loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ujue wingi unaofaa wa aina za vyakula katika mlo

ULAJI usiofaa ni miongoni mwa sababu za kuwapo kwa magonjwa yasiyoambukiza ambayo kwa mujibu wa takwimu Shirikisho la Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), yanasababisha asilimia 27 ya vifo vyote.

Kitabu: ‘Mtindo wa Maisha na Magonjwa Yasiyoambukiza; Dalili, Athari na Kinga; Elimu kwa Jamii’ kinasema: “Tafiti za mwaka 2012 zilionesha kuwa, kwa kila watu 100 wenye umri wa miaka 25 na kuendelea, 9 wana kisukari, 26 wana shinikizo la damu, 25 wana mafuta yaliyozidi kwenye damu, na 34 wana uzito uliozidi.”

Sababu za magonjwa haya zinatajwa kuwa ni hasa mabadiliko ya mtindo wa maisha kama kutofanya mazoezi, ulaji usiofaa, matumizi ya pombe, tumbaku na dawa za kulevya, msongo wa mawazo na kutopata usingizi wa kutosha. Mintarafu ulaji, kila chakula kutoka kila kundi kina kiasi chake kinachoshauriwa ili kupata aina zote za virutubishi vinavyohitajika mwilini.

Kwa mfano, TANCDA katika chapisho hilo inaelimisha ikisema, kiasi cha chakula chenye wanga kinachofaa katika mlo mmoja ni kiasi cha ngumi mbili huku kiasi cha protini kikiwa ni ujazo wa mkono mmoja, upana wa kidole kidogo. Kwa mujibu wa kitabu hicho, kiasi cha mbogamboga kinachofaa kwa mlo mmoja ni kiasi cha kujaza mikono yote miwili ya mlaji.

Katika mafunzo ya hivi karibuni kwa wanachama wa Taasisi ya Kuelimisha Jamii Kuhusu Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TOANCD) iliyoandaliwa na TANCDA kuwajengea uwezo, Mtaalamu wa Chakula na Lishe, Mary Materu anasema: “Matunda na mbogamboga za msimu zinapatikana kwa wingi msimu wa mvua, lakini watu wanafanya kosa kuzidharau.”

“Ni vyema kutumia matunda au mbogamboga zinazopatikana hasa za asili zikiwamo zilizosahaulika…. Changanya kadiri zinavyopatikana; mfano, pata matembele, kunde, majani ya maboga, bamia na mlenda…,” akasema.

Kuhusu matunda ambayo kiasi kinachoshauriwa kufaa kwa mlo mmoja ni ukubwa wa ngumi moja, Mary anasema: “Tusijikite sana kusaga matunda kuwa juisi; ukinywa juisi ujue umekula kama sehemu moja ya tano ya tunda maana juisi si mbadala wa matunda; matunda ni pekee na muhimu hasa zile nyuzi zake ambazo mara nyingi hutolewa unapotengeneza juisi…”

Kuhusu mafuta, kiasi kinachotajwa kufaa kwa mlo ni ukubwa wa mwisho wa kidole gumba. Hata hivyo, Mwenyekiti wa TANCDA, Profesa Andrew Swai anasema: “… usizidishe mafuta katika vyakula… mafuta huganda kwenye mishipa ya damu; yakizidi yanaweza kuziba mishipa. Jitahidi kuepuka mafuta yatokanayo na wanayama kwani yana lehemu nyingi; badala yake, pendelea kutumia mafuta yatokanayo na mimea.”

Profesa Swai anasisitiza: “… Usikoboe nafaka ... magamba yaliyo kwenye vyakula huzuia sukari isipatikane haraka. Kukoboa pia hupoteza protini, vitamini na madini yaliyo kwenye maganda yaliyoondolewa.”

Anaongeza: “Magamba kwenye nafaka, matunda na mboga huwa na nyuzinyuzi ambazo husaidia kupata choo kwa urahisi na hivyo, kuepusha sumu kurudi mwilini na kusababisha saratani ya utumbo mkubwa, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.”

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi