loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Madiwani 5 ACT- Wazalendo wajiunga CCM

CHAMA cha ACT Wazalendo kimepata pigo baada ya madiwani watano wa Kigoma Ujiji, kujivua uanachama na udiwani, kwa kile walichoeleza ni kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.

Madiwani hao jana walikwenda Ofisi Ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam kutangaza uamuzi huo.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally amesema madiwani hao ni wa Kata za Kasingirima, Kagera, Kasimbu, Kipampa na Gungu, zote za Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Hatua ya kujiengua kwa madiwani hao, imeiporomosha ngome ya ACT Wazalendo Kigoma, ambayo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, iliibuka na ushindi katika kiti cha ubunge ,ambacho Zitto Kabwe alikinyakua.

Wakizungumzia sababu za kujiengua ACT na kuomba kujiunga na CCM, madiwani hao walisema wamechukua hatua hiyo, kwa lengo la kuunga mkono kazi zinazofanywa na Rais Magufuli.

“Mimi sioni ‘future’ (mustakabali) wa kesho nikiwa ndani ya ACT kwenye mpango mzima wa kuleta maendeleo Kigoma Ujiji na taifa kwa ujumla. Kwa busara na uamuzi wangu nimeamua kuondoka,” amesema Rashid Hamis, ambaye ni Diwani wa Kata ya Gungu.

Alisema chini ya Rais Magufuli hivi sasa upelekaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, unakwenda kwa uwiano nchini na kwa kasi kubwa, bila ubaguzi wowote.

Hamduni Nassoro, Diwani wa Kata ya Kasingirima, alisema ameamua kung’atuka ndani ya ACT Wazalendo ili kuongeza wigo wa fursa za maendeleo Kigoma Ujiji, badala ya kuwa kikwazo cha utekelezaji kwa ufanisi.

Kwa upande wale, Ismail Hussein ambaye ni Diwani wa Kata ya Kagera alisema amechukua uamuzi huo, kwa lengo la kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais Magufuli katika kutekeleza ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo kununua ndege, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na mradi wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere huko Rufiji.

Madiwani wengine waliojiengua ACT ni Fuad Nassoro wa Kata ya Kasimbu na Mussa Ngongolwa wa Kata ya Kipampa. Nao walipongeza juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli katika kuboresha maisha ya wananchi, kwa kuwapelekea maendeleo.

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi