loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Polisi yawakalia kooni wahujumu Tazara

WATU wanaoharibu na kuiba vifaa katika miundombinu ya reli ya Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara) kwa ajili ya vyuma chakavu na hujuma wameonywa kuacha mara moja kabla sheria haijachukua mkondo wake dhidi yao.

Aidha, wananchi wanaoishi kando ya miundombinu hiyo wameombwa kuwafichua wahujumu na wezi hao kwa kuwa uharibifu wanaoufanya unahatarisha maisha ya Watanzania na uchumi wa nchi.

Onyo hilo limetolewa juzi na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Tazara, Advera Bulimba wakati wa ziara ya kimafunzo katika mitambo ya kuzalisha kokoto na mataruma ya reli eneo la Kongoro jijini Mbeya.

Kamanda Bulimba alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wananchi kujihusisha na vitendo vya uhalifu vya kung’oa na kuiba miundombinu ya reli na kwenda kuuza kama vyuma chakavu, jambo ambalo linadhoofisha utendaji wa reli ya Tazara.

“Madhara ya kuhujumu reli ni makubwa na yanaweza kugharimu maisha ya watu na kusababisha ulemavu wa kudumu, jambo hilo halitakubalika chini ya uongozi wa kikosi cha Polisi Tazara,”alisema.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Reli ya Tazara, Fuad Abdallah akiwa katika ziara hiyo, aliwataka wafanyakazi wa kiwanda cha kuzalisha kokoto na mataruma ya reli kutumia vizuri na kuitunza mitambo hiyo iliyonunuliwa kwa gharama kubwa ili iweze kutumika kwa muda mrefu.

Abdallah aliwataka wafanyakazi wa kiwanda hicho kuendelea kufanya kazi kwa kujituma na kutunza mitambo hiyo kwa kuwa kiwanda hicho ndiyo ‘roho’ ya Tazara katika kuimarisha miundombinu ya reli.

Wakati Tazara ikitoa angalizo hilo kuhusu hujuma katika miundombinu, Shirika la Reli Tanzania (TRC) mwishoni mwa mwaka jana ilisema reli ya kaskazini ilihujumiwa baada ya kung’olewa mataruma saba na vifaa vya kuunga reli na reli katika maeneo mbalimbali.

Kutokana na matukio hayo, makamanda wa polisi katika mikoa inakopita miundombinu hiyo kwa kushirikiana na kikosi cha Polisi cha reli ya TRC, walianzisha elimu na ulinzi shirikishi kwa wakazi wa karibu na reli hiyo ili kuimarisha ulinzi na kuwafichua wahujumu.

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments