loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mkanganyiko ratiba unavyochafua Bodi ya Ligi

BODI ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TLBP) juzi imeingia kwenye mgogoro mkubwa na Klabu ya Yanga baada ya kusahau kuipangia ratiba ya kucheza mchezo wa ligi hiyo ndani ya wiki nzima, huku ikifahamika wazi ndio timu pekee iliyocheza michezo michache ikilinganishwa na nyingine.

Ligi hiyo inayojumuisha timu 20 hadi sasa mechi za mzunguko wa kwanza zinaelekea mwishoni, Yanga wamecheza michezo 15 ikiwa ni nyuma kwa tofauti ya michezo mitatu na timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo, ambazo zimeshuka uwanjani mara 17.

Matatizo ya ratiba na kusababisha baadhi ya timu kuwa na viporo vingi yamekuwa sugu, kwani misimu mingi malalamiko hayo kwa timu za Simba na Yanga yamekuwa yakijitokeza na imefikia hatua mamlaka husika zimeshindwa kutafuta mbinu itakayosaidia kumaliza suala hilo. Kwa msimu uliopita, Simba walionekana kuwa na viporo vingi ikilinganishwa na vikosi vingine na hiyo ilitokana na Bodi ya Ligi kushindwa `kubalance’ mechi za Simba, ambayo ilikuwa ikishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Juzi uongozi wa Yanga kupitia Ofisa habari wake, Hassan Bumbuli alizungumza na vyombo vya habari kutoa malalamiko yao kuhusu suala la ratiba kwa kushindwa kuwapangia mchezo ndani ya wiki nzima wakati wanajua ndio timu pekee iliyocheza michezo michache kwenye ligi hiyo.

Bumbuli alidai kwa hali inayoendelea wao wanajua ni moja ya mikakati ya kuihujumu timu yao kuwatengenezea mazingira bingwa mtetezi wa ligi hiyo Simba ambao wanaongoza ligi hiyo kwa sasa. Hata hivyo kupitia malalamiko hayo, Bodi ya Ligi haikuwa nyuma kwani kupitia Mwenyekiti wake, Steven Mguto ilikiri kufanya kosa hilo kwa madai kwamba vijana wake wakati wanafanya majukumu ya kupanga waliisahau timu ya Yanga kuipangia mchezo.

Aidha, alieleza hata Yanga nao walipaswa kuwakumbusha viongozi wa ligi hiyo kama waliona hawakupangiwa ratiba ya mechi, na kuwaomba radhi wanajangwani hao huku wakidai suala hilo watalishughulikia ndani ya wakati.

Changamoto inayoonekana hapa bodi ya ligi haitimizi majukumu yake na kwamba wanaendesha ligi hiyo kubwa nchini bila kuwa na ratiba maalumu.

Tatizo la ratiba ya michezo ya ligi limekuwa likileta misukomisuko kwa timu kubwa za Simba na Yanga kila msimu na kwa hili linaloendelea wahusika kwa maana ya Bodi ya ligi wanapaswa kuzungumza na viongozi wa Yanga na kuja na mfumo wa ratiba isiyo kuwa na upendeleo kumaliza suala hilo ambalo linaonekana kuleta shida.

Pili, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia bodi hiyo wanapaswa kuleta wataalamu kutoka nchi za nje watakaokuja kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake ili kupanga ratiba itakayotenda haki bila kuangalia hizi timu kubwa.

Tatu, TFF wanapaswa kuzingatia matukio muhimu kabla ya kuanza kupanga ratiba ya mechi hiyo itasaidia kuheshimu ligi na kuipandisha thamani kuwavutia wawekezaji kuingiza fedha zitakazokuwa zinasaidia klabu husika kujijenga kiuchumi.

MAJANGA ya asili yako mengi ni pamoja na radi, matetemeko ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi