loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Soko madini mkombozi wachimbaji Ruvuma

WILAYA ya Tunduru iliyopo mkoani Ruvuma imebarikiwa kuwa na utajiri wa madini mbalimbali ya vito vya thamani na dhahabu, na wenyewe wanasema kuna takribani kila aina ya madini isipokuwa tanzanite.

Ukisoma makala haya hadi mwisho utagundua kwamba endapo madini hayo yangesimamiwa ipasavyo tangu yalipoanza kuchimbwa mwaka 1995, wachimbaji wadogo na serikali ingekuwa imeshavuna mapato makubwa kupitia mrabaha na kodi zinazotokana na mauzo ya madini hayo.

Kwamba ni katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja kimeleta manufaa makubwa.Kabla ya ujio wa serikali ya awamu ya tano, sekta ya madini ilishindwa kuwanufaisha Watanzania ipasavyo, shukrani kubwa ziwaendee Watanzania waliomchagua Rais John Magufuli ambaye alipoingia madarakani akafanya mabadiliko muhimu yakiwemo ya sheria katika sekta ya madini yakilenga kuhakikisha rasilimali hizo adhimu zinalinufaisha taifa.

Moja ya vitu ambavyo Rais aliagiza ni kuanzishwa kwa masoko ya wazi ya madini kila mkoa ambapo katika Mkoa wa Ruvuma yameanzishwa masoko mawili ya madini, moja katika wilaya ya Tunduru na soko la mkoa lililopo mjini Songea. Soko la vito na dhahabu la mjini Songea lilifunguliwa Mei 3 mwaka 2019 na soko la Tunduru likafunguliwa Mei 27 mwaka huo huo.

Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma, Jumanne Nkana anasema tangu kufunguliwa kwa masoko hayo hadi kufikia Desemba 31, 2019, jumla ya gramu 206,712 za madini ya vito ziliuzwa sokoni hapo zikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 513.

Anautaja mrabaha uliolipwa kutokana na mauzo hayo kuwa zaidi ya Sh milioni 32 na ada ya ukaguzi iliyolipwa serikalini kuwa Sh milioni 5.4 huku kodi ya huduma kwa halmashauri husika ikiwa ni takribani Sh milioni 1.5.

Nkana anasema dhahabu iliyouzwa katika kipindi hicho ni gramu 24,415.96 zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 2.310 na kuingiza serikalini Sh milioni 138 kama mrabaha na Sh milioni 23 kupitia ada ya ukaguzi.

Kodi ya huduma iliyolipwa kwa Halmashauri husika ni zaidi ya shilingi milioni 6.9, anasema. Anasema katika masoko hayo mawili, jumla ya fedha zilizopatikana ni Sh bilioni 2.824 huku zaidi ya Sh milioni 171 zikilipwa kama mrabaha na ada ya ukaguzi iliyolipwa serikalini ikiwa zaidi ya Sh milioni 28.5.

Jumla ya kodi ya huduma iliyolipwa katika halmashauri husika ni zaidi ya Sh milioni 8.4. Nkana anakiri kuwa kabla ya kuanzishwa kwa masoko hayo kulikuwa hakuna takwimu zozote za mauzo ya madini kwa sababu wafanyabiashara wengi walikuwa hawalipi mrabaha na kodi nyingine zinazotakiwa kulipwa kwa mujibu wa sheria.

“Kwa kweli watu wengi sasa hivi wanafanya biashara ya madini kwa kuzingatia sheria,” anasema. Anafafanua kwamba tangazo la serikali namba 418 la Mei 24,2019, lilianzisha kanuni ambazo zinamtaka mchimbaji yeyote asiyekuwa na leseni au mwenye leseni kuuza madini yake kupitia soko la wazi la madini na siyo kwingineko.

Kwa mujibu wa kanuni, anasema mtu yeyote ambaye atakiuka utaratibu huo anachukuliwa hatua ikiwemo kupokonywa madini na kulipa kodi, ada na tozo zote ambazo alitakiwa kulipa iwapo madini hayo yangeenda kuuzwa soko la wazi la madini. Adhabu nyingine anasema ni kulipa faini mara tatu ya thamani ya madini ambayo amekamatwa nayo sambamba na kupokonywa leseni.

“Kuna watu walijaribu kuipima serikali mnamo Novemba 2019. Hao mabwana walikwenda kufanya biashara ya madini nje ya soko na walipobainika walikamatwa na kupelekwa mahakamani na kupata adhabu zote hizo,’’ anasema Nkana.

Akielezea zaidi tukio hilo, Nkana anasema watu hao walikamatwa mjini Songea wakiwa na jiwe la vito lenye uzito wa gramu 8.6 kutoka Tunduru, likiwa na thamani ya Sh milioni 71.

Anasema watu hao baada ya kutiwa hatiani, walipokonywa madini na kuwa mali ya serikali na kisha kulipishwa faini ya mara tatu ya thamani ya madini ambayo ilikuwa ni zaidi ya Sh milioni 212 na kunyang’anywa leseni ya madini.

“Serikali hivi sasa haitaki mchezo katika masuala ya madini, kila mmoja anatakiwa afanye biashara ya madini kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa,’’ anasisitiza.

Analitaja soko la wazi la madini kuwa lipo kwa ajili ya kila Mtanzania ambapo anayetaka kufanya biashara ya madini na kwamba sheria imeweka wazi kuwa mtu ambaye atauza madini katika soko hatadaiwa kodi ya ongezeko la thamani ambayo ni asilimia 18 ya thamani ya madini, pia atasamehewa kodi ya zuio ambayo ni asilimia tano.

Anasisitiza kuwa kodi nyingine zote zikiwemo mrabaha, ada ya ukaguzi na kodi ya huduma zinatakiwa kulipwa na mnunuzi wa madini husika, hivyo anatoa wito kwa wananchi na wachimbaji wote wakipata madini wapeleke katika masoko ya madini.

Katibu wa chama cha wachimbaji wadogo wa madini wilaya ya Tunduru, Teddy Mataka anasema soko hilo limewakomboa wachimbaji ambao kwa miaka mingi walikuwa wakinyonywa na walanguzi kwa kuwazia madini kwa bei ambayo sio halali.

Anasema tangu kuanzishwa kwa soko hilo wachimbaji wamelifurahia sana kwa sababu sasa wanauza madini yao kwenye soko la uhakika na kwa bei inayolingana na thamani ya madini yanayouzwa.

“Biashara ya madini ya vito ni ya siri kati ya mnunuzi na muuzaji, lakini biashara hii sasa haina siri tena kwa serikali kwa sababu baada ya kuuziana madini wanarudi kwenye ofisi yetu ya soko la madini wakiwa na risiti zao ambazo zinarekodiwa kwa ajili ya serikali kupata mrabaha wake,’’ anasema Mataka.

Anasema hivi sasa wachimbaji wanauza madini bila kero na kwa uhuru zaidi na kwamba hata wanunuzi wa madini wanafarijika na uwepo wa soko hilo kwani limemsaidia kila mnunuzi katika soko kuwa na chumba chake. ‘’Tunampongeza sana Rais John Magufuli kwa kuja na wazo la kila mkoa kuanzisha soko la madini.

Kwa kweli hili soko hivi sasa ni mkombozi wa machimbaji wadogo,’’ anasema.

Anasema soko hili limesaidia wanunuzi wa madini ya vito kuendelea kubaki Tunduru ambako kuna madini mengi ya vito ukilinganisha na mikoa mingine na kwamba kutokuwepo kwa soko kungesababisha wanunuzi kwenda kuweka soko sehemu nyingine hivyo kunafaika wao na madini ya Tunduru.

Mataka anasema tangu mwaka 1996 Tunduru imekuwa hainufaiki na madini kwa sababu katika kipindi hicho aliyekuwa Waziri wa Madini alihamisha wanunuzi wa madini kutoka Tunduru na kwenda Mtwara hali ambayo ilisababisha wananchi wa Mtwara kunufaika na madini ya vito kutoka Tunduru.

Hata hivyo, anataja changamoto kubwa katika soko hilo kuwa ni kutokuwepo kwa vifaa vya kisasa ambavyo vinaweza kutambua thamani halisi ya madini hayo ili kila mmoja kunufaika kwa asilimia 100 kupitia madini ya vito.

Rashidi Juma ni mchimbaji mdogo wa madini katika eneo la Muhuwesi ambaye anasema tangu kuanzishwa kwa soko la madini yeye na wachimbaji wenzake wadogo wanafaidika na uchimbaji na serikali nayo ikifaidika tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma.

Anakiri kwamba kabla ya kuanzishwa kwa soko hilo wachimbaji wadogo walikuwa wananyonywa sana na wanunuzi. [“Mnunuzi alikuwa ananunua madini nyumbani kwake na kwa bei anayopanga mwenyewe bila kujali thamani ya madini ulio nayo. Kila siku walikuwa wanashusha thamani madini kutokana na kukosekana kwa ushindani.

Kuwaweka sehemu moja kwakweli kimeongeza ushindani mkubwa,’’ anasema Rashid.

Mwandishi ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni baruapepe albano. midelo@gmail.com, simu 0784765917

foto
Mwandishi: Albano Midelo

Post your comments