loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wahaya na mchakato wa kumtoa mwali

SHREHE za kumtoa mwali katika mila za Wahaya ni shughuli kubwa na kilele cha mchakato mzima wa kuanzisha maisha ya ndoa ya vijana.

Adriani Andrea, anaeleza kanuni za shughuli hii akisema: “Wazazi wa kijana huleta ‘lubisi’ ambayo ni pombe ya jadi; kwa jina maarufu huitwa Kalaile Katai -ikimaanisha: ‘kabinti ketu kameamkaje’ ambayo ni salamu ya kawaida kwa mama aliyejifungua.

Wazee wakiwa wamevaa kanzu, koti mabegani na wameshika mikuki yao mkononi, wakiambatana na wakina mama, huvaa vizuri pia wakiwa wamejifunika kwa shuka nyeupe hufika nyumbani kwa mwali majira ya machweo ya jua.

Msafara wao huwa wamebeba lubisi, vibuyu vitatu; na binti – ambaye ni mdogo wa kijana anayeoa, aliyebeba mundu - (aina ya panga lenye mpini mrefu), pamoja nao wanawake wawili waliobeba mgongoni watoto mmoja wa kike mwingine wa kiume. Sanduku la nguo atakayovaa bibi harusi hubebwa na dada wa kijana.

Kijana wao huja pamoja nao pia. Lengo la tukio hili ni kumtakia mwali maisha mema ya uzao katika maisha anayoingia. Wafikapo uwanjani, mbali kidogo kama ilivyo ada hutoa taarifa ya kuwasili kwao na kumngoja mjumbe kuwakaribisha ndani.

Msafara huingia ndani wakitanguliza vijana waliobeba kalaile katai, wakifuatiwa na wazee na akina mama na wote pamoja huku vigelegele maarufu cha Kihaya “iiii iiiii iiii iiii” na hoi hoi vikirindima kutokea ndani na wao kuitikia: “iiiiiiiiii….” Lubisi huwekwa sebuleni, na wazee huzunguka nguzo iliyotundikwa taa pembeni na kamba ya kupokea mikuki na kukita mikuki yao kwa pamoja; kina mama wakielekea ukumbi wa ndani kwa wenzao.

Kisha mshenga huinuka na kusalimia, akifutiwa na msafara mzima na mara hutoa taarifa ya zawadi aliyoleta na lengo la kufika kwao: ndio kumchukua mke wao.

Msemaji wa familia huwapokea na kuwakaribisha. Kisha huletewa ‘akamwani’, pombe iliyoandaliwa ndani na waliyoleta huingizwa ndani. Mazungumzo ya kawaida huendelea kwa muda huku wakiburudika na vinywaji na vyote vilivyoandaliwa, lakini si mlo (chakula). Mirindimo ya nyimbo na ngoma za asili huendelea hasa katika ukumbi wa akina mama.

Baada ya muda kiasi mshenga huomba kumwona mwali pamoja na alioambatana nao. Shangazi humleta mwali sebuleni hali amefunikwa pamoja na mpambe na kukalishwa kwenye mkeka.

Kijana hukaribishwa akisindikizwa na wimbo maarufu ‘Toina kumubona’ – yaani ‘Huwezi kumwona’ inaashiria atoe chochote ndipo aoneshwe/ au amfunue uso wa mchumba wake. Ni kitendo kiletacho bashasha na vifijo. Akishawamridhisha shangazi kwa kilichotolewa mwali hufunuliwa, na vigelegele vingi zaidi hupigwa. Kijana hurudi kwenye nafasi yake.

Wazazi wa binti huleta zawadi walizoandaa kwa ajili yake, pamoja na za jamaa wengine na kuvionesha kimoja baada ya kingine mbele ya umati. Wakwe watarajiwa pia huleta sanduku la nguo za bibi harusi kuhitimisha zoezi hilo.

Kisha mwali hurudishwa ndani. Baadhi ya zawadi hizo, hasa za matumizi ya nyumbani ya kawaida kama vile sufuria/chungu, visu, na kibuyu kikubwa kiasi chenye shingo ndefu kiitwacho ‘lushubu’ zilifungashwa na kuning’inizwa kwenye ‘mugamba’, ambao ni kama mtambaapanya/ mti maalumu ulionakshiwa vizuri ili vionekane.

“Lushubu humkumbusha binti anaporudi kutembea kwao asisahau kuleta lubisi kwa wazazi wake,” anasema Helena Amerika. Akiwa huko ndani wanawake huendelea na kughani mashairi ya aina aina. Enzi hizo alialikwa malenga mahiri wa kughani mashairi yenye kuasa na kufunda. Muundo wa ghani hizo uliambatana na wenzake kumwitikia kila amalizapo shairi moja.

Helena Amerika anasema usiku huo kimsingi, huwa maalumu kwa akinamama kumuaga rasmi binti yao. Walimfunda kwa jinsi ambayo wakati mwingine ilimtoa machozi, hasa ilipogusia magumu yanayoweza kumkuta, na jinsi ya kuyakabili.

Alifundwa kuwa itokeapo rabsha nyumbani humo, asitoke nje ya nyumba ila ikilazimu hasa kutokana na kipigo kisichovumilika, akimbilie ulipowekwa ‘mugamba’ na kusimama chini yake. Kimila, mume huzuiwa kuendelea kumpa kipigo mkewe akisijisalimisha mahali hapo, la sivyo atatakiwa kumlipa faini, maana kwa kitendo hicho - ‘kakimbilia kwao’.

Wazee sebuleni huendelea kubadilishana mazungumzo, wakati mwingine vikiwemo vijembe vya makusudi ili pia kufahamiana hata ustahimilivu. Hii ilisaidia kujuana kitabia hasa iwapo kutahitajika vikao vya suluhisho siku za usoni. Wakati mwingine alialikwa malenga wa zeze, aghalabu mwanaume ambaye pia alighani maudhui ya majigambo ya kijamii kama vile koo mbalimbali au watemi walivyopambana na wenzao.

Hatimaye mshenga alitokeza sebuleni na kuaga, na mara hiyo huongoza wenzake kuwaaga wazazi na jamaa wa mwali, huchukua mikuki yao na kurejea nyumbani. Warudipo nyumbani hutoa taarifa ya safari yao na sherehe huendelea huko ikiwa ni pamoja na chakula kilichoandaliwa rasmi.

Kwa binti nako sherehe huendelea usiku kucha na hasa akinamama wakimfunda binti kwa nasaha mahsusi za kumjenga katika maisha yake ya ndoa. Kuelekea muda wa alfajiri kabla ya mawio ya jua, binti huletwa kwa baba yake sebuleni na kutakiwa ampakate kama ilivyokuwa utotoni mwake.

Baba yake humpa nasaha zake kwa maudhui kama haya: ‘Binti wangu, nakutoa leo uende kuanza maisha yako, huko ndipo utakapokuta baba na mama zako, uwaheshimu na kuwahudumia kama ulivyoishi na sisi; urudipo hapa uje katika heri; kamwe usirudi viwiko vya mikono vikitazama nyuma ila siku zote vielekee mbele. “Uende na amani”.

Maneno haya huashiria binti aje na zawadi na siyo akiwa mikono nyuma! Anasema Mzee Pastori Mushumbusi. “Mara binti hurudishwa ndani kuandaliwa kumtoa. Huu ulikuwa wakati mgumu sana kwa binti maana alipakatwa na mama yake naye akimpa mawaidha ya ziada,” anasema Clara Pastori. Mkesha huo ulihitimishwa kwa kumtoa mwali nje ya nyumba.

Clara Pastori anasema: “Binti hali amefunikwa, husindikizwa na shangazi yake hadi kwenye viimo vya mlango na pale humkuta kaka yake na huweka mikono yake kwenye mabega yake na kuongozwa nje ya nyumba kwa mwendo wa taratibu, huku nyuma vigelegele na ghani vikirindima.”

Kaka humwongoza kupita uwanja wa mbele ya nyumba takriban mita hamsini mpaka mahali palipo kimti kidogo kilichooteshwa. Humshika mkono na kumtaka avunje sehemu ya juu ya kimti hicho au katawi kanakoweza kuvunjwa kabaki kananing’inia, akimwambia maneno yafuatayo: “Nakusindikiza uende ukaishi kwa mumeo; na kama ilivyo kwa tawi ulilovunja haliwezi tena kuinuka usirudi aslani nyumbani hapo, ila kwa heri na siyo kwa shari.” Kisha kaka hugeuka na kurudi nyumbani bila kugeuka nyuma.

Mwali husimama na mara huja dada wa mumewe na kumbeba mgongoni na hatua chache mbele, hupokewa na wasindikizaji wengine kutoka kwa bwana harusi. Bwana harusi huwepo karibu, lakini hana shughuli yoyote. Hutangulia nyumbani na wapambe wake kuandaa mapokezi. Mwali sasa hupelekwa hatua za hesabu, mwendo mdogo mdogo hadi mahali palipoandaliwa kusubiri muda wa kupokewa rasmi.

Baada ya kaka wa binti kurudi ndani, wasindikizaji wakibeba zawadi za bibi harusi ukiwemo mgamba huenda kujiunga na waliotumwa kumleta bibi harusi. Bibi harusi huingizwa ukumbini/viwanja vya mumewe mnamo alasiri. Bwana harusi huenda mahali alipopumzikia mkewe na kumchukua kuja mahali pa hadhara walipokusanyika jamaa na wageni waalikwa.

Hukaa mahali palipoandaliwa na shamrashamra huendelea, zikiwamo ghani na ngoma za asili, au miziki na keki kulingana na ratiba. Zama za sasa bibi harusi hupelekwa kwa msajili rasmi wa ndoa ikiwa ni kanisani, msikitini au bomani, na kisha kwenye kumbi za sherehe. Hata hivyo, sherehe bado hukamilishwa jioni.

Muda maalumu uliotengwa, kijana huinuka kuelekea kwa baba yake ili akabidhiwe mke rasmi. Baba humvika kanzu, na kumkabidhi mkuki, vikiwa ishara ya kumweka katika kundi la wazee.

“Anapompa mkuki huweza kusema maneno kama: ‘Mwanangu sasa umekua, na kuingia urika wa wazee. Nakukabidhi mkuki huu ikiwa alama ya kuwa msimamizi na mlinzi wa nyumba yako. Uwe hodari na shujaa katika kaya yako,” anaeleza Adrian Andrea. Sherehe huendelea kama ilivyoratibishwa ikiwemo kuwashika mkono/kuwapongeza maharusi.

Kuelekea jua kuzama, mawifi wa bibi harusi hutokea na kumbeba bibi harusi kumuingiza ndani ya nyumba chumbani mwake. Bwana harusi humfuatia punde na akishafika huko humfunua na kurudi ukumbini akiwa amebeba mkuki wake kumshukuru baba yake kwa kufanya majigambo. Majigambo ni utamaduni wa kutoa sifa na shukrani kwa ushindi na mafanikio.Sherehe ya harusi humalizika kwa tendo hilo.

Mwandishi ni msomaji na mchangiaji katika gazeti hili. Ni mwenyeji wa Mkoa wa Kagera na ni mwalimu mstaafu. Anapatikana kwa simu 0767547424.

foto
Mwandishi: Pontian Kashangaki

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi