loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mbinu za kutafsiri makala zenye dhana za kitamaduni

UTAMADUNI ni mkusanyiko wa mila na desturi zote za jamii inayotumia lugha moja mahsusi kama njia yake ya mawasiliano. Hivyo, lugha ni sehemu ya utamaduni na inaelezea utamaduni wa jamii husika.

Lugha zote zina uwezo wa kumsaidia binadamu kuelewa mambo mbalimbali yanayotokea duniani na yanayomzunguka. Lakini kila lugha inaweza kufanikisha hilo kwa namna inayotofautiana.

Kila lugha inatumia maneno tofauti na pia huyapanga maneno hayo katika mfumo tofauti unaokubalika kwa watumiaji wa lugha hiyo. Makala haya yataangalia kwa ufupi matatizo wanayokabiliana nayo wafasiri wa matini zenye dhana za kitamaduni na mbinu mbalimbali za kukabiliana nayo. Makala yatajikita zaidi katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili.

Katika kutafsiri kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili, mfasiri atatakiwa kupata visawe vya kitamaduni vinavyoendana katika lugha chanzi na lugha lengwa. Visawe hivyo vinapokosekana, hapo ndipo mfasiri anapokumbana na matatizo.

Wataalamu mbalimbali wa tafsiri wameeleza kwamba tofauti katika tamaduni zinasababisha matatizo makubwa kwa mfasiri kuliko ilivyo katika tofauti ya kisarufi. Ni kwa msingi huo ndiyo maana inasemwa kwamba tafsiri si mchakato wa kisintaksia tu, bali pia inahusisha utamaduni.

Katika kufanya tafsiri, maneno ambayo ni ya kawaida katika lugha kama vile chakula, nyota, kuogelea, jua, mwezi n.k hayaleti matatizo katika tafsiri kwa kuwa yanapatikana karibu katika lugha zote. Lakini maneno ya kitamaduni katika Kiingereza mfano monsoon, autumn yanaleta matatizo katika tafsiri kwa kuwa hayako katika utamaduni wa Kiswahili.

Kuna umuhimu mkubwa kwa mtu anayetafsiri kufahamu utamaduni wa watumiaji wa lugha chanzi ili kuzingatia tofauti hizo wakati wa kutafsiri. Kwa mfano tunapozungumzia uhusiano katika familia, lugha ya Kiswahili na Kiingereza zina namna tofauti ya kuelezea uhusiano katika familia, kwa mfano; Kiswahili Kiingereza Shangazi Aunt Mama mdogo Aunt Mjomba Uncle Baba Mdogo Uncle Katika mfano huo hapo juu, mfasiri anapotafsiri kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili inabidi atoe maelezo kuhusu uhusiano huo, kwamba “uncle” anayezungumziwa ni baba mdogo au ni mjomba na “aunt” ni shangazi au mama mdogo ili msomaji katika Kiswahili aelewe kwamba “uncle” au “aunt” katika Kiingereza sio lazima awe mjomba au shangazi tu.

Pia kuna majina ya vyakula mbalimbali kulingana na utamaduni wa lugha fulani kwa mfano, katika Kiswahili kuna mpunga, mchele, wali, pilau ambapo katika Kiingereza ni “rice” tu kwa vyote. Kwa hiyo, unapotaka kutafsiri kutoka Kiswahili kwenda katika lugha ya Kiingereza itakuwa vigumu kupata visawe vinavyofanana na majina ya vyakula hivyo kwa sababu ni vyakula ambavyo katika utamaduni wa lugha hiyo havipo.

Baada ya kuona mifano michache hapo juu, sasa tuangalie pale ambapo hakuna kabisa kisawe kinacholingana, nini kifanyike? Zipo mbinu ambazo zinatumika ili kuweza kutoa maana inayokaribiana na ile ya lugha chanzi. Mbinu ya kwanza ni utohoaji ambapo neno linalohusiana na utamaduni katika lugha chanzi linahamishwa kwenda katika lugha lengwa kwa kutumia matamshi ya lugha lengwa.

Kwa mfano majina ya wanyama ambao hawapatikani katika mazingira yetu kama “kangaroo” na “seal” yanatoholewa na kutamkwa kufuatana na fonetiki ya Kiswahili na kuwa kangaruu na sili. Mbinu nyingine ni kutafsiri kwa kutumia kifungu cha maneno ambacho kinafafanua shughuli au namna kitu kinavyoonekana. Mbinu hii mara nyingi hutumika kama hakuna kisawe kinachofanana na lugha chanzi.

Kwa mfano, maneno ya Kiingereza yanayohusiana na vyakula kama toast, egg chop, sandwich n.k katika Kiswahili itabidi yatolewe maelezo ya mwonekano wake au jinsi vinavyopikwa yaani “mkate unaokaushwa kwenye moto” na “yai la kuchemsha lililozungushiwa nyama ya kusaga” na “vipande vya mkate vyenye nyama”.

Mbinu nyingine ni kuliondoa neno ambalo halina kisawe kinachofanana katika lugha lengwa. Katika mbinu hii maneno yaliyokosa visawe katika lugha chanzi huachwa na yanatafsiriwa yale tu yenye maana katika lugha lengwa. Lakini mbinu hii haifai kwa sababu kuliondoa neno kunaweza kusababisha kupoteza maana, isipokuwa kama neno linaloondolewa halina umuhimu kulingana na ujumbe unaotolewa.

Mwisho, wafasiri wanapofanya tafsiri wanao wajibu mkubwa wa kuzingatia utamaduni wa lugha chanzi na zaidi utamaduni wa lugha lengwa ili kufanikisha tafsiri. Kuzingatia utamaduni wa lugha wakati wa kutafsiri kunafanya tafsiri ieleweke, ikubalike na itimize malengo yaliyokusudiwa. Pale ambapo hakuna kisawe, basi mbinu mbalimbali zilizoelezwa hapo juu zinapaswa kutumika ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa walengwa.

Mwandishi wa makala haya anatoka Idara ya Tafsiri na Ukalimani, BAKITA.

HUDUMA bora za afya ya msingi zinapunguza uhitaji, gharama na ...

foto
Mwandishi: Vidah Mutasa

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi