loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Unyonyeshaji, lishe bora mwarobaini wa udumavu

“WAKATI mwingine mwalimu anaweza kumchapa na kumpa adhabu kali mtoto darasani akidhani anafanya makusudi kutokuelewa anachofundishwa, kumbe akili yake imedumaa kwa kukosa lishe,” kimeandika chanzo kimoja cha mtandao kikimnukuu mtaalamu kutoka Jukwaa la Lishe Tanzania (Panita), Debora Essau.

Kinamnukuu pia mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Tuzie Edwin akisema, watoto wenye udumavu huwa na uwezekano mkubwa wa kuugua magonjwa mengine sugu yasiyo ya kuambukiza na ambayo ni hatari kama moyo na saratani hata wakiwa wakubwa.

Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA) katika kitabu chake kiitwacho, ‘Mtindo wa Maisha na Magonjwa Yasiyoambukiza: Dalili, Athari na Kinga; Elimu kwa Jamii,’ linayataja mambo yanayochochea ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kuwa ni pamoja na ulaji usiofaa, kutofanya mazoezi, matumizi ya pombe, tumbaku na dawa za kulevya; msongo wa mawazo na kutopata usingizi.

Mkala haya yatajikita namna unyonyeshaji na lishe kwa mjamzito na mtoto katika siku 1,000 tangu mimba kutungwa unavyohusiana na tatizo la udumavu. Hili ni tatizo linalowapa mzigo mkubwa watoto wanapokuwa wakubwa kwani udumavu huathiri hata kufikiri kwa mtoto huyo, kukumbuka mambo, kutafakari na hata kuelewa haraka masomo darasani.

Kimsingi, udumavu ni hali ya kudumaa kwa maendeleo ya mtoto kimwili na kiakili inayomfanya awe mfupi kuliko umri wake. Sababu ya hali hii huweza kumkumba mtoto akiwa bado tumboni mwa mama yake endapo wakati wa ujauzito mama huyo hakupata lishe bora.

Wataalamu wa lishe wanahimiza ikiwezekana mama hata kabla ya kupata ujauzito ajiandae kwa vyakula bora na kuendelea hadi anapojifungua, kisha kumnyonyesha maziwa pekee kwa miezi sita na kuendelea kumpa chakula bora hadi anapofikisha miaka miwili kamili ambazo ni siku 1,000 zinazoanzia siku mama anapata ujauzito. Kibaya zaidi, mtoto akishadumaa, hata baadaye akila na kunenepa hali hiyo, hususani kudumaa kwa akili hakuwezi kurekebishika.

Kwa mujibu wa vitini vilivyotolewa katika mkutano wa viongozi wa dini kujadili malezi bora ya watoto sambamba na nafasi muhimu ya akina baba katika malezi ili kujenga taifa imara ulioandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Interfaith Partnership (TIP) kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), theluthi moja ya watoto nchini Tanzania (milioni 3) wamedumaa.

Hii ina maana kuwa, ni wafupi ukilinganisha na umri wao na cha kushangaza, wengi wao wanaishi katika mikoa hodari kwa kilimo, hivyo kwao tatizo siyo upungufu wa chakula bali namna ya kukukitumia.

Tanzania Interfaith Partnership (TIP) ni shirika lisilo la kiserikali linalozihusisha taasisi nne za dini nchini ambazo ni Ofisi ya Mufti wa Zanzibar (MoZ), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).

Kitini cha Malezi kwa Mtazamo wa Kikristo kinasema: “Ni asilimia 59 yaani watoto sita kati ya kumi ambao hunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo, hii ina maana kuwa asilimia 40 wana kinga ya mwili ambayo ni pungufu kukabili magonjwa.”

Nacho Kitini cha Malezi kwa Mtazamo wa Kiislamu kinasema: “Ni asilimia 21; watoto wawili katika ya kila watoto kumi tu ya watoto wenye umri wa miezi sita hadi 23 wanaoishi vijijini, wanaokula mchanganyiko wa vyakula mbalimbali.”

Vitini vyote viwili vinasisitiza unyonyeshaji maziwa ya mama wa mapema na pekee kwa miezi sita ya mwanzo, humwandalia mtoto mwanzo mzuri wa maisha, hivyo, unapaswa kuendelea hadi mtoto afikishe miaka miwili.

Baada ya kutimiza miezi sita, mlo wa mtoto unatakiwa uwe na mchanganyiko wa vyakula mbalimbali. Kwa mujibu wa vitini hivyo, watoto wadogo wanahitaji mboga mboga, maharage, matunda, mayai (ya kuku wa kienyeji), maziwa, samaki na dagaa ili kukua vyema kimwili na kiakili.

Ugali, wali, viazi na uji pekee havitoshi. Hata kile watu wanachoita unga wa lishe bila kumpa mtoto aliyeanza kula matunda na mbogamboga si sahihi. Unga unaoitwa wa lishe mara nyingi huwa na wanga na protini, lakini kunakosekana vitamini na madini ya kutosha, vitu ambavyo ni muhimu sana kwenye mwili wa mtoto na vinapatikana zaidi kwenye matunda na mbogamboga.

Katika mkutano huo uliofanyika Dar es Salaam Alhamisi iliyopita, ilibainika kuwa hata vitabu vitakatifu na viongozi wa dini wanahimiza unyonyeshaji bora ili kulinda afya za watoto na kupata taifa imara. Inasisitizwa kuwa akina mama waanze mara moja kuwanyonyesha watoto wachanga takribani saa moja baada ya kujifungua.

Unyonyeshaji wa mapema humpatia mtoto mchanga maziwa ya awali yenye rangi ya njano yenye virutubisho maalumu vinavyoweza kumlinda mtoto dhidi ya magonjwa na husaidia pia kusisimua utokaji wa maziwa wa mara kwa mara, jambo ambalo hutokea katika siku ya pili au ya tatu baada ya mtoto kuzaliwa.

Mintarafu suala hili, Kitini cha Malezi kwa Mtazamo wa Kikristo kinasema: “Maziwa ya mama ndicho kitu pekee anachohitaji mtoto ili kukua vyema kimwili na kiakili katika miezi sita ya mwanzo wa maisha yake; hawahitaji chakula kingine wala maji…” Kinaongeza: “Baada ya miezi sita, akina mama wanapaswa kuendelea kuwanyonyesha watoto wao huku wakianza kuwapa vyakula mchanganyiko.”

Nacho Kitini cha Malezi kwa Mtazamo wa Kiislamu kinasema: “Mlo kamili wenye vyakula mbalimbali husaidia ubongo na mwili kukua vizuri. Watoto wasiokula mchanganyiko wa vyakula kuanzia miezi sita hadi miaka mitatu, wako katika hatari ya kudumaa. Hali hii huathiri ukuaji mzuri wa kiakili na kimwili wa watoto na watoto waliodumaa hawafanyi vizuri darasani.”

Ndiyo maana katika mkutano huo Mtaalamu wa Saikolojia, Betty Jayne na Ofisa wa Hifadhi ya Mtoto katika UNICEF Tanzania, Ofisi ya Zanzibar, Ahmed Rashid Ally, wanasema wazazi na walezi hususani walimu, hawapaswi kutanguliza hasira na kuwaadhibu watoto, bali kuwalea, kuwakanya na kuwaelekeza kwa upendo.

Vitini hivyo vinabainisha kuwa, maeneo ya mijini, hata watoto wadogo mara nyingine hupewa vinywaji vya sukari, vyakula vilivyokaangwa kwa mafuta mengi, biskuti, pipi na keki wakati vitu hivyo havina umuhimu katika miili yao.

“Wazazi wanaweza kufikiri kuwa wanafanya jambo jema, la hasha, vyakula hivyo siyo vizuri kwa watoto,” kinasema Kitini cha Malezi kwa Mtazamo wa Kikristo. Nacho Kitini cha Malezi kwa Mtazamo wa Kiislamu kinaongeza: “Kama wakila vitu vya aina hiyo kwa wingi sana, huwapunguzia hamu ya kula vyakula bora, pia wanaweza kuwa na uzito mkubwa kupita kiasi na kupata magonjwa sugu kama kisukari na ugonjwa wa moyo.”

Aidha, katika semina ya hivi karibuni kwa waandishi wa habari wanachama wa Taasisi ya Kuelimisha Jamii Kuhusu Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TOANCD) iliyoandaliwa na TANCDA kuwajengea uwezo, Mtaalamu wa Chakula na Lishe, Mary Materu anasema ni muhimu watu wote wakiwamo wajawazito kula vyakula kutoka makundi yote kadiri inavyoshauriwa kitaalamu kwa kila mlo. Materu anasisitiza “… Siyo sawa kula nafaka zilizokobolewa, kutengeneza juisi za matunda; juisi siyo mbadala wa matunda na epuka kuongeza sukari kwenye vyakula au vinywaji. Kwa mtu mzima inashauriwa sukari isizidi vijiko vya chai vitano kwa siku.”

Katika mada walizozitoa kwa nyakati tofauti kwenye semina hiyo, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza, Profesa Andrew Swai na Dk Mashombo Mkamba, wanasema ni muhimu hata wajawazito kupata milo inayofaa ili kuimarisha afya zao na watoto wao walio tumboni. Tukirudi na kujikita katika unyonyeshaji, inaelezwa katika vyanzo mbalimbali kuwa lishe bora huhitajika kwa mjamzito ili kuimarisha afya yake na ya mtoto na pia, humwezesha mtoto aliyezaliwa kuepuka matatizo ya kiafya ukiwamo udumavu na mengine.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), baadhi ya faida za kunyonyesha mtoto maziwa ya mama ni pamoja na kuwa maziwa ni chanzo cha lishe bora kwa watoto, hupunguza hatari ya kushikwa na magonjwa, hushinikiza uzito wenye afya na yana uwezo wa kumfanya mtoto awe mwerevu.

Faida nyingine za maziwa ya mama kwa mtoto ni kumsaidia mama kupunguza uzito mwilini na kupunguza hatari ya mama anayenyonyesha kuugua msongo wa mawazo. Tafiti pia zinaonesha kwamba kunyonyesha humpunguzia mwanamke hatari ya kupata saratani ya matiti.

HUDUMA bora za afya ya msingi zinapunguza uhitaji, gharama na ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi