loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kobe Bryant, binti yake wafa ajalini

NYOTA wa mpira wa kikapu duniani, Mmarekani Kobe Bryant na binti yake, Gianna, ni miongoni mwa watu tisa waliokufa katika ajali ya helikopta iliyotokea mjini Calabasas, California, Marekani, imeelezwa.

Bryant aliyetamba katika mchezo huo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 41, alikuwa akisafiri na helikopta yake binafsi, ambayo ilianguka na kuwaka moto na kuua watu wote waliokuwa ndani yake.

Mkuu wa polisi wa LA alisema kuwa hakuna mtu aliyenusurika katika ajali hiyo iliyotokea baada ya helikopta hiyo kudaiwa kugonga mlima kutokana na ukungu uliomfanya rubani kushindwa kuona vizuri.

Awali, ilielezwa kuwa helikopta hiyo ilikuwa na watu watano, lakini Polisi imethibitisha kuwa kulikuwa na watu tisa ndani yake na uchunguzi tayari umeanza ili kujua chanzo cha ajali hiyo, ambayo imempoteza gwiji wa mpira wa kikapu duniani.

Bryant, ambaye ni bingwa mara tano wa Michuano ya Mpira wa Kikapu Ligi Kuu ya Marekani (NBA) mara tano alikuwa anatambuliwa duniani katika historia ya kuwa mmoja wa wachezaji bora wa vikapu.

Salamu za rambirambi kutoka kwa watu maarufu na wachezaji wenzake nyota huyo zimekuwa zikimiminika zikionesha mshtuko wa kifo cha nyota huyo wa mpira wa kikapu.

Viwanja vyote vya mpira wa kikapu nchini jana vilitenga muda wa kukaa kimya ili kutoa heshima kwa nyota huyo, ambaye aliichezea Lakers kwa misimu 20. Bryant atakumbukwa katika tuzo za Grammy (Gat the Grammy Awards), ambazo zilikuwa zikitolewa katika Uwanja wa Los Angeles Lakers, eneo ambalo alikuwa akichezea kipindi chote. “Tumechanganyikiwa na tuna uzuni sana kwa sasa,” alisema mtangazaji wa Grammys,

Alicia Keys. “Kwa sababu mapema leo katika mji wa Los Angeles, Marekani na duniani kwa ujumla tumepoteza shujaa wetu mkubwa katika mpira wa kikapu, Kobe Bryant, ndio maana leo tumesimama katika nyumba aliyoijenga.”

NBA katika taarifa yake ilisema kuwa imesikitishwa na ajali iliyosababisha kutoweka kwa uhai wa mchezaji huyo na binti yake, Gianna, mwenye umri wa miaka 13.

“Kwa misimu 20, Kobe alituonesha kile ambacho kinawezekana kwa mtu ambaye ana kipaji na nia ya ushindi,” ilisema taarifa hiyo.

AJALI ILITOKEAJE?

Ofisa wa Polisi, Alex Villanueva alisema kuwa helikopta inaonesha kuwa ilikuwa na watu tisa wakati inaanguka, na kufuta tamko la awali kuwa huenda ilikuwa na watu watano ndani yake.

Katika taarifa iliyotolewa na mji wa Calabasas zilisema kuwa wamepokea taarifa hiyo kwa maskitiko makubwa sana.

“Ndege hiyo ilianguka nje kidogo ya mji wa Las Virgenes asubuhi kwa saa za hapa. Hakuna aliyenusurika katika ajali hiyo,” aliongeza mtoa taarifa huyo.

Gavin Masak, alikuwa anaishi karibu na eneo tukio hilo lilipotokea, alisema kuwa helikopta hiyo ilianguka na kulikuwa na mlio mkubwa na baadae moshi kuonekana katika eneo hilo.

Shuhuda mwingine alisema kuwa alisikia injini ikiwa kama ina shida hata kabla helikopta haijafika chini. Polisi wa LA wameonesha picha za tukio la ajali hiyo zikionesha gari la zima moto na moshi ukifuka kutoka milimani.

Bodi ya Taifa ya Usafiri imeitambua helikopta iliyoanguka kuwa ni Sikorsky S-76B na imesema kuwa itatuma kikosi chake kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.

BRAYANT NI NANI?

Bryant alicheza mpira wa kikapu kwa misimu 20-katika viwanja vya Los Angeles Lakers, pamoja na mafanikio mengine mara 18 alikuwa NBA All Star na anashikilia nafasi ya kwa ufungaji wa pointi nyingi katika kipindi chote.

Alistaafu mwaka 2016. Pia alitwaa tuzo ya mfungaji bora wa NBA pamoja na bingwa mara mbili wa mashindano ya Olympiki. Aliwahi kupata pointi 81 dhidi ya wachezaji wa Toronto Raptors mwaka 2006, katika historia ya michezo ya NBA.

TUZO YA OSCAR

Bryant alishinda tuzo za Oscar kama mchezaji wa filamu fupi mwaka 2018 filamu hilo ilikuwa ‘Dear Basketball’, filamu ya dakika tano iliyoangazia barua moja ya michezo aliyoandika mwaka 2015.

Bryant na mke wake, Vanessa, walijaliwa kupata watoto wanne, ambao mbali na Gianna aliyefariki katika ajali hyo, wengine ni pamoja na Natalia, Bianca na Capri.

Pia washiriki wa tuzo za Oscar mwaka huu walisimama kimya kwa dakika chache katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Lakers kumkumbuka Bryant, ambaye amecheza katika timu hiyo kwa misimu 20.

foto
Mwandishi: NEW YORK, Marekani

Post your comments