimia kubwa wakitozwa faini kuanzia Sh 20,000 hadi 30,000.

Amesema ametoa faini kulingana na utetezi wa mtuhumiwa ambapo wapo waliokiri makosa ya kutupa ganda la pipi na kuapa kutorudia tena.

Pia amebainisha mahakama hiyo imeshaendesha kesi 28 katika Manispaa ya Kinondoni kesi hizo zinahusiana na utiririshaji hovyo wa maji taka.

Amesema watu 21 kati ya hao 28 walilipa faini isiyozidi Sh 100,000 na kuachiwa huru huku saba wakikanusha kutenda kosa na kupangiwa terehe nyingine ya kusikilizwa kesi zao.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amesema wamedhamiria kukabiliana na uchafuzi wa mazingira ndiyo maana mahakama imeanza na waliokamatwa kwa makosa ya uchafuzi.

Amesema ofisi yake imeanza kuwakamata ombaomba, wazururaji, wanaowasaidia fedha na wadada wanaofanya biashara ya ngono.

Kuhusu ombaomba alisema imetenga eneo Chanika watakaokamatwa wakiombaomba mitaani wapelekwe huko kulima bustani.

Pia aliwataka wenye magari kutowapatia fedha ombaomba barabarani kwa kuwa kwa kufanya hivyo ni kosa na wakikamatwa watashtakiwa.

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments