loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

EAC yajipanga virusi vya corona

NCHI za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimejipanga vilivyo kukabiliana na virusi hatari vya corona ambavyo vinaenea kwa kasi ulimwenguni ili kuhakikisha haviingii katika nchi hizo kutoka nchini China hususan katika mji wa Wuhan.

Wakati Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikiwatoa wasiwasi Watanzania kuhusu virusi hivyo kutokana na muingiliano mkubwa uliopo kati ya wananchi wa Tanzania na China, nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Sudan Kusini zimetoa tahadhari kwa raia wake kuwa waangalifu wanaposafiri kwenda China.

Akizungumza na Habari- LEO Afrika Mashariki juzi kuhusiana na virusi hivyo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustin Ndugulile, aliwatoa hofu Watanzania kwa kuwaambia kuwa serikali imejipanga vilivyo kuhakikisha hakuna mtu mwenye virusi vya corona atakayeingia nchini kupitia njia zote zinazotumiwa na wageni kuingia nchini.

Alisema mpaka sasa hakuna mtu ambaye amegunduliwa kuwa na virusi hivyo nchini au kuwa na dalili za ugonjwa wa corona.

“Mpaka sasa hatuna mgonjwa wa corona nchini, lakini kwa kuwa nchi yetu ina mwingiliano mkubwa wa watu kwenda China na kutoka China kuja kwetu, serikali imeanza kuchukua tahadhari kadhaa, la kwanza tulilofanya ni kutoa tamko kwa umma kwamba kuna ugonjwa unaoendelea huko duniani na watu wachukue tahadhari,” amesema.

Dk Ndugulile alisema hatua nyingine ambazo zimechukuliwa na serikali ni kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji hususan katika viwanja vya ndege ambako watu husafiri kutoka na kwenda China.

Alisema serikali pia imejiandaa kwa vifaa vya kuwapima watu wanaotoka nje ya nchi kwa kutumia kifaa maalumu cha kuangalia joto la mwili ambalo likizidi lile la kawaida ni moja ya dalili za kuwa na virusi vya corona.

“Mashine zetu zikionesha kuwa mtu fulani ana joto la juu lisilo la kawaida hatua ya kwanza ni kumtenga kwa kipindi ambacho tutajiridhisha kuwa ni joto la athari ya virusi hivyo ama laa,” alisema.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo, alisema serikali haitazuia wageni hasa kutoka China au kuzuia safari za ndege kwenda China au kutoka nchini humo kuingia nchini kama njia ya kukabiliana na kuenea kwa virusi hivyo kwa sababu mifumo ya kukabiliana navyo ipo imara kuweza kutambua na kuukabili.

“Wananchi wanaokwenda China wachukue tahadhari wanapoenda huko wajikinge pua na mdomo pamoja na kunawa mikono vizuri na wale wanaokuja nchini tumeweka mifumo na mashine za kuwatambua, ambapo watakaokutwa na virusi yapo maeneo maalum tuliyoyaandaa kwa ajili ya uangalizi maalum,” alisema Dk Ndugulile.

Kenya yajiweka sawa

Serikali ya Kenya nayo imeanza kuchukua tahadhali kuhakikisha virusi vya corona haviingii katika taifa hilo. Taarifa iliyotolewa juzi na Wizara ya Afya nchini humo ilisema umeandaliwa utaratibu maalum wa kuwakagua wasafiri wote wanaoingia nchini humo kutoka China kupitia viwanja vyake vya ndege.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Kitengo cha Afya katika wizara hiyo, Dk Patrick Amoth, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, serikali itaendelea kuchukua tahadhari hadi hapo Shirika la Afya Duniani (WHO) litakapotoa utaratibu mwingine wa kukabiliana na tatizo hilo.

“Tumepeleka tahadhari katika kaunti zetu 47 na tumeimarisha uchunguzi katika kila kituo ambacho kinawezesha wageni kuingia nchini,” alisema Dk Amoth.

Kenya ina safari tatu za ndege kutoka China kwenda Nairobi katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta (JKIA), pamoja na safari mbili zinazofanywa na Shirika la Ndege la Kenya kwenda katika mji wa Guangzhou, China kila siku.

Uganda yajizatiti mipakani

Serikali ya Uganda imeanza kuchukua hatua za tahadhari baada ya virusi vya corona kuenea katika mataifa mengi duniani.

Msemaji wa Wizara ya Afya nchini humo, Emmanuel Ainebyoona, juzi alisema maofisa wa afya waliowekwa mipakani kuchunguza ugonjwa wa ebola, watatumiwa pia kuchunguza homa hiyo itokanayo na virusi vya corona.

Alisema pamoja hatua hizo, serikali inawataka wananchi wote wanaotarajia kusafiri kwenda China au katika mataifa yaliyogundulika kuwa na virusi hivyo kuchukua tahadhari, ikiwamo kuvaa vifaa vya kuzuia mdomo na pua ili kujikinga na virusi hivyo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya, Dk Charles Olaro, alisema serikali imeunda kikosi kazi cha kukabiliana na virusi hivyo, ambapo kwa sasa kinafanya majadiliano kuona njia bora za kuikinga Uganda dhidi ya virusi hivyo.

Uganda ina kiwango kikubwa cha wafanyabiashara wanaosafiri kutoka nchini humo kwenda China na wananchi wa China wanaoingia Uganda kwa shughuli za uwekezaji.

Rwanda yatoa tahadhari Wizara ya Afya ya Rwanda imetoa tahadhari ya usalama kwa raia wake wote wanaosafiri kuelekea China, pamoja na walioko China na wanatarajia kurudi nyumbani kuwa wanapaswa kuchukua tahadhari zote ili wasipate virusi hivyo.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, taasisi na vyombo vya usafiri pia vinatakiwa kuchukua tahadhari ya kuwalinda abiria ili wawe salama muda wote wanapoanza safari hadi wanapofika wanakoenda.

“Tulichokifanya ni kukaa pamoja na wadau wa usafiri wa anga yakiwamo mashirika ya ndege na kuwaagiza kuwafundisha abiria wao njia za kuchukua ili kuwa salama pamoja na kutoa ushauri kuhusu maeneo yasiyofaa kufika,” alisema Waziri wa Afya wa Rwanda, Dk Diane Gashumba. Rwanda ina safari za moja kwa moja kwenda China, pamoja na watalii wengi kutoka China wanaotembelea nchi hiyo.

Sudan Kusini yajipanga Serikali ya Sudan Kusini imepanga kuweka vituo vya uchunguzi hususan katika maeneo yote yanayotumiwa kuingia katika taifa hilo ikiwamo katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Juba.

Wizara ya Afya ya nchi hiyo imewataka wananchi walioko China na wanaotarajia kwenda nchini humo kuchukua tahadhari ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo hatari ambao tayari umeua watu zaidi ya 80 nchini China hadi kufikia juzi.

Dalili za corona Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), dalili za mgonjwa au muathirika wa virusi vya corona ni joto lililozidi la binadamu, kuchoka pamoja na kukohoa mara kwa mara. Ugonjwa huo umeua watu zaidi ya 80 nchini China na wengine zaidi ya 2,700 wameripotiwa kuugua duniani kote hadi kufikia jana.

Baadhi ya mataifa yaliyogundulika kuwa na virusi hivyo ni China, Vietnam, Singapore, Nepal, Canada, Australia, Thailand, Japan, Taiwan, Korea Kusini, Ufaransa na Marekani.

Wakati huo huo, Mwandishi Wetu, Oscar Job anaripoti kuwa safari ya watalii 10,000 wa nchini China waliokuwa wawasili mwezi ujao, imekwama baada ya uamuzi wa aifa hilo kuwazuia raia wake kama watalii kusafiri nje ya hicho hiyo kama njia moja wapo ya kuzuia na kudhibiti kuenea kwa virusi vya ugonjwa wa Corona.

Akitoa taarifa ya kuhusiana na suala hilo jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania Jaji Thomas Mihayo, alisema matarajio watalii hao waliokuwa wawasili nchini kwa Kampuni ya ndege ya ATCL itarejea mara tishio la ugonjwa huo litakapomalizika.

Pia alisema hata tayari Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imeshatoa angalizo kuhusu ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuwaasa wananchi kujihadhari nao.

MGOMBEA ubunge kwa tiketi ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi