loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kikwete amwagia sifa Museveni

RAIS wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete, amemmwagia sifa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kwa jitihada zake za kuijenga Uganda na kuifanya kuwa yenye amani na utulivu huku uchumi wake ukipaa na kwamba ni mshauri na dira kwa viongozi wa nchi nyingine barani Afrika.

Kikwete alimmwagia sifa hizo Rais Museveni juzi, wakati wa kumbukumbu ya miaka 34 ya ushindi wa chama tawala cha nchi hiyo cha National Resistance Movement (NRM), katika Halmashauri ya Manispaa ya Ibanda, nchini Uganda, alipoalikwa kushiriki sherehe hizo.

Kikwete alimwelezea Museveni kama kiongozi wa viongozi wote barani Afrika kutokana na jukumu analolitekeleza la kuwashauri na kuwaelekeza viongozi hao juu ya majukumu yao katika kulitetea bala hilo.

Maadhimisho hayo yaliyoshirikisha wananchi wote wa Uganda yalikuwa na kauli mbiu ya ‘Sherehekea harakati za kizalendo za NRM/NRA zilizoleta umoja wa kitaifa na maendeleo ya kiuchumi.’

Awali kabla ya Uhuru wa Uganda, NRM ilikuwa ikijulikana kwa jina la National Resistance Army (NRA). Katika hotuba yake kwa wananchi wa Uganda, Rais Mstaafu Kikwete alisema harakati za NRM/NRA zilibadili mwelekeo wa Uganda kutoka uliozoeleka wa mambano ya uhuru na kushika mwelekeo tofauti ulioifanya Uganda kuwa nchi tulivu na yenye amani hadi leo.

“NRM/NRA ilileta ushindi kwa Uganda ambao uliifanya nchi ishike mwelekeo tofauti na ule watu waliokuwa wanaujua. Uganda sasa imejiletea amani na utulivu yenyewe, Waganda sasa ni wamoja na wanasonga mbele kimaendeleo,” alisema.

Kikwete ambaye aliiongoza Tanzania kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2015, alisema harakati za Museveni katika kuikomboa Uganda na kuiletea maendeleo endelevu zimemfurahisha na kumfanya kiongozi huyo akubalike miongoni mwa viongozi wa bara la Afrika.

Kikwete aliwafurahisha wananchi na viongozi wa Uganda waliohudhuria sherehe hizo, alipowaeleza kuwa, katika maisha yake alifanikiwa kumfahamu Rais Museveni na harakati zake za ukombozi wa Uganda tangu akiwa anasoma kidato cha sita.

“Nilimfahamu Rais Museveni tangu nikiwa kidato cha sita, alikuwa askari shupavu kweli kweli. Alipokuwa pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliongoza muungano wa wanafunzi wa ukombozi, bado wakati huo nilikuwa kidato cha sita, tulikuwa tukikuangalia kama mfano kwetu.” “Wakati ulipoondoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1971, mwaka uliofuata wa 1972 nilijiunga katika chuo hicho na tulianza kusikiliza stori kuhusu mambo mazuri uliyokuwa ukiyafanya pale,” alisema.

Kikwete alimshukuru Rais Museveni kwa kuwa mfano bora kwake na viongozi wengine barani Afrika na alimuomba asichoke kuwa mshauri wa viongozi wengine hasa wapya barani Afrika.

“Endelea kuwa kiongozi wa mfano kwa vitendo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Barani Afrika na duniani kwa ujumla, hakika mchango wako hautafutika katika historia ya ukombozi katika bara hili,” alisema Kikwete.

Rais Museveni alimshukuru Kikwete kwa mchango wake uliowezesha Jumuiya ya Afrika Mashariki kupiga hatua katika kuyafikia malengo yake.

Aidha, aliwataka viongozi wa Afrika kusisitiza kilimo bora ili kuondoa njaa duniani.

“Kama unafanya kazi kwa ajili ya tumbo tu utapata chakula, lakini tambua kuwa mahitaji yako sio kwa ajili ya tumbo peke yake. Unahitaji pesa kwa ajili ya nguo za familia yako, unahitaji nyumba nzuri, unahitaji usafiri mzuri, unahitaji pesa kwa ajili ya bili za umeme na maji,” alisema Rais Museveni.

Mwaka 1986 chama cha NRM kilishinda vita vya ukombozi dhidi ya majeshi yaliyokuwa yanamtii Dk Milton Obote pamoja na Iddi Amin Dada yaliyokuwa yakipambana na jeshi la ukombozi lililokuwa likiongozwa na Yoweri Museveni.

MGOMBEA ubunge kwa tiketi ...

foto
Mwandishi: IBANDA, Uganda

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi