loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

SMZ yaombwa kuruhusu kuagiza mchanga nje

KAMATI ya Baraza la Wawakilishi ya Fedha, Kilimo na Biashara imeishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuruhusu watu binafsi kuagiza mchanga nje ya nchi au Tanzania Bara kumaliza upungufu wa rasilimali hiyo unaokwamisha utekelezaji wa baadhi ya miradi ya ujenzi ya serikali na sekta binafsi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini amesema hayo akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo na kusema tatizo la uhaba wa mchanga ni kubwa likitishia kuzorota kwa baadhi ya miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa shule.

Amesema miradi ya ujenzi wa shule za sekondari 12 inayotekelezwa na washiriki wa maendeleo imeanza kusuasua kwa uhaba wa mchanga.

Ametoa mfano mradi wa ujenzi wa chuo cha elimu mbadala Kibuteni Makunduchi katika Mkoa wa Kusini Unguja unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Alisema ujenzi wa chuo hicho umedorora kwa sababu ya upungufu wa mchanga, kwa mujibu wa wakandarasi wanaoendelea na ujenzi huo.

“Zanzibar tuna na uhaba wa rasilimali ya mchanga na njia pekee ya kulipatia ufumbuzi tatizo hilo ni kuiomba serikali kuwaruhusu watu binafsi kuingiza mchanga, ikiwemo kutoka Tanzania Bara kwa kuweka utaratibu,” alisema.

Alisema kinachotakiwa kufanywa na serikali ni kuweka utaratibu mzuri kuingiza mchanga huo kutoka nje na kuweka mwongozo wa sheria ili kuepuka athari za kimazingira kujitokeza.

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walikubaliana na ushauri wa kamati hiyo ambapo mwakilishi wa jimbo la Paje, Jaku Hashim Ayoub alisema uhaba wa rasilimali ya mchanga unatishia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya serikali na sekta binafsi.

“Mimi nakubaliana moja kwa moja na ushauri uliotolewa na Kamati ya Fedha, Kilimo na Biashara ya Baraza la Wawakilishi, wakati umefika tuagize mchanga nje kukabiliana na uhaba uliosababisha changamoto ikiwemo kuchelewa kwa miradi ya serikali,” alisema.

Aidha mwakilishi wa jimbo la Shaurimoyo, Hamza Hassan Juma aliitaka wizara kuweka utaratibu mzuri wananchi wa kawaida kupata huduma za mchanga kwa shughuli za ujenzi.

Alisema utaratibu uliopo sasa wa wananchi kupata mchanga umekuwa na urasimu mkubwa ikiwemo kuandika barua kutoka kwa viongozi wa shehia ambapo alisema haiwezekani mwananchi wa kawaida anahitaji mchanga wa kiwango kidogo cha kujenga nyumba yake lazima awasilishe barua ya kuomba mchanga.

Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Dk Makame Ali Ussi alisema machimbo ya mchanga Kichwele Mkoa wa Kaskazini Unguja yatafungwa kuzuia athari za mazingira.

Alisema baadhi ya machimbo yaliyokuwa yakizalisha mchanga umefanyika uharibifu mkubwa ikiwemo kuchimba mchanga kwenda chini hadi mita tatu na kusababisha kutoa maji.

“Wizara inalifahamu tatizo la uhaba wa mchanga nchini na juhudi zinachukuliwa kuona njia ya kulipatia ufumbuzi ikiwemo kuepuka athari za kimazingira, kwani Zanzibar ni kisiwa kidogo ambacho kama hatua sahihi hazitachukuliwa ipo hatari kubwa,”alisema.

KAMPUNI ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya umeme cha Kilimanjaro ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi