loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Jafo ataka kasi ujenzi hospitali Chamwino

SUMA JKT imetakiwa kuhakikisha shughuli za ujenzi wa hospitali ya Uhuru inayojengwa wilayani Chamwino inafanyika usiku na mchana ili kuiwezesha hospitali hiyo kukamilika Mei mwaka huu.

Pia uongozi wa Halmashauri ya Chamwino umetakiwa kufuatilia na kusimamia ujenzi huo kwa karibu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vifaa vya ujenzi vinapatikana kwa wakati.

Maagizo hayo yalitolewa juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Hospitali ya Uhuru inajengwa kwa gharama ya Sh bilioni 3.99 ikiwa ni baada ya Rais John Magufuli kuelekeza kiasi cha fedha zilizokuwa zitumike kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru mwaka 2018 na pia kuelekeza fedha zilizokuwa zimetolewa na kampuni ya Airtel kama gawio kwa serikali.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Jafo alisema ni vyema mkandarasi SUMA JKT kuhakikisha anafanya kazi saa 24 ili kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Uhuru iliyopangwa kukamilika Mei, mwaka huu.

“Lengo la ujenzi wa hospitali hii ni kusaidia kutoa huduma bora za afya na kuwapunguzia wananchi umbali wa kufuata huduma za afya, hivyo ni wajibu wa mkandarasi kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika serikalini.

“Najua mvua ziliwaathiri kidogo, lakini hakikisheni mnafunga taa kubwa hapa site, ili ujenzi ufanyika hadi usiku,” alisema.

Jafo pia aliuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kuhakikisha wanasimamia ujenzi huo kwa weledi, ili gharama zitakazotumika ziendane na thamani ya majengo atakayojengwa.

“Mkuu wa Mkoa (Dk Binilith Mahenge) na viongozi wote wa Halmashauri ya Chamwino hakikisheni kuwa vifaa vinapatikana kwa wakati ili mkandarasi asipate shida na kukwamishwa katika utekelezaji wa kazi yake…”

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Chamwino

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi