loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kesi ya Lugola, wenzake 18 yaiva

UCHUNGUZI dhidi ya vigogo wa Wizara ya Mambo ya Ndani, akiwamo aliyekuwa waziri Kangi Lugola na aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye, upo katika hatu za mwisho na watakaobainika kuwa na makosa, watapandishwa kizimbani wakati wowote kuanzia sasa.

Vigogo hao wapo katika uchunguzi, unaofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuhusu kashfa ya kuingia mkataba tata nje ya nchi wa ununuzi wa vifaa vya Idara ya Zimamoto na Uokoaji, wenye thamani ya Euro milioni 408 (Sh trilioni moja).

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Azam juzi, Kaimu Mkurugenzi wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo, alisema uchunguzi huo unaendelea vizuri na kwamba mafanikio makubwa yamepatikana hadi sasa.

Aidha, alisema idadi ya watu wanaochunguzwa kuhusiana na kashfa hiyo imeongezeka kutoka wawili (Lugola na Andengenye) hadi kufikia 19. “Idadi ya watumishi wa umma wanaochunguzwa kuhusiana na kashfa hiyo imeongezeka hadi kufikia 19, hata hivyo hatuwezi kuwataja kwa sasa ili kutoingilia uchunguzi.

“Uchunguzi wa tuhuma za jinai wakati mwingine unachukua muda mrefu, lakini kwa sasa tunaendelea vizuri na tumepata mafanikio makubwa. Wakati wowote tutaingia hatua nyingine,” alisema Kaimu Mkurugenzi huyo wa Takukuru.

Wakati Takukuru ikieleza hatua iliyofikia katika uchunguzi huo, gazeti hili linajua kuwa wafanyakazi sita wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, waliokuwa kwenye kamati ya utekelezaji wa makubaliano na Kampuni ya Rom Solutions Co. Ltd ya nchini Romania, wameshahojiwa na taasisi hiyo mjini Dodoma kuhusu kashfa hiyo, iliyovuta hisia za watu wengi.

Inadaiwa walipoenda nchini humo kwenye mazungumzo kuhusiana na mkataba huo, walipewa kompyuta mpakato (Laptop) na walilipwa Dola za Marekani 800 kwa kila kikao walichohudhuria na Kampuni ya Rom Solution.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Takukuru Februari 5, mwaka huu, waliokwishahojiwa hadi wakati huo ni Kamishna wa Zimamoto, Mbaraka Semwanza, Naibu Kamishna wa Zimamoto, Fikiri Salala, Naibu Kamishna wa Zimamoto, Lusekela Chaula, Naibu Kamishna wa Zimamoto, Ully Mburuko, Ofisa Ugavi Mkuu wa Zimamoto, Boniface Kipomela na Mchumi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Felis Mshana.

Wiki moja kabla ya hapo, Takukuru iliwahoji watendaji wa juu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Ramadhan Kailima na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni. Wengine waliohojiwa ni Lugola, aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu na Andengenye.

Vigogo na watendaji hao wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wanahojiwa na Takukuru kutokana na agizo la Rais Dk John Magufuli, kuhusu mkataba ulioingiwa na wizara hiyo, kununua vifaa vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kupitia kampuni ya Rom Solutions Co. Ltd. Kashfa hiyo ya mkataba wa kifisadi iliyomkumba Lugola, ilisababisha kujiuzulu kwenye nafasi yake ya uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Lugola ambaye ni Mbunge wa Mwibara, alichukua hatua hiyo kutokana na wizara hiyo kuingia mkataba huo wenye utata wa thamani ya zaidi ya Sh. 1 trilioni na kukopa mkopo, bila ruhusa ya Wizara ya Fedha na Mipango. Vigogo wengine wa wizara hiyo waliong’oka, kufuatia kashfa hiyo ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Kingu na Andengenye.

foto
Mwandishi: Abdallah Bawazir

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi