loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hatma ya Kinana, Membe, Makamba baada siku 7

HATMA ya makada wakongwe watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, Yusuf Makamba na Benard Membe itajulikana baada ya siku saba zijazo.

Itajulikana baada ya Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu, kukamilisha taarifa inayowahusu na kuikabidhi kwa vikao husika.

Kamati hiyo inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, kwa kipindi cha wiki nzima imekuwa kwenye mchakato wa kuwahoji wanachama hao kutokana na kukabiliwa na tuhuma mbalimbali.

Desemba mwaka jana, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM iliagiza makada hao watatu kuhojiwa, kutokana na kukabiliwa na tuhuma za maadili kwa mujibu wa Katiba ya Chama na Kanuni ya Maadili na Uongozi.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole Desemba 13, mwaka jana, hata hivyo haikueleza bayana ni makosa gani ya kimaadili ambayo wanatuhumiwa nayo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, makada wengine watatu, January Makamba, Nape Nnauye na William Ngeleja walisamehewa baada ya kumuomba radhi Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais John Magufuli.

Wanachama hao waliomba radhi kwake (Magufuli) baada ya “kukiri mbele yake kufanya makosa ya kimaadili, yaliyokidhalilisha chama na viongozi wake mbele ya umma”.

Wanachama hao inadaiwa sauti zao, za wakifanya mawasiliano kwa njia ya simu, zilinaswa na zilivujishwa kwenye mitandao nchini, wakizungumzia masualambalimbali kuhusu chama na mwenyekiti.

Sehemu ya mazungumzo yaliyovuja ya Mzee Makamba na Kinana ni pamoja na kuandaa taarifa ya malalamiko dhidi ya mwanaharakati huru, Cyprian Musiba ambaye wanamtuhumu kwa ‘kuwadhalilisha’ bila kuchukuliwa hatua yoyote na kuhoji analindwa na nani.

Awali Musiba aliwatuhumu makada hao kuwa wanamhujumu Mwenyekiti wa chama, Rais Magufuli , madai ambayo makada hao waliyachukulia kama wamedhalilishwa.

Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje Membe, licha ya kusikika kwenye mazungumzo hayo yaliyovuja, amekuwa pia akituhumiwa na baadhi ya wanachama kuwa anajipanga ‘kumhujumu’ Rais Magufuli katika uchaguzi mkuu, uutakaofanyika mwaka huu.

Membe alikuwa wa kwanza kuhojiwa Alhamisi iliyopita na kamati hiyo jijini Dodoma. Baada ya mahojiano hayo yaliyochukua saa tano, waziri huyo wa zamani alibainisha kuwa amefurahia hatua hiyo, hasa mijadala iliyoibuka ya kulijenga taifa.

“Nimepata nafasi nzuri ya kufafanua mambo kadhaa ambayo chama changu kilitaka kuyajua...Safari hii ya kuja Dodoma imekuwa na manufaa makubwa sana, sana kwangu, kwa chama na kwa taifa letu...mengine yatakuwa yanapatikana kidogo kidogo nikishiba,” alisema Membe.

Hata hivyo, mahojiano ya Kinana na Makamba hayakufanyika kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na awali na Mangula. Hali hiyo iliibua sintofahamu, ikiwemo uvumi kwamba wazee hao wamejivua uanachama.

Siku nne baada ya minong’ono na uvumi kuhusu vigogo hao wa CCM, hatimaye walijitokeza juzi Lumumba Dar es Salaam katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM na kutii agizo la kamati hiyo la kuwahoji.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Polepole alieleza kuwa tayari Kamati Kuu iliyoketi jana chini ya uongozi wa Rais Magufuli, imepokea taarifa ya utekelezezaji wa Azimio la NEC kuhusu kuwaita na kuwahoji wanachama hao watatu Kinana, Makamba na Membe.

Aliongeza kuwa baada ya kamati hiyo, kupokea taarifa hiyo, ilitoa siku saba kwa Kamati hiyo ya Nidhamu kushughulikia suala hilo.

Aidha, katika taarifa hiyo, Polepole alieleza kuwa kikao hicho cha Kamati Kuu pamoja na kujadili suala hilo, pia kilipokea taarifa ya Maandalizi ya Mwelekeo wa Sera za CCM kwa Mwaka 2020 – 2030 na Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Kamati hiyo pia ilipitia Uandishi wa Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na kuagiza maoni ya wadau mbalimbali, kujumuishwa na kuzingatia ratiba ya kukamilisha uandishi wake ili vikao vya chama, vifanye uamuzi na kupitisha.

“Pia ilipitia na kupokea maombi ya kujiunga uanachama wa CCM kutoka kwa Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye, wanachama na viongozi wa vyama vingine vya siasa” alisema. Sumaye alirejea CCM juzi.

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro na Halima Mlacha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi