loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ujenzi SGR wapata trilioni 3.3/-

SERIKALI ya Tanzania imesaini mkataba wa mkopo wa Sh trilioni 3.3 na wabia wa maendeleo 17 kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kuanzia Dar es Salaam hadi Makutupora, Dodoma.

Mkataba huo ulisainiwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwa niaba ya serikali ya Tanzania na Mkurugenzi wa Benki ya Standard Chartered, Sanjay Rughani kwa niaba ya wabia hao 17, ambao wengi wao wanapewa fedha kutoka mataifa ya Sweden na Denmark.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba wa mkopo huo, Dk Mpango alisema mradi wa SGR ni moja ya miradi mikubwa zaidi na ukikamilika utakuwa njia salama na ya kuaminika ya kusafirisha watu na mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Kanda ya Ziwa na nchi jirani.

“Kwa msaada wa Standard Chartered na washirika wetu, ufadhili wa mradi utaongeza juhudi za serikali katika kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji,” alisema.

SGR ikiwa na urefu wa kilomita 550, ni mradi muhimu unaounganisha Dar es Salaam na Dodoma kupitia Morogoro na Makutopora. Kwa mujibu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), kukamilika kwa njia hiyo kutapunguza changamoto ya usafirishaji mizigo na kupunguza gharama zake kwa asilimia 40.

Hiyo inatokana na ukweli kuwa treni hiyo, itabeba tani 10,000 ikiwa ni sawa na malori 500 kwa wakati mmoja. Aidha, reli hiyo itaunganisha Tanzania na mataifa jirani ya Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia na Congo (DRC).

Mradi huo tayari umezalisha kazi za moja kwa moja kwa watanzania 8,000 na kutoa fursa za kiuchumi kwa jamii zinazozunguka mradi kwa wakati huu, kwa kuwezesha chakula na makazi kwa wafanyakazi wa ujenzi wa reli hiyo. Mpango huo wa ukusanyaji wa raslimali fedha kupitia Standard Chartered Tanzania, ndio mpango mkubwa kuwezeshwa na Wizara ya fFedha na Mipango kwa sasa.

Dk Mpango alisema riba ya mkopo huo ni nzuri kulingana na viwango vilivyopo sokoni. Pia alisema bado deni la taifa ni himilivu. Alisema fedha za mradi huo, zitaanza kutoka wiki ijayo.

Dk Mpango alisema kwamba Watanzania hawatamuuliza kwa nini ujenzi wa SGR haujakamilika, kwani fedha zipo na sasa kazi yake ni kusimamia ujenzi huo. Alisema watoto na wajukuu watalipa deni hilo, ambalo lina faida kwao, kwani reli inadumu kwa zaidi ya miaka 200. Dk Mpango alizishukuru serikali za Sweden na Denmark, kwa kuwezesha taasisi kuchangia mkopo huo, chini ya usimamizi wa benki ya Standard Chartered. Katika utiaji saini huo, mabalozi wao nchini walikuwepo.

“Mataifa haya mawili, Sweden na Denmark, yameonyesha urafiki wa kweli, sio tu kwa maneno lakini pia kwa vitendo. Tafadhali pokeeni shukrani ya dhati za nchi yetu kwa wakala wa mikopo na wakopeshaji wengine katika nchi hizo ambao wameunga mkono mradi huu, kama nchi tunaheshimu ahadi zenu,” alisema Dk Mpango.

Taasisi nyingine alizozishukuru ni Benki ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (DBSA), Benki ya Biashara na Maendeleo (TDB) na Benki ya Export- Exter (Afrexim) kwa kuunga mkono mradi huo. Mkurugenzi wa Benki ya Standard Chartered, Sanjay Rughani alisema amefurahi kusaini mkataba huo wa uwekezaji Tanzania. Alisema benki yake imeonesha kukomaa katika soko la fedha kimataifa na imekuwa benki ya kwanza, kuandika historia hiyo kubwa.

“Kama Benki ya kimataifa inayoongoza Afrika, ikiwa na zaidi ya miaka 100 nchini Tanzania, ni muhimu sio tu kwa Chartered ya Standard lakini pia kwa wateja wetu na tunafurahi kufikia hatua hii kubwa hapa Tanzania, ya kufadhili mradi wa SGR ambao utaleta faida kubwa kwa Tanzania na kuunga mkono maono ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo 2025,” alisema Rughani.

Rughani aliongeza kuwa benki hiyo, itaendelea kuongeza mtandao wake wa kibenki na uaminifu, ambao umeijenga ili kuiweka Tanzania katika nafasi ya kuwa sehemu salama ya uwekezaji. Mkurugenzi Mtendaji wa Standard Chartered Afrika na Mashariki ya Kati, Sunil Kaushal, alisema kusainiwa kwa mkataba huo, kunaashiria faida ya uwezo wa mtandao usio na shaka wa benki yao.

“Wawekezaji wa jamii ya kimataifa wanatamani kuingia barani Afrika kuwekeza na asilimia 80 ya wateja wetu wa juu wa makampuni na taasisi wanaotumia mtandao wetu Afrika na Mashariki ya Kati kwa Standard Chartered, Afrika inabaki kuwa kipaumbele na tunajivunia kutumia utaalamu wetu kusaidia serikali ya Tanzania na fedha zinazohitajika kwa mradi wa SGR,” alisema.

Utiaji saini huo ilihudhuriwa pia na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Norgaard Dissing- Spandet, Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Anders Sjoberg, Balozi wa Italia, Robert Mengoni, Mkurugenzi wa Nchi Biashara ya Kimataifa kwa Ubalozi wa Uingereza, Calumm Mcallum, Meneja wa Nchi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dk Alex Mubiru na Mwakilishi wa Mkazi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) nchini Tanzania, Jens Reinke.

Pia ulihudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara wa Fedha na Mipango Doto James, Gavana wa Benki Kuu, Profesa Florence Luoga, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli la Tanzania, Masanja Kadogosa wajumbe wa bodi ya benki ya Standard Chartered Tanzania.

BEKI  wa zamani wa ...

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi