loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tehama yawezesha mapinduzi Mahakama Tanzania

MFUMO wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) umetajwa kuleta mapinduzi chanya kwa Mahakama ya Tanzania baada ya kurahisisha masuala mbalimbali ikiwemo uendeshaji wa mashauri, kuhifadhi hukumu na kutambulisha mawakili wa kujitegemea wenye leseni hai.

Pia imeelezwa kuwa mifumo hiyo imeondoa changamoto ya kupotea au kutoonekana kwa majalada ya kesi pamoja na kuokoa gharama za fedha kwa ajili ya majaji kwenda nje ya Dar es Salaam kusikiliza kesi.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka huu jijini Dar es Salaam, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma amesema hadi Desemba 13, 2019 hukumu au maamuzi yaliyoingizwa kwenye mfumo huo kwa Mahakama ya Rufani ni 1523.

Pia alisema katika Masjala Kuu na Kanda za Mahakama Kuu hukumu au maamuzi yaliyoingizwa kwenye mfumo ni 1,297, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi 433, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara 238, Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi 72 na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi 76.

Jaji Profesa Juma alisema mahakama ina vituo sita vyenye huduma za mtandao wa mawasiliano kwa njia ya video (Video Conference) ambavyo ni Mahakama Kuu Dar es Salaam, Mahakama Kuu Mbeya, Mahakama Kuu Bukoba, Kituo cha Mafunzo cha Kisutu, Gereza la Keko na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (Lushoto).

Alisema Oktoba 2019 Mahakama ya Rufani ikiokoa fedha nyingi kwa kuendesha vikao maalum vya mahakama hiyo vilivyofanyika kwa njia ya video conferencing katika vituo vya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya,Tabora, na Bukoba na kwamba kulikuwa na jumla ya maombi 60 ya kusikilizwa ambapo majaji 18 waliyasikiliza.

Alieleza kuwa gharama zilizotakiwa kutumiwa kuendesha mashauri hayo kwa kusafiri nje ya Dar es Salaam ni Sh milioni 100 lakini baada ya kutumia mifumo hiyo ya teknolojia majaji wa Rufani walitumia Sh milioni tano pekee.

‘’Kila Jaji wa Rufani alipangiwa kusikiliza maombi kuanzia mawili hadi sita na kwamba gharama ya kutumia mawasiliano ya moja kwa moja kupitia video ilikuwa Sh milioni tano ambayo ilihusu gharama za mtandao, usafiri wa Naibu Msajili aliyesafiri kwenda Mwanza kuratibu, pia ilijumuisha kuwalipa mawakili wa kujitegemea wanaotakiwa kuwawakilisha wafungwa walio magerezani kwa makosa ya mauaji,’’alifafanua Jaji Mkuu.

Pia alisema Januari 13, mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara ya kwanza, ilitoa dhamana kwa mshitakiwa Abubakar Segui aliyekuwa katika gereza la Keko kwa njia ya mawasiliano ya moja kwa moja kwa njia video na kwamba huo ni mfano wa mwelekeo wa utoaji haki siku zijazo.

‘’Wananchi watakaotembelea mabanda ya mahakama katika Wiki ya Sheria watapata fursa ya kujifunza kwa kiasi gani Mahakama ya Tanzania imejipanga kutoa haki katika karne ya 21 kwa ufanisi kwa matumizi ya Tehama,’’ alisisitiza.

MGOMBEA ubunge kwa tiketi ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi