loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Watu binafsi kuuza gesi asilia vituoni

BIASHARA ya kuuza gesi asilia kwenye vituo kama ilivyo mafuta, imeshika kasi baada ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kuanza kutoa idhini kwa kampuni binafsi kufanya biashara hiyo.

Limesema kuwa linatarajia vituo hivyo, vitaanza kutoa huduma hiyo kuanzia Juni mwakani. Inaelezwa kuwa kampuni binafsi 24, tayari zimeonesha nia ya kufanya biashara hiyo na nyingi zikiwa zinazouza mafuta.

Kampuni hizo zipo tayari kuanza ujenzi wa vituo vya kuuza gesi hiyo, kwa ajili ya matumizi ya magari.

Kwa mujibu wa utaratibu, baada ya kutolewa tangazo kwa wenye nia kujitokeza, ni lazima TPDC itoe idhini kwa kampuni zilizoomba, kwani kwa mujibu wa sheria ndilo lina jukumu la kufanya biashara ya gesi asilia nchini. Lakini, kuna kipengele kinachoruhusu kampuni nyingine, kufanya biashara hiyo na tayari bodi ya TPDC imetoa idhini hiyo.

Akizungumza na Habari- Leo Afrika Mashariki jana, Meneja wa Biashara ya Gesi TPDC, Emmanuel Gilbert, alisema baada ya bodi kutoa idhini, kampuni zilizojitokeza moja moja zinapaswa kupeleka maombi maalum ili wapatiwe idhini, itakayowawezesha kupata leseni katika Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji nchini (Ewura).

Alisema wiki iliyopita, bodi yao ilikaa na kuidhinisha sekta binafsi, kufanya biashara ya gesi, kwa kila moja kupeleka TPDC maombi yanayoeleza uwezo wake wa kufanya biashara hiyo.

Gilbert alisema tayari kikao cha awali baina ya kampuni hizo 24, TPDC na Ewura, kimefanyika. Kwamba wawekezaji hao, wapo tayari kuanza ujenzi wa vituo, lakini ni lazima kwanza kupitia taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha biashara hiyo, inafanyika kwa kuzingatia viwango bora.

Alisema awali, sekta hiyo ilitaka Ewura kutoa leseni, kwa kuangalia viwango vya ujenzi wa vituo, lakini bei isidhibitiwe mpaka biashara itakapokomaa, lakini jambo hilo lilipingwa.

“Inatakiwa kuuza kwa bei isiyomnyonya mtumiaji, lakini na yeye (mfanyabiashara) apate faida, huku akihakikisha kituo kinakuwa na viwango kuepuka milipuko hivyo lazima kudhibitiwa na Ewura,” alisema.

Gilbert alisema baada ya kupatiwa leseni na Ewura, kampuni husika itatumia miezi sita kuagiza vifaa kwa ajili ya ujenzi na baadaye kuanza ujenzi, hivyo Februari mwakani ujenzi utaanza.

Meneja wa Biashara ya Gesi huyo wa TPDC, alisema kwa walivyojipangia Mei 30 mwakani ujenzi wa vituo hivyo vya kuuzia gesi asilia, utakuwa umekamilika kama hakutakuwa na changamoto, hivyo kuanza kutoa huduma kwa ajili ya magari na matumizi mengine.

Alisema mradi huo unaenda sambamba na ujenzi wa vituo vikubwa viwili vya kujaza mafuta vitakavyokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Kituo Kikuu cha Mabasi Yaendayo Mikoani Ubungo, kwa ajili ya kujaza kwenye mabasi ya mwendokasi, ambayo yatatumia gesi asilia mara atakapoanza kazi mwekezaji mpya ili kuepuka gharama.

Amesema usanifu wa michoro ya ujenzi wa vituo hivyo, unafanywa na kampuni kutoka Afrika Kusini. Baada ya kukamilika itatangazwa zabuni ya ujenzi wa vituo vitano, ikiwa ni pamoja na kituo kinginne cha Feri na Kibaha, kunapojengwa kiwanda cha dawa cha Kairuki.

Alisema katika vituo vikubwa viwili, kutakuwa na magari maalum yatakayobeba gesi na kupeleka kwenye vituo vidogo ili kuuzwa kwa wananchi

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, ametoa ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi