loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dar, Pwani kuboresha daftari kuanzia kesho

KAZI ya kuboresha daftari la wapigakura kwa jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani inaanza kesho kwa siku saba na muda hautoongezwa, huku wananchi wakihimizwa kujitokeza ili kuweza kushiriki kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Uboreshwaji huo utafanyika hata siku za mwisho wa wiki na hata kama kuna sikukuu. Ofisa Elimu, Idara ya Habari na Elimu ya Mpigakura kutoka Tume ya Uchaguzi (NEC), Titus Mwanzalila amesema hayo wakati wa kutoa mafunzo kwa wakufunzi wa wananchi kuhusu daftari la kupigia kura, mafunzo yaliyoandaliwa na Mtandao wa Uangalizi wa Uchaguzi Tanzania(TACCEO).

Akizungumza Mwanzalila alisema ni vema wananchi wa mikoa hiyo wakatumia vema siku hizo ili kujihakikishia kuwa na sifa kupiga kura.

Alitaja makundi yanayotakiwa kujiandikisha kuwa ni pamoja na waliopoteza kadi zao, kuboresha taarifa za watu ambao majina yao yapo kwenye daftari lakini wamefariki dunia, waliohama vituo vyao vya awali na wale watakaotimiza umri wa miaka 18 ifikapo Oktoba mwaka huu.

Alisema kazi hiyo ya kuboresha daftari ni kwa awamu ya kwanza na uboreshwaji mwingine utafanyika Machi mwaka huu na kusisitiza wote kutumia fursa hiyo ili kuhakikisha wanajiandikisha na kupata haki ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu.

Alisema katika utekelezwaji wa kazi hiyo haihitajiki kwenda na nyaraka yoyote kwa ajili ya kuboresha ila kwa yule aliyepoteza kadi anahitajika kutaja majina kamili kama yalivyokuwa kwenye kadi ili aweze kupewa nyingine.

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi