loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Yanga yaifuata Simba FA

YANGA imeendeleza wimbi la ushindi dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya baad aya kuifunga 2-0 katika mchezo wa Kombe la FA, hatua ya 32 bora katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana.

Hii ni mara ya pili kwa Yanga kuifunga Tanzania Prisons msimu huu, ambapo kwa mara ya kwanza waliifunga 1-0 na kuwa timu ya kwanza kuifunga timu hiyo katika ligi msimu huu.

Kwa ushindi huo, Yanga sasa imetinga hatua ya 16 bora sawa na watani zao Simba, ambao juzi waliifunga Mwadui ya Shinyanga kwa mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja huo wa Uhuru.

Ushindi huo wa Simba ulikuwa ni sawa na kulipa kisasi kwa Mwadui, ambayo hadi sasa ndio timu pekee iliyoifunga Simba katika Ligi Kuu, Tanzania Bara.

Mabao ya Yanga yalifungwa na wachezaji wapya wa timu hiyo, Bernard Morrison na Yikpe Gislain na kuiwezesha Yanga kuibuka na ushindi huo wa mabao 2-0.

Morrison ndiye alikuwa wa kwanza kuifungia Yanga bao pale alipofunga kwa penalti, katika dakika ya 11, baada ya beki wa Tanzania Prison, Michael Ismail kunawa mpira wa krosi katika eneo la hatari, uliopigwa na Juma Abdul. Mpaka mapumziko, Yanga ilikuwa mbele kwa goli 1-0, licha ya wapizani wao kuonesha uimara wa hali ya juu katika muda wote wa mchezo.

Mshambuliaji mwingine mpya, Yikpe alifunga bao katika dakika ya 63 kwa mpira wa kichwa baada ya kutumia vyema pasi ya Haruna Niyonzima, ambaye aling’ara katika mchezo wa jana.

Pamoja na matokeo hayo, kivutio kikubwa katika mchezo huo, alikuwa ni mshambuliaji mpya wa Yanga, Morrison ambaye licha ya kufunga goli, alionesha kiwango cha hali ya juu, huku akiuchezea mpira kwa namna anavyotaka.

Haikua siku nzuri kwa mshambuliaji David Molinga, ambaye aliumia kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na mfungaji wa bao la pili, Yikpe.

Dakika za mwishoni, Deus Kaseke alitoka na nafasi yake kuchuliwa na Patrick Sibomana, wakati Feisal Salum aliingia kuchukua nafasi ya Morrison. Kwa upande wa wapinzani wao, waliongeza nguvu kwa kumtoa Salum Kimenya na kuingia Samson Bangula ambaye hata hivyo hakuleta matokeo chanya kwa timu yake.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments