loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

VALENTINE: Siku ya kueneza upendo iliyogeuzwa kuwa ya ngono

FEBRUARI 14 ni siku ya arobaini na tano ya mwaka. Yaani zimebaki siku 321 kuumaliza mwaka huu. Hii ni tarehe waliyozaliwa watu mashuhuri kama Andrew C. McLaughlin, mwanahistoria kutoka Marekani aliyezaliwa mwaka 1861.

Wapo pia Charles Wilson, mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fizikia wa mwaka wa 1927, aliyezaliwa tarehe kama hii mwaka 1869; Herbert Hauptman, mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Kemia wa mwaka 1985 aliyezaliwa mwaka 1917.

Kwa upande wa Wakristo, walio wengi, wanafuata mapokeo ya Roma kwa kuadhimisha kumbukumbu za watakatifu Sirili na Methodi wa Thesalonike, Valentine, Vitalis wa Spoleto, Zenone wa Roma, Basiano na wenzake, Eleukadio, Ausenti abati, Antonino wa Sorrento, Yohana Mbatizaji n.k.

Februari 14 imefanywa kuwa siku ya kueneza upendo na amani. Yapo machapisho na vyanzo kadhaa vya historia ya siku hii vikionesha kuwa Februari 14 ni siku ya kumkumbuka Valentine, kijana aliyejitoa kwa ajili ya kueneza upendo na amani kabla hajauawa kwa sababu ya kusimamia imani ya dini yake.

Historia ya siku hii imeanzia karne ya tatu, enzi za utawala wa Kirumi chini ya Mfalme Claudius II, aliyeamini kuwa askari mkakamavu lazima awe kapera (asiyeoa), hasa wakati huo ambapo kulikuwa na vita katika taifa hilo.

Claudius alitegemea vijana wangejitolea na kujiunga na jeshi lake. Lakini vijana wengi hawakupenda vita kwa kuwa hawakutaka kuziacha familia zao na watoto wao.

Hivyo, Claudius akaona ili kuwakomesha vijana waingie jeshini ni kupiga marufuku ndoa kwa askari, akiamini kuwa askari mkakamavu na bora zaidi ni yule asiyeoa wala kuwa na familia. Kwa kufanya hivyo alitegemea vijana hawatajali sasa kujiunga na jeshi kwa sababu ya familia zao.

Tangazo la Claudius liliwahuzunisha sana mabinti na askari wa nchi hiyo ambao hawakuwa na wenza lakini wengi wao walipata faraja baada ya Valentine kupinga agizo la mfalme na kuamua kufungisha ndoa kwa siri.

Hata hivyo, taarifa za Valentine kukaidi agizo la mfalme zilimfikia Claudius, aliyeamuru kukamatwa kwa kijana huyo ili auawe. Kweli, Valentine alitiwa gerezani kabla hajahukumiwa adhabu ya kifo cha kunyongwa.

Wakati akiwa jela akisubiri siku yake ya kunyongwa Valentine alikuwa akitembelewa na vijana waliokuwa wakimpelekea maua kuonesha kuwa wanamuunga mkono.

Mmoja wa vijana waliokuwa wakienda kumtembelea ni binti wa mkuu wa gereza ambaye aliruhusiwa kuingia mpaka kwenye selo la Valentine “kupiga naye stori”.

Inasemekana kwamba Valentine aliangukia katika mapenzi na binti huyo wakati anasubiria kunyongwa. Muda mchache kabla hajanyongwa Valentine aliomba kalamu na karatasi na kuandika barua iliyokuwa na salamu za kwanza za Valentine kwa binti huyo; mwisho wa barua alihitimisha kwa maneno: Kutoka kwa Valentine wako. Valentine akanyongwa Februari 14, mwaka 270.

Tangu hapo Valentine anakumbukwa kama mtetezi wa wapendanao na sikukuu yake kuadhimishwa kote duniani. Baada ya kunyongwa kwa Valentine, vijana wa Roma walianza kumuiga Valentine na kuwaandikia na kuwatumia wanawake waliowapenda salamu za mapenzi na kumalizia barua zao kama ilivyokuwa kwa Valentine kwamba ‘kutoka kwa Valentine wako’.

Tangu siku hiyo tarehe hiyo ikaanza kuhusishwa na urafiki, upendo na mahaba huku ikihusishwa zaidi na mambo ya mapenzi. Tangu wakati huo, jamii ilianza kuadhimisha siku ya upendo kwa watu wote.

Kwa nchi zinazoendelea, mapokeo ya siku hiyo yalishamiri mwanzoni mwa miaka ya 1990 kwa namna tofauti ya usherehekeaji, ambapo wengi wao wameipotosha kabisa maana ya ‘Siku ya Wapendanao’ na kuifanya siku ya mapenzi ya wawili.

Siku hiyo imezidi kuwa maarufu kadri miaka inavyoenda huku kampuni mbalimbali zikiigeuza kuwa ya biashara zaidi kwa kufanya kila kitu maalumu kwa siku ya wapendanao kionekane kuwa chekundu kuanzia kadi za salamu, maua, mpaka nguo wavaazo wapendanao.

Kwa sasa, mwezi wa Februari umeonekana kuwa ‘mwezi wa mahaba’. Ni kipindi cha kuonesha upendo, hasa kwa adui zetu, pia ni wakati wa suluhu na amani kuanzia kwenye familia hadi jamii.

Kuna watu wengi pia ambao hawasherehekei siku hii kwa kuhoji umuhimu wa kuonesha kumjali umpendaye katika siku moja tu ya mwaka badala ya siku zote 365.

Wasioisherehekea siku hii wana mantiki, hasa ikizingatiwa kuwa siku hii imekuwa ni ya ‘uasherati zaidi’, huku tamaa za kimwili na kutaka kuonekana wa kisasa zaidi vikitawala. Washerehekeaji wakuu wa siku hii katika nchi za dunia ya tatu ni vijana, hasa walio kwenye balehe.

Kama ulitembelea maduka ya kadi, maua na zawadi siku chache kabla ya leo Februari 14, bila shaka umejionea pilikapilika za vijana wa kike na wa kiume wakitafuta maua, kadi na zawadi kwa ajili ya wapenzi wao.

Wanasahau kwamba siku hii ni maalumu kwa ajili ya upendo wa kiroho, kuungana na adui zetu, kuombana misamaha, kubadilishana zawadi na kupeana ujumbe na kadi za upendo na kuyasahau mabaya na chuki zilizopita.

Vijana wameigeuza siku hii na kuifanya kuwa maalumu kwa mavazi na mapambo ya rangi nyekundu. Wameifanya kuwa siku ya ngono, tena wakati mwingine ngono zembe.

Wengi huanzisha uhusiano mpya wa kimapenzi na kwa wenye ndoa ndiyo siku ya kutokomea kwenye nyumba ndogo na kwenda kwenye starehe na vimada. Kwa wazazi makini, hii ni siku ya kufahamu iwapo kijana wako ameanza uhusiano wa kimapenzi ama la, kwa sababu mwonekano wa furaha na uchangamfu katika mwili na sura yake utaongezeka.

Ningewashauri vijana, Februari 14 isiwatie ari ya kuingia katika maisha ya ndoa kwa kukurupuka. Si busara kuchochea mapenzi ya Siku ya Valentine kuwa mwanzo wa majuto baada ya kuambukizwa virusi vya ukimwi kwenye ngono zembe.

Kwa ajili ya kuwasaidia vijana, Warumi wa kale waliitumia sherehe hii kuandika majina ya wasichana waliofika umri wa kuolewa katika vikaratasi vidogo vilivyokunjwa mviringo, kisha vikaratasi hivyo vikawekwa katika chombo juu ya meza.

Baadaye wavulana waliotaka kuoa waliitwa na kila mmoja alichagua karatasi moja ikiwa na jina la msichana na kisha hujiambatanisha na huyo msichana aliyempata kutokana na kura aliyochagua kwa muda wa mwaka ili wajuane vizuri kabla ya kufunga ndoa, au kama hawakuelewana hurudia tena kufanya kura inapofika siku hiyo mwaka unaofatia.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya mapenzi wameeleza kuwa Siku ya Valentine kwa kiwango kikubwa inaongeza kasi ya maambukizi ya Ukimwi mijini na vijijini, hasa kwa vijana wa shule za sekondari.

Ni vyema kurudi kwenye mstari. Tujihadhari na tafsiri ovu tuliyoipandikiza vichwani mwetu kuhusu namna ya kuadhimisha siku hii. Tueneze upendo wa kiroho na amani kwa wengine wenye kuhitaji, hasa walemavu, yatima na wazee.

Ni siku ya kuwakumbuka waliotengwa, kwa sababu mbalimbali, tuwatembelee wafungwa na wagonjwa mahospitalini kuwaonesha upendo na kuwapa zawadi. Tunapaswa tubadilike na kufanya yale yaliyo mema na siyo kuambukizana maradhi na kudanganyana.

0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi