loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM: Mishahara kwa watumishi haitoshi, hata wangu hautoshi

RAIS John Magufuli amekiri kuwa mshahara wake na watumishi kutoka sekta zote nchini hautoshi kwa sababu serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa sasa.

Mkuu huyo wa nchi ameyasema hayo leo, Alhamisi, katika maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika kitaifa katika ukumbi mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaa leo.

“Kuna changamoto ya uhaba wa rasilimali fedha, sio tu kwa mhimili wa mahakama, lakini pia kwa sekta nyingine, mshahara wa watumishi wa sekta zote nchini hautoshi, hata mimi wa kwangu hautoshi,” ameeleza.

Hata hivyo Rais Magufuli amesema serikali itajitahidi kukabiliana na changamoto hiyo ili kuweka mazingira bora ya kazi kwa watumishi wake. Rais Magufuli pia ameupongeza mhimili wa Mahakama kwa kazi nzuri ambayo imeifanya katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.

Ameeleza kuwa Mahakama imeweza kushughulikia changamoto kama zile za mlundikano wa kesi mahakamani na mahabusu, kesi kuchukua muda mrefu kusikilizwa, vitendo vya rushwa na malalamiko ya watu kubambikiwa kesi.

“Mafanikio yaliyofikiwa yamechangiwa na kuongezeka kwa idadi ya majaji na mahakimu, matumizi ya TEHAMA kwenye usikilizwaji wa kesi pamoja na matumizi ya Mahakama zinazotembea ambazo zimepunguza mlundikano wa kesi na kesi kusikilizwa kwa kipindi kirefu,”ameongeza.

Wakati huohuo, Rais Magufuli ameahidi kumpatia Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma kiasi cha Shilingi bil. 10 ili kuuwezesha mhimili huo kujenga makao makuu ya mahakama jijini Dodoma.

foto
Mwandishi: Janeth Mesomapya

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi