loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wahadzabe wanavyozidi kutoka ‘porini’

AMAYEGAAMO na Mdana Amayegama Ama ni salamu inayotumiwa na watu wa jamii ya Wahadzabe au Wahadza kama salamu ya jumla. Sehemu kubwa ya jamii hiyo bado inaishi katika maisha mithili ya ujima kwa maana ya kuokota na kuwinda, chakula chao kikuu kikiwa nyama, mizizi, matunda na asali.

Ingawa kuna mabadiliko ya taratibu, lakini bado jamii hiyo inaendelea kuishi kwenye viota katikati ya mapori. Serikali ya Mkoa wa Singida imekuwa ikiendelea kufanya juhudi katika kusaidia jamii hiyo.

Wahadzabe ni miongoni mwa makabila madogo zaidi sana linalopatikana kaskazini mwa Tanzania kando ya ziwa Eyasi kwenye bonde la ufa na kupakana na uwanda wa Serengeti.

Halikadhalika wamekuwa wakipatikana katika wilaya ya Mkalama mkoani Singida. Ingawa wamekuwa hawashiriki sana kwenye sensa ya watu na mkazi, kabila hilo dogo linakisiwa kuwa na watu wasiovuka 2,000.

Kwa asili kabila hili halina uhusiano sana na watu wa makabila mengine ya Tanzania. Ni kabila ambalo linahusishwa na lugha za Kikhoisa za Afrika Kusini na hivyo kwa Tanzania linakuwa kabila linaloonekana kuwa la peke yake.

Lugha ya Kihadzabe bado ni ya mdomo zaidi kuliko kuandikika. Hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni, wengi wa Hadza wamejifunza Kiswahili kama lugha ya pili. Jamii hiyo inatajwa kuwa ni ya mwisho kabisa barani Afrika inayotegemea uwindaji na ukusanyaji matunda kwa ajili ya kuishi.

Hata hivyo, Wahadzabe wapo katika hatari ya kupoteza asili yao kwa kuwa maeneo waliyokuwa wakiishi tangu enzi za mababu yamevamiwa na wakulima na wafugaji na kwa msingi huo, jamii hiyo imekuwa ikishauriwa kubadilika pia kwa maana ya kuanza shughuli za uzalishaji badala ya kutegemea asili.

Wakati fulani, aliyewahi kuwa mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone, aliwahi aliwapelekea majembe 70 ili wayatumie kulima lakini aliporudi huko kufuatilia matokeo ya zana hizo za kilimo akakuta wametumia mipini ya majembe hayo kwa kutengeneza visu na mikuki kwa ajili ya kuwindia.

Awamu ya pili akapeleka majembe 150 na hali haikuwa tofauti sana na hiyo. Hata walipopatiwa shamba la kulima lenye ukubwa wa ekari 10 baada ya kupanda hawakurudi tena kuangalia vimeota ama la na ulipofika msimu wa mavuno waliambulia gunia moja tu la mahindi. Wakati wa sensa ya watu na makazi nchini mwaka 2012 hawakujitokeza ili wahesabiwe hivyo ikabidi kutafutwa kwa mbinu mbadala kufanikisha jambo hilo muhimu kwa taifa.

Mbinu hiyo ilikuwa ni kuchinjwa kwa swala, nyama ikachomwa, wakaenda kwa wingi kutoka mafichoni walipokuwa. Hata hivyo, jamii hiyo imekuwa ikibadilika taratibu na watoto wao kupelekwa katika shule ya bweni ya Munguli.

Watoto hao wameanza kuleta pia mabadiliko kwenye jamii hiyo. Serikali iliamua kujenga shule hiyo ya bweni maalumu kwa ajili ya watoto wa kabila hilo katika juhudi za kuwaendelea Wahadzabe.

Uchunguzi kijiji cha Munguli katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama unaonesha kwamba kuna mabadiliko kwa jamii hiyo kwa sababu wameanza kuishi maisha ya kawaida na wengi wao wamehama maporini na kuishi kijijini na familia zao huku wakiruhusu watoto wao waende shule.

HUDUMA bora za afya ya msingi zinapunguza uhitaji, gharama na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi