loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bil 5.9/- zaboresha elimu mahitaji maalumu

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano imetumia Sh.bilioni 5.9 kununua na kusambaza vifaa maalum vya kielimu na saidizi katika shule za msingi na sekondari, zinazopokea wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya ya siku 10 Tehama yenye kauli mbiu 'Tehama kwa Walemavu Inawezekana'.

Amesema katika ulimwengu wa teknolojia hakuna atakayeachwa nyuma ndio maana Serikali imeweza kusambaza vifaa saidizi kwa wakufunzi na walimu wenye mahitaji maalumu kwa shule za sekindari na vyuo ili kuwajengea uwezo wa matumizi ya Teknolojia hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akwilapo ametaja vifaa vilivyonunuliwa na kusambazwa kuwa ni shime sikio (Hearing Aids) kwa ajili ya wanafunzi wenye matatizo ya usikivu, mashine za kuandikia maandishi ya breli kwa ajili ya wasioona na vivunge vyenye fimbo nyeupe (Braille kit).

Amesema, katika kipindi cha miaka minne ya Rais John Magufuli, pia Serikali imefanya upanuzi na ukarabati wa Chuo cha Ualimu Patandi ili kuongeza udahili wa walimu kutoka walimu 300 na kufikia walimu 450 kwa mwaka wa masomo 2019/2020.

Pia imejenga shule ya sekondari ya mfano katika chuo hicho yenye uwezo wa kudahili wanafunzi 640 wenye mahitaji maalum.

Aidha, shule hiyo itasaidia wanachuo kufanya mazoezi ya kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa vitendo na kuwa mahiri katika fani wanazosomea.

“Mnaweza kuona jitihada ambazo serikali imekuwa ikizifanya nitoe wito kwa familia, na wadau wa maendeleo kuendelea kuona umuhimu wa kuchangia juhudi za serikali katika kuwapatia huduma stahihiki wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika ujifunzaji, " alisema.

Amesema ushiriki wa jamii ni muhimu kwani masuala ya watu wenye ulemavu ni mtambuka hivyo jitihada za pamoja zinahitajika ili kufikia malengo yaliyoanishwa katika miongozo ya kitaifa na kimataifa.

Aidha akizungumzia mafunzo ya TEHAMA na teknolojia saidizi yanayotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Katibu amesema yanalenga kuwajengea uwezo wakufunzi na walimu wa sekondari wasioona, viziwi na wenye ualbino katika matumizi ya TEHAMA na teknolojia saidizi ili kuboresha ufundishaji katika vyuo vya ualimu na shule za sekondari nchini.

Amesema, mafunzo hayo yatawapatia maarifa na stadi kuhusu mfumo, vipengele na utendaji kazi wa kompyuta, utumiaji wa programu saidizi za sauti na kukuza maandishi katika kompyuta, kupata stadi za matumizi ya mitandao katika kutafuta na kutuma taarifa katika tovuti na barua pepe na kutumia kikamilifu maudhui ya kielektroniki katika ufundishaji na ujifunzaji.

Kaimu Kamishna wa Elimu Paulina Mkonongo amesema, kufanyika kwa mafunzo hayo ni mkakati wa Serikali kuhakikisha elimu inaboreshwa katika makundi yote.

Awali Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu Maalum Greyson Mlanga alimweleza Katibu Mkuu kuwa mafunzo hayo kuwa yanashirikisha wakufunzi 140 wenye mahitaji maalumu, wakiwemo viziwi 37, wasioona na wenye uoni hafifu 103 kutoka vyuo vya ualimu vya serikali na walimu wa shule za sekondari nchini.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo, Mkufunzi kutoka Chuo cha Ualimu Morogoro Godfrey Omary ameishukuru Serikali kwa kutoa mafunzo hayo kwa kuwa yanakwenda kuondoa ulemavu katika maeneo yao ya kazi kiutendaji lakini pia itapunguza utegemezi na kufanya kazi kwa ufanisi.

Mafunzo kuhusu matumizi ya TEHAMA na Teknolojia saidizi kwa walimu na wakufunzi na wenye mahitaji maalumu yanatarajiwa kuhitimishwa Februari 05, 2020.

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments