loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ni kisasi Simba Vs Mwadui leo

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanashuka dimbani leo kuikabili Mwadui katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Azam (FA) hatua ya 32 bora utakaochezwa kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Unaweza kuwa ni mchezo wa kisasi hasa kwa Simba baada ya mapema msimu huu kukutana raundi ya kwanza na wekundu hao kuangukia pua kwa kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa vijana hao wa Shinyanga.

Mchezo huo utaamua mshindi mmoja atakayesonga mbele hatua ya 16 bora kuungana na wengine waliotangulia katika michezo ya juzi na jana.

Wekundu hao wanataka kuweka rekodi ya kushinda na kusonga mbele baada ya kushindwa kung’ara misimu miwili iliyopita katika michuano hiyo kufuatia kutolewa mapema raundi za awali. Ukitizama kiuwezo, Simba ina nafasi ya kushinda kwasababu kwanza haijapoteza mchezo wowote kwenye uwanja wake wa nyumbani msimu huu.

Lakini kingine ina kikosi chenye ubora na kasi kikiongozwa na wachezaji hatari kama Meddie Kagere, John Bocco, Hassan Dilunga, Jonas Mkude na wengine.

Hivi karibuni wametoka kushinda michezo miwili ya Kanda ya Ziwa kwa mabao 2-1 dhidi ya Mbao na 4-1 dhidi ya Alliance.

Ukilinganisha na Mwadui si timu ya kubeza ila imekuwa ikisuasua katika baadhi ya mechi zake zilizopita. Imetoka kupoteza mchezo wa ligi dhidi ya Azam FC kwa bao 1-0.

Katika msimamo wa ligi, Wekundu wa Msimbazi wanaongoza kwa pointi 41 huku Mwadui ikishika nafasi ya 16 kwa pointi 17.

Lakini pamoja na ubora walionao Simba, hawapaswi kuwadharau wapinzani kwani nao pia wanajiandaa wakitambua wanakutana na timu ya aina gani.

Michezo mingine itakayochezwa leo ni Kagera Sugar dhidi ya Might Elephant, Mtibwa Sugar dhidi ya Sahare All Stars, JKT Tanzania dhidi ya Tukuyu Stars, Ndanda dhidi ya Dodoma FC, Gwambina FC dhidi ya Ruvu Shooting, African Sports dhidi ya Alliance na Ihefu dhidi ya Gipco FC.

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments