loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Waziri atoa siku 7 'mchwa' wakamatwe

WAZIRI  wa Madini Dotto Biteko ametoa wiki moja kwa   Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuwachukulia hatua kali wafanyakazi wabadhilifu wa mradi wa kuchoronga  miamba katika sekta ya mafuta na gesi.

Biteko aliyasema hayo leo, Jumanne katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi (Tamico), ambapo alimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo la Stamico, Venance Mwase kuwachukulia hatua wafanyakazi hao wabadhilifu kwa kile alichodai kuwa wamekua wakighushi risiti na ankara za malipo.

“Kuna ubadhilifu unafanyika hapa, kuna wafanyakazi mikono  yao sio misafi, nafahamu Mkurugenzi unalijua hili vizuri na wahusika unawafahamu, sasa nakuagiza uwachukulie hatua haraka sana kabla mimi sijachukua hatua,” alisema Biteko na kuongeza:

“Tena nataka hatua hii ichukuliwe isizidi wiki moja na nipate taarifa, wale wote ambao wamehusika wajiandae, serikali imekuwa ikipoteza mapato ambayo yanaishia kwenye mikono isiyo misafi, wapo Watanzania wengi ambao wanaweza kuusimamia na serikali ikapata faida,” alisisitiza.

Shirika hilo la Stamico limekua likitoa  huduma za kibiashara za uchorongaji miamba wa biashara katika sekta ya mafuta na gesi ambapo katika Mwaka wa Fedha 2019/20  limefanikiwa kupata kandarasi nne  za uchorongaji kupitia zabuni mbalimbali zenye thamani ya shilingi bilioni 2.2.

 

Hata hivyo Biteko alionyesha kusikitishwa na ubadhilifu unaofanywa na baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu na kusema kuwa mtambo huo wa uchorongaji ulinunuliwa na serikali kwa fedha nyingi ambazo ni dola milioni 100 ambazo zingeweza kupelekwa katika sekta ya afya na kununua madawa na huduma nyingine za afya.

Licha ya changamoto hizo za ubadhilifu Biteko alipongeza Shirika hilo ambalo kupitia mtambo huo limeweza kufanya kazi na kuingiza shilingi bilioni nne na kupata faida ya Sh milioni 600.

Awali akimkaribisha Waziri Biteko, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Simon Msanjila alipongeza Stamico kwa mafanikio waliyofikia kutoka shirika lililokuwa linazalisha hasara mpaka kutoa gawio serikalini.

“Stamico mwaka jana mmeweza kupeleka gawio la Sh. Bilioni moja serikalini tofauti na siku za nyuma ambapo shirika hilo lilikuwa likizalisha hasara na madeni yalifikia Sh. bilioni 63,” alisema.

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Na Vicky Kimaro

Post your comments