loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Yajayo elimu mkoani Mwanza yanafurahisha

Swali: Majukumu yako ni yapi?

Jibu: Mimi ni Ofisa Elimu Mkoa ninayeshughulikia seksheni ya elimu kimkoa inayotoa huduma ya elimu kwa jamii. Huduma hizo ni kusimamia utekelezaji wa sera ya elimu ndani ya mkoa kwa kushirikiana na viongozi wenzangu katika wilaya, halmashauri na mkoa; na wadau wote wa maendeleo ili kuhakikisha sera hiyo inatekelezwa huku lengo kuu likiwa ni kuwa na Mtanzania aliyeelimika, mwenye maarifa ya kumwezesha kuchangia katika kuleta maendeleo ya taifa.

Swali: Hali ya kitaaluma mkoani kwako ikoje?

Jibu: Kwanza niseme kuwa, Mkoa wa Mwanza una shule 982 za msingi. Kati ya shule hizo, 858 ni za serikali na shule 124 ni za binafsi. Shule za sekondari zipo 288. Kati ya hizo, 207 ni za serikali na shule 81 ni za binafsi. Katika shule za sekondari za serikali, 19 zina madarasa ya kidato cha 5 na 6. Idadi hii ya shule imeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2018, wakati shule za msingi zimeongezeka 16, shule tatu zikiwa ni za serikali na 13 za binafsi.

Upande wa sekondari zimeongezeka kutoka shule 11, saba za serikali na nne za binafsi. Aidha, mkoa una vituo shikizi 16 katika halmashauri za Buchosa, Ukerewe na Sengerema vinavyosaidia wanafunzi wenye umri mdogo kutotembea umbali mrefu ikiwa ni wanafunzi wa kuanzia madarasa ya awali hadi wale wa darasa la tatu.

Kwa ikama ya wanafunzi, mkoa una jumla ya wanafunzi 854,653 (wavulana 426,748 na wasichana 427,905) kwa shule za msingi, na kwa sekondari, wapo wanafunzi 160,120 (wavulana 82,505 na wasichana 77,615.

Swali: Vipi kuhusu uhitaji wa walimu?

Jibu: Kwa shule za msingi yapo mahitaji ya walimu 17,560, waliopo ni 12,684 na upungufu ni 4,878 (Mwanza Jiji kuna ziada ya walimu watatu). Shule za sekondari zinahitaji walimu 4,332 kwa masomo ya sanaa na waliopo ni 4,077, hivyo upungufu ni walimu 389 katika Halmashauri za Sengerema, Magu na Manispaa ya Ilemela. Kwa sayansi, mahitaji ni walimu 3,116 waliopo ni 1,351 na upungufu ni walimu 1,765 kwa halmashauri zote.

Masomo ya biashara yanayohitaji walimu 342. Kwa sasa waliopo ni 113 na upungufu ni 229, lakini pamoja na upungufu tulio nao katika Idara ya Elimu Msingi na Sekondari, bado walimu tulio nao wanaendelea kutimiza majukumu yao ya ufundishaji kama ilivyokusudiwa.

Swali: Kuna changamoto gani katika miundombinu?

Jibu: Kwanza pamoja na jitihada kubwa zilizofanywa na serikali kuu, jamii na wadau mbalimbali wa elimu katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, bado mkoa una upungufu mkubwa wa miundombinu. Katika shule za msingi upo upungufu wa vyumba vya madarasa 10,411, matundu ya vyoo 23,485 na nyumba za walimu 14,842. Sekondari upungufu wa vyumba vya madarasa ni 1,513, matundu ya vyoo 4,525, maabara 137 na nyumba za walimu 4,586.

Upo pia upungufu wa samani. Kwa shule za msingi, kuna upungufu wa madawati 73,365 na sekondari upo upungufu wa viti na meza 33,791 kwa kidato cha kwanza hadi cha nne na viti na meza 815 kwa wanafunzi wa kidato cha tano hadi cha sita.

Swali: Hali ya ufaulu kimkoa ikoje?

Jibu: Jumla ya wanafunzi wa darasa la saba 67,383 sawa na asilimia 98.8 ya waliosajiliwa, walifanya mtihani kuanzia Septemba 11- 12 mwaka jana. Wanafunzi 56,556 sawa na asilimia 83 walifaulu mtihani huo. Kuhusu matokeo ya kidato cha sita mwaka jana, wanafunzi 5,202 walifaulu mtihani huo ikiwa ni sawa na asilimia 97.8 ya wanafunzi 5,317 waliofanya mtihani huo. Ufaulu huo ni ongezeko la asilimia 3.0 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2018 ambapo wanafunzi walifaulu kwa asilimia 94.8.

Swali: Vipi kuhusu utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo mkoani kwako?

Jibu: Tunaishukuru sana serikali kuu imekuwa msaada mkubwa katika utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo. Katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2019, serikali kuu ilitoa fedha za ruzuku chini ya Mpango wa Elimu Msingi Bila Malipo kwa mkoa wetu; jumla ya Sh bilioni 5.4 kwa shule za msingi na bilioni 6.6 kwa shule za sekondari ikiwa ni wastani wa Sh bilioni 1.3 kwa mwezi.

Swali: Mkoa una mikakati gani ya kuboresha elimu?

Jibu: Idara ya elimu tumejiwekea mikakati mbalimbali ya ufuatiliaji shughuli za kielimu ili kuhakikisha kamati za shule/ bodi za shule zinahimiza wazazi na wananchi kwa jumla, kujenga hosteli kwa ajili ya kuwanusuru wanafunzi hasa wa kike kutotembea umbali mrefu kwenda na kutoka shuleni. Kamati na bodi hizo pia zitawahimiza wazazi kuchangia chakula cha mchana kwa wanafunzi wa kutwa ili kupunguza utoro.

Mikakati mingine ni kamati za taaluma za halmashauri kufanya ufundishaji makini unaozingatia mfumo wa utungaji wa mitihani ya Baraza la Taifa Mitihani (Necta) inayoimarisha uwezo wa wanafunzi na kutoa mazoezi ikiwemo mitihani ya mara kwa mara, kuhimiza halmashauri kuandaa utaratibu wa wanafunzi watahiniwa wa shule za kutwa (Darasa la saba, kidato cha tano na sita) kuwa na kambi za kulala shuleni miezi miwili kabla ya kufanya mitihani yao.

Swali: Nini mwito wako kwa wadau wa maendeleo ya elimu?

Jibu: Idara ya elimu mkoa tunawaomba wadau na jamii kwa jumla, kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuchangia rasilimali fedha, vifaa na nguvu kazi ili kukabiliana na changamoto katika sekta ya elimu katika mkoa wetu. Mengine yanayohitajika katika utatuzi wa changamoto hizo ni pamoja na samani za shule, miundombinu ya maji na umeme, vifaa vya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) kama kompyuta, mashine za kurudufishana, ‘scanner’ na usafiri kwa wanafunzi.

Swali: Miundombinu kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza ikoje?

Jibu: Kwa mwaka huu haitoshelezi kwa halmashauri za Buchosa, Ilemela, Kwimba, Magu, Misungwi na Jiji la Mwanza. Uwiano wa wanafunzi wanaotakiwa kwa chumba kimoja ni 50 (1:50), mahitaji ya vyumba vya madarasa kwa wanafunzi 44,149 wanaotegemea kuanza kidato cha kwanza kwa halmashauri hizo ni 883 na vyumba vilivyopo ni 392.

Hivyo, hadi Januari tulikuwa na upungufu wa vyumba 491. Sengerema na Ukerewe zenyewe hazina upungufu, zina ziada. Tumejenga hosteli kwa ajili ya wanafunzi wanaotoka mbali na hadi Julai mwaka jana, zilikuwepo hosteli 47 na zinazoendelea kujengwa ni 18.

HUDUMA bora za afya ya msingi zinapunguza uhitaji, gharama na ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy, Mwanza

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi