loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Matumizi ya istilahi za kigeni yalivyofifisha zile za Kiswahili

Utangulizi Maana ya jumla ya neno istilahi ni msamiati, lakini msamiati huu unajikita katika uwanja maalumu. Hivyo kama ukiulizwa maana ya istilahi utajibu kwa usahihi kuwa istilahi ni msamiati wa uwanja maalumu wa taaluma kama vile, utabibu, uhandisi, kilimo, ufugaji, mazingira na ufundi.

Kwa kifupi ni maneno maalumu ambayo yanarahisisha kutotaja kitu kwa maneno mengi, kwa mfano badala ya kusema mbuzi wangu anaumwa ugonjwa wa kuvimba miguu unaoambukizwa na bakteria, unasema mbuzi wangu anaumwa chambavu.

Halikadhalika badala ya kutoa maelezo mengi kama vile, kuku wangu wanaharisha na wamezubaa, unasema kuku wangu wanaumwa kideri au mdondo. Kwa ujumla istilahi ni msamiati ambao hupambanua kile kinachotajwa kwa maneno machache.

Fifisha au kufifisha maana yake ni kufanya kitu kipoteze uasili wake wa mwanzo au kusababisha kitu kupoteza nguvu zake na kuonekana kuwa kitu hicho kimepitwa na wakati.

Kwa mfano kama msamiati ulitumika au kuanza kutumika kwa muda mrefu, halafu ukaja msamiati mwingine ambao unatumika badala yake na kupata matumizi ambayo yamesababisha msamiati wa awali kutotumika lakini bado msamiati huo wa awali upo kwenye kamusi za lugha, tunasema msamiati huo umefifia katika matumizi.

Baadhi ya msamiati/ istilahi ambazo matumizi yake yamefifia ni kama vile neno kombamwiko. Neno hili ukiwauliza baadhi ya watu maana yake wanaweza kukwambia ni maneno mawili yaliyounganishwa yaani komba na mwiko lakini kwa hakika neno hilo ni moja likirejelea mdudu ambaye kwa sasa hujulikana sana kwa jina la mende.

Huu ni mfano wa kufifia kwa matumizi ya neno hilo hasa kwa wakazi wa Tanzania kwa kuwa jirani zetu Wakenya wanalitumia neno hilo kumrejelea mdudu mende. Tunapozungumzia kuwa istilahi ni msamiati wa uwanja maalumu, tunamaanisha kuwa neno au msamiati wa Kiswahili unaweza kutumika kwa maana tofauti na ile iliyozoeleka kwenye mazingira tofauti.

Kwa mfano katika muktadha wa manahodha wa vyombo vya bahari ngamia ni kamba nene iliyosukwa imara kwa ajili ya kusaidia vyombo vya baharini kutia nanga.

Kamba hii ndiyo ambayo imenasibishwa na usemi wa Kiswahili usemao “Ni heri ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia mbinguni”.

Bila shaka wengi wamefaidika na ufafanuzi huu kwa kuwa nilijaribu kuwauliza baadhi ya watu kuhusu ngamia anayetajwa kwenye usemi huu na walijibu kuwa wao walidhani ni yule mnyama wa jangwani.

Katika istilahi za kilimo na ufugaji kule Kaskazini mwa Afrika ngamia ni mnyama ambaye hupatikana zaidi huko na atafahamika kuwa ni mnyama mkubwa wa kufugwa mwenye shingo ndefu, nundu kubwa na miguu mirefu yenye nyayo pana zisizo na kwato ambaye aghalabu hutumiwa katika safari za jangwani au utalii katika baadhi ya maeneo.

Namna ya kupata istilahi za Kiswahili Kiswahili kinaweza kuelezea jambo kwa kukidhi na kwa ukamilifu kwa kupitia njia nyingi. Msamiati au istilahi mbalimbali katika jamii hupatikana kwa namna nyingi kama itakavyobainishwa hapa chini.

Finyanzo ni njia mojawapo ya uundaji istilahi za Kiswahili kwa kuchukua sehemu ya neno na kuunganisha na neno jingine ili kuunda neno moja lenye maana inayokubalika katika uwanja fulani, kwa mfano istilahi hii ya chajio imetokana na kuchukua sehemu ya neno, cha - kula na kuungan isha sehemu ya neno ji-oni na kupata istilahi cha+jio, chemchemi ya maji moto = chemimoto, matuta kama ngazi = matungazi, teknolojia ya habari na mawasiliano =Tehama na mfupa wa paja = fupaja.

Muunganiko wa maneno ya Kiswahili ambayo yanaelezea dhana moja ni njia nyingine ya kutengeneza istilahi za Kiswahili, kwa mfano mwana + harakati tunapata neno mwanaharakati, mwendo + kasi tunapata mwendokasi na nishati + iliyotulia tunapata neno nishatituli.

Lugha za makabila ni chanzo kingine cha kupata istilahi za nyanja mbalimbali, utaratibu huu hutumika pale ambapo kugha za makabila ya Watanzania na lahaja za Kiswahili zimeshindwa kupata msamiati unaokidhi maana ya kinachotaka kutajwa. Mbinu hii huangalia neno la lugha za Kiafrika linalokidhi kinachotaka kurejelewa kwa neno moja badala ya kutumia maneno mengi.

Kwa mfano, neno kitivo ambalo limechukuliwa kutoka katika lugha ya Kipare likimaanisha sehemu ya shamba ambayo ina rutuba na maji ambayo yanawezesha mazao yanayooteshwa pale yawe na rutuba.

Mazao kama vile mpunga na magimbi hustawi vyema eneo la kitivo kwa sababu ya majimaji ambayo yanatuama hapo kwa muda mrefu, neno hili limechukuliwa na kuingizwa katika lugha ya Kiswahili kwa maana ya idara au muunganiko wa idara nyingi za fani moja kwenye vyuo vikuu au vya elimu ya juu.

Neno jingine ambalo limechukuliwa kwenye lugha za Kiafrika ni Bunge ambalo humaanisha baraza la wazee ambalo linakaa ili kuamua jambo la kijamii kutoka lugha ya Kigogo.

Utohozi ni mbinu nyingine ambayo maneno kutoka lugha fulani hutoholewa kutoka lugha hiyo na hatimaye hufanyiwa marekebisho kwa kufuata kaida au sheria za kifonolojia na kimofolojia za lugha inayopokea neno hilo kabla ya kutumiwa. Maneno yanapotoholewa hutamkwa na kuandikwa kwa utaratibu wa lugha hiyo iliyopokea maneno hayo.

Hata hivyo maana ya maneno yaliyotoholewa hubakia ileile ya awali. Kwa mfano neno shati limetoholewa kutoka neno la Kiingereza shirt, neno sketi limetoholewa kutoka katika lugha ya Kiingereza skirt. Kufifia kwa msamiati wa Kiswahili Kama ambavyo imeelezwa hapo juu lugha ya Kiswahili imejitahidi kutafuta msamiati wa kutosha ili kuweza kukamilisha mawasiliano katika jamii.

Katika juhudi za kuhakikisha jamii ya Waswahili inawasiliana vyema kumekuwa na juhudi za makusudi zilizofanywa ili jamii iweze kuwasiliana pasi na ku ruhusu utata. Kwa hivyo, ikafanyika juhudi ambayo imezalisha maneno mengi ya Kiswahili ambayo yanakidhi kile kinachotaka kusemwa au kitakachosemwa.

Baadhi ya misamiati hiyo ilipata mashiko katika matumizi na kushamiri kwa hivyo, ukiizungumza katika jamii, walio wengi au wote wanakuelewa baadhi ya misamiati hiyo ni kama vile kisimbuzi kwa maana ya kifaa kinachofichua alama za kielektroni zilizizofichwa ili ziweze kuonekana au kusikika kwenye televisheni, redio na simu, nywila neno au maneno ya siri yaliyoidhinishwa kwa ajili ya mtumiaji na arafa ujumbe mfupi wa maneno unaotumwa kwenye simu, kompyuta au kifaa kingine cha elektroni.

Baadhi ya misamia imefifishwa matumizi yake kwa sababu ambazo wakati mwingine unaweza kushindwa kuzieleza ijapokuwa sababu iliyo wazi ni ile ya mazoea ya kutumia visawe vya lugha nyingine kurejelea kile kinachotaka kusemwa.

Angalia mifano hii. Barakoa pengine in aandikwa barkoa - vazi au sanamu linalovaliwa usoni kwa ajili wa kuwachekesha au kuwafurahisha watu wakati wa sherehe fulani. Vazi linalovaliwa ili mtu kuficha uso wake kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe, kwa mfano kuzuia vimelea visipenye, kuzuia uso wako ili watu wengine wasikutambue.

Msamiati huu tunasema umefifia matumizi yake kwa kuwa neno la Kiingereza mask linatumika zaidi kurejelea barakoa ambayo ilitumiwa na inaendelea kutumiwa na baadhi ya jamii ya Waswahili, ingawa matumizi yamefifia.

Ni rahisi kueleweka unaposema wale wahalifu walikuwa wamevaa mask ili sura zao zisionekane na wengine siku hizi wanasema kinyago, kuliko barakoa ambalo ndilo neno sahihi.

Itaendelea

Mwandishi ni Mchunguzi Lugha Mwandamizi, Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita). Mawasiliano yake ni 0712747199/0757900894.

foto
Mwandishi: Mussa Kaoneka

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi