loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Moto wateketeza bidhaa za mamilioni sokoni

JIJI la Mwanza jana lilikumbwa na taharuki baada ya moto kuzuka katika soko la wafanyabiashara wadogo (machinga) eneo la Makoroboi.

Moto huo ulisababisha hasara kwa kwa umeteketeza bidhaa za aina mbalimbali na baadhi ya vibanda vya wafanyabiashara hao.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro amesema hayo jana alipozungumza kwenye eneo la tukio kwenye Msikiti maarufu wa Wahindi.

Muliro aliwapa pole wafanyabiashara hao, kwa kupoteza mali zao. Alisema moto kwenye soko hilo, ulizuka majira ya saa 10:00 alfajiri.

Kamanda huyo alisema Jeshi la Zimamoto kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), walifanikiwa kudhibiti moto huo.

Alisema uchunguzi wa awali uliofanywa, unaonesha kuwa moto huo umesababishwa na hitilafu ya umeme, iliyotokana na majokofu yaliyokutwa kwenye soko hilo, ambayo inadaiwa hayakuzimwa.

“Tunaendelea na uchunguzi zaidi na hakuna vifo vilivyotokea kwenye tukio hili,” alisema. Alisema tukio hilo la moto, limeathiri eneo lenye upana wa mita 80 na urefu wa mita 15 kutoka upande wa kushoto na kulia.

Aliwahakikishia wakazi wa jiji la Mwanza, kuwa ulinzi umeimarishwa katika eneo hilo ili kudhibiti bidhaa na mali za wafanyabiashara hao hadi pale serikali itakapofanya tathimini, kujua hasara ya mali iliyosababishwa na moto huo.

Kamanda Muliro alisema watu zaidi ya 150, wamepata hasara kwenye tukio hilo, kwa bidhaa zao kuchomwa moto.

Aliwataka wafanyabiashara hao kuwa na miundombinu rafiki, ambayo haiwezi tena kuwaletea madhara ya aina hiyo.

Kamanda wa Kikosi cha Jeshi la Zima Moto Mkoa wa Mwanza, Ambwene Mwakibete alisema imebainika kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme.

Aliwashauri wananchi wanapotaka kupata huduma ya umeme, wafuate taratibu zote zinazotakiwa ili taratibu za kiusalama ziweze kuzingatiwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk. Philis Nyimbi alitoa pole kwa waathirika kwa bidhaa zao kuteketea kwa moto.

Alitoa pole hizo kwa niaba ya uongozi wa serikali ya mkoa. Alisema Jeshi la Zimamoto kwa kushirikiana na Shirika la Umeme (Tanesco), watakaa kwa pamoja ili kutafuta chanzo kilichosababishwa na moto huo, ikiwemo madai ya baadhi ya wafanyabiashara kujiunganishia umeme bila ya kufuata taratibu.

Alisema jumla ya vibanda 65 na wafanyabiashara 159 wameathiriwa na moto huo kwa kupoteza bidhaa na mali zao.

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy, Mwanza

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi