loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kasi iongezwe kufundisha Kiswahili

MWAKA jana Zanzibar ilikuwa mwenyeji wa kongamano la kwanza la Kimataifa la Kiswahili kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yenye jumla ya wanachama sita, Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini.

Katika kongamano hilo ambalo linatarajiwa kufanyika pia mwaka huu, Waziri wa Uganda anayeshughulikia Afrika Mashariki, Kirunda Ali Kivejinja alizikumbusha nchi hizo kutumia lugha hiyo adhimu ya Kiswahili kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo.

Wanachama wa EAC wanaweza kutembea kifua mbele kwa kuwa na bahati ya pekee ya kujidai kwa kuunganishwa na lugha yao moja ya kibantu ya Kiswahili tofauti na nchi nyingine ambazo kwa mawasiliano wanalazimika kutumia lugha za kigeni zikiwemo Kiingereza na Kifaransa.

Tayari EAC pamoja na Umoja wa Afrika (AU) wameshapitisha pia lugha ya Kiswahili kuwa ni moja ya lugha rasmi zinazoweza kutumika katika vikao vyao. Katika kikao cha sasa cha AU kinachoendelea jijini Addis Ababa, Ethiopia, Kiswahili kinatumika kama moja ya lugha rasmi ya kikao hicho.

Aidha nchi za Sudan Kusini, Rwanda na Afrika Kusini zimeonesha wazi nia ya kutaka walimu wa Kiswahili kwenda kufundisha katika nchi hizo na kwa msukumo uliotolewa na Waziri Kivejinja kukuza lugha hiyo ya Kiswahili kwa nchi zote wanachama wa EAC, wigo wa mahitaji ya walimu kwa lugha hiyo umeongezeka zaidi.

Hakuna ubishi kwamba Kiswahili ni lugha ya wana Afrika Mashariki na kwa hatua hiyo ilifikiwa kila nchi ndani ya EAC ijisikie kuwa na jukumu la kuiendeleza, kuitumia na kuitangaza na kuvuka mipaka ya ndani na nje ya bara la Afrika.

Ingawa ni kweli pia kwamba nchi nyingine za EAC bado zinahitaji kuongeza jitihada katika matumizi ya Kiswahili, mazingira ya sasa na msukumo uliopo wa kukuzwa kwa lugha hiyo ni lazima uongezeke.

Tunapenda kusisitiza kuwepo kwa jitihada za makusudi za kuwaandaa vijana wetu kwenda kufundisha lugha hiyo katika shule na vyuo vyetu EAC, AU na vile vya nchi nyingine ili iweze kupata mizizi inayohitajika katika ukuaji na umuhimu wake.

Sisi tunaamini kwamba kazi iliyofanywa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kutumia lugha hiyo kuwaungamisha Watanzania katika harakati za kujinasua kutoka katika ukoloni, inaweza pia kutumika kuimarisha mshikamano na uhusiano wa wana EAC kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

Moyo na upendo wanaoendelea kuonesha viongozi wetu wakuu wawili wa EAC, Rais John Magufuli wa Tanzania na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kuitumia lugha hiyo katika mikutano mbalimbali ya hadhara inatosha kutoa hamasa kwa viongozi wakuu wa nchi nyingine za jumuiya hii kufanya hivyo pia kwa lengo lile lile la kutuleta pamoja na kujivunia lugha yetu ya Kiswahili.

RIPOTI ya 15 kuhusu uchumi wa Tanzania ya ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi