loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kilimo kipewe msukumo EAC

RIPOTI ya Benki ya Dunia kuhusu Maendeleo ya Kilimo katika mataifa ya Afrika Mashariki, imebainisha kuwa Sekta ya Kilimo katika mataifa hayo imeanza kuwa na mabadiliko chanya.

Taarifa kuhusu ripoti hiyo iliwasilishwa Dar es Salaam hivi karibuni na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kwa Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, Bella Bird.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mabadiliko katika sekta ya kilimo yakitumiwa vyema, yataleta fursa zaidi katika kuongeza ajira, kuondoa umasikini na kuongeza uzalishaji wenye tija kwa nchi za EAC.

Aidha ripoti hiyo iliyofanyiwa utafiti kwa muda wa miaka miwili, pia imeendelea kuitaja Tanzania kuwa ni nchi namba moja kati ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.

Ripoti hiyo imeonesha kuwa kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali ya Tanzania katika kukuza Sekta ya Kilimo, mabadiliko chanya yameanza kuonekana, ikiwemo kuwepo kwa ongezeko la wakulima wa kati, huku wakulima wadogo wanaolima kwa ajili ya chakula tu wakipungua.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mataifa mengine pia ya EAC yameonesha kupata mafanikio makubwa katika kukuza sekta hiyo ya kilimo.

Ni wazi kuwa taarifa hiyo ya Benki ya Dunia juu ya kuimarika kwa sekta ya kilimo katika nchi za EAC imepokewa vizuri na wananchi wa jumuiya hiyo kutokana na ukweli kuwa sekta hiyo ndiyo tegemeo la jamii kubwa ya wananchi wa ukanda huo hususani katika maeneo ya vijijini.

Taarifa kuwa kumekuwa na ongezeko la wakulima wa kada ya kati na kupungua kwa idadi ya wakulima wadogo wanaofanya shughuli za kilimo kwa ajili ya chakula tu, zinatoa picha kuwa sasa wana Afrika Mashariki wengi wameamua kutumia sekta ya kilimo kama njia kuu ya kujikwamua kimaisha.

Kutokana na ukweli huo ni wazi kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo, sekta ya kilimo itakuwa ni mhimili mkuu wa mataifa hayo katika kuzalisha kiwango kikubwa cha ajira na hivyo kutumika kama moja ya suluhisho katika kukabili tatizo la ajira, hususani kwa vijana.

Mbali ya kutoa suluhisho la ajira, lakini pia mabadiliko hayo chanya katika sekta ya kilimo yanatoa ishara ya wazi kabisa kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo, sekta ya kilimo itageuka kuwa tegemeo katika kuchangia ukuaji wa uchumi kwani idadi kubwa ya wakulima watakuwa wamepiga hatua kutoka kilimo cha chini kwenda cha kati na hatimaye kilimo cha juu cha kibiashara.

Wakati tukiyatazamia hayo yaweze kutokea, tunatoa rai kwa serikali na taasisi zinazosimamia sekta ya kilimo ndani ya EAC kuendelea kutilia mkazo programu mbalimbali zilizowekwa na zinazoendelea kuwekwa katika kuboresha sekta ya kilimo ili ziweze kuzaa matunda yaliyokusudiwa.

Ni imani yetu kuwa kama mikakati yote ya kukuza sekta ya kilimo itasimamiwa vema katika utekelezaji wake italeta maana iliyokusudiwa kwani kilimo kitapiga hatua kubwa na kugeuka kuwa tegemeo la mapinduzi ya kiuchumi kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF), Jumanne ya wiki hii lilizindua ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi