loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Utoaji mahari katika mila za Wahaya

IJUMAA iliyopita, niliandika makala yenye kichwa cha habari: Mbwembwe Zinazotawala Mchakato wa Uchumba kwa Kabila la Wahaya. Leo, nitajikita katika mambo yanayojiri katika utoaji mahari kwa mujibu wa mila za Wahaya ambao ni wenyeji wa Mkoa wa Kagera.

Katika zama hizi za utandawazi, desturi za mila za kumtafutia kijana mke hazifuatwi sana. Vijana wanaweza kufahamiana katika maeneo ya mbali na familia zao, kama vile vyuoni, kazini na penginepo, wakaweka nia ya kuchumbiana na kuwa mke na mume.

Pamoja na uhuru huo, jukumu la kuweka uchumba na kutoa mahari, linabaki kuchukuliwa na wazazi na kutoa ushauri pale unapohitajika. Hivyo vijana hao huleta taarifa ya nia yao kwa wazazi, ambao husimamia jambo hilo kwa kufuata mila na desturi. Hata kama baba wa kijana husaidiwa na kijana kutokana na kipato alicho nacho, jamii humtambua baba kuwa ndiye anayemtolea mwanawe mahari.

Mahari ni jambo muhimu na la msingi ili kuruhusu ndoa katika jamii ya Wahaya. Kwa kawaida, hutolewa kwa awamu kulingana na uwezo wa wazazi. Baada ya mshenga kukamilisha hatua ya kushika uchumba kwa kuleta ‘simbula emihunda’, ambayo ndiyo kishika uchumba, hutakiwa kurudi siku iliyopangwa ili kuelezwa mahari atakayotoa. Mahari halisi ya Wahaya huitwa ng’ombe, hata kama kilicholetwa ni mbadala wa mnyama hai ambacho aghalabu ni pesa.

Pombe - lubisi, ambacho ndicho kinywaji cha jadi, huletwa kila mshenga anapokuja kwa wakwe kukamilisha hatua fulani. Huko pia huandaliwa lubisi kwa ajili ya waalikwa na wageni. Mahari hiyo hutolewa sambamba na vitu kadhaa ambavyo ni kama zawadi kwa watu maalumu wakiwa ni pamoja na mama mzazi, bibi na babu.

Awali ya yote, huletwa beberu yaani mbuzi dume hai majira ya jioni, pamoja na kisu na chumvi, kwa ajili ya babu wa binti. “Mbuzi huyo,” anasema Mzee Nestori Ishengoma: “Huchinjwa kesho yake na kuwakirimia marafiki, na jamaa wa ukweni.”

Anaongeza: “Ni namna ya kuwashirikisha ndugu wote katika kumtoa binti, wakiamini kuwa mtoto ni wa jamii nzima. Akisha kamilisha hilo, mshenga hupewa orodha ya mahari atakayotoa.”

Kimsingi, siku ya kuleta mahari huwa ni siku ya sherehe kubwa. Shughuli hii huanza alasiri, na kuendelea hadi usiku wa mapema, lakini wageni hawalali huko, sharti warudi na kutoa taarifa kwa baba ambaye hubaki nyumbani. Mama wa kijana huambatana nao. Wazee huvaa kanzu nyeupe, koti na kofia pana kichwani, mikononi, hushika kibuyu kidogo chenye shingo ndefu cha kunywea pombe.

Wanawake ‘huvaa’ mashuka meupe. Mama wa kijana huvaa shada la eshisha kichwani kama kitambulisho cha heshima yake. Nao pia hubeba kakibuyu kadogo kenye shingo fupi, ila hawakaoneshi hadharani. Kwa mujibu wa wazee mbalimbali wa Kihaya, vijana wa kiume na kike ndio hubeba pombe, mikungu ya ndizi, ntukuru zilizonakshiwa kwa ustadi mkubwa, na ndani yake huwekwa zawadi nyinginezo ikiwa ni pamoja na kitoweo (nyama), viungo mbalimbali na vitu vingine.

Vibuyu vya pombe na mikungu ya ndizi navyo hunakshiwa vizuri kwa majani ya migomba na eshisha. Mzee mmoja anayekataa kutajwa jina mwenye umri wa takriban miaka 70 anasema: “Huyo ng’ombe huswagwa pamoja na msafara huo wa watu.

Sasa, wafikapo kule ukweni, wanasimama; lazima wasimame mbali kidogo na nyumbani wanakokwenda kutoa mahari…” Anaongeza: “Ndipo sasa yule mshenga hujongea ndani na kutoa taarifa kuwa wameshawasili, na kurudi kwa wenzake akisubiri kutumiwa mjumbe kuwaruhusu waingie.’

Vyanzo mbalimbali vya kuaminika vinasema, baada ya kutumiwa mjumbe kuwakaribisha, mshenga huwaongoza kuingia ndani; huwasalimia wakwe kwa heshima kubwa, wakianzia ukumbi wa wazee – barazani/sebuleni na kuendelea ukumbi wa ndani kwa akina mama.

Hata hivyo, hawaingii na mahari (vitu) walivyoleta, vijana hubaki navyo nje. Baada ya kukaa kidogo, mshenga huinuka na kukalia mkeka akiomba kuleta alivyokuja navyo. Huruhusiwa na kutoka nje kuingia na vijana waliobeba mahari na kuwasilisha walivyobeba mbele ya umati uliokusanyika, akitoa maelezo ya kila kimoja kadiri ilivyoorodheshwa na kuviweka kwenye shuka maalumu lililotandazwa chini. Iwapo mahari halisi ni pesa, huwa imefungashwa kwa nakshi ndani ya mojawapo ya ntukuru na huingiza mkono ndani na kuitoa; bila kufungua.

Kawaida huulizwa kama ‘imetimia’ naye hutamka kuwa imetimia, na kuirudisha ndani. Ni ishara ya kuaminiana. Kwa mujibu wa uzoefu na uchunguzi, kama ni ng’ombe hawamleti ndani, bali hutumwa mjumbe kwenda kujiridhisha kuwa anafaa.

Watu muhimu ambao sharti wapewe zawadi ambazo ni sehemu ya mahari ni pamoja na bibi wa binti ambaye hupewa blanketi, mama mzazi na mama mdogo ambao kila mmoja hupewa shuka au kitenge nyakati hizi, kaka mkubwa wa binti hupewa kanzu au kitambaa cha suti. Kila kipengele kitolewacho kwa mlengwa huambatana na kibuyu, au vibuyu vya pombe kama alivyoelekezwa mshenga. Baba akisharidhika na mawasilisho, msemaji wake ambaye tangu awali ndiye hutoa kauli, hupokea mahari na kuelekeza itolewe sebuleni.

Mali huvutwa ndani bila kunyanyuliwa kuashiria kupokewa huku vigelegele, vifijo na hoihoi vikirindima kutoka ukumbi wa akina mama. Mara hiyo, mshenga huongoza tena kundi lake kushukuru, na kushika miguu kwa mara nyingine.

Kaka wa binti huwapo mahali hapo, naye hushikwa miguu hata kama hajaoa. Warudipo kwenye nafasi zao, huletewa ‘akamwani’ hiki ni kitendo au cha kumkaribisha na kumkirimu mgeni na maongezi ya kawaida huendelea, pombe hugawiwa huku watu wakibadilishana mawazo kwa hiki na kile. Shughuli hii humalizika na mshenga kuingia tena sebuleni na kuomba kurejea alikotoka.

Huruhusiwa akiombwa asichelewe kuja kumchukua binti, maana sasa ni mali yake tayari. Wageni huondoka wakisindikizwa na wenyeji, lakini baba na mama wa binti huwa hawatoki nje. Tangu wakati huo, binti ambaye sasa huitwa mwali, huwekwa chini ya uangalizi mzuri zaidi, ikiwa ni pamoja na kupunguziwa kazi, kulishwa vizuri, kurembwarembwa ngozi yake hadi ilainike, na kufundwa na mama yake.

Wakirejea nyumbani mshenga hutoa taarifa ya safari yao, na kupongezwa. Sherehe huendelea hadi liamba. Wazee sasa huanza maandalizi ya kwenda kumchukua mwali ambayo ndiyo siku ya ndoa. Mwandishi ni msomaji na mchangiaji katika gazeti hili. Ni mwenyeji wa Mkoa wa Kagera na ni mwalimu mstaafu. Anapatikana kwa simu 0767547424.

foto
Mwandishi: Pontian Kashangaki

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi